Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ametoa nafasi kwa Wadau wa Utalii nchini kuwa Uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii upo tayari kupokea ushauri, mapendekezo pamoja na mawazo mapya yatakayosaidia kuchochea na kuinua idadi ya watalii wa ndani.
Pia, Amewataka watu binafsi, mashirika pamoja na Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kutaka kuwekeza kwenye sekta ya utalii wasisite ofisi yake ipo wazi kwa mtu yeyote.
"Kwa yeyote atakayetaka kuniona kwa ajili ya kukuza na kuendeleza utalii hasa utalii wa ndani kwangu Mimi pamoja Waziri milango ipo wazi muda wote" alisisitiza Kanyasu.
Hayo ameyasema wakati alipokuwa akizungumza na Watalii wa ndani wapatao 200 kutoka jijini Dar es Salaam ambao walitembelea katika Msitu Asilia wa Magoroto katika wilaya ya Handeni mkoani Tanga kwa ajili ya kutalii ndani ya msitu wenye kila aina ya vivutio vya utalii likiwemo ziwa la kutengenezwa.
Kundi hilo la watalii wa ndani liliratibiwa na Kampuni ya Dalida Tours and Travel Agency kupitia chini ya Usimamizi wa Mratibu wa safari hiyo , Emma David.
Mhe. Kanyasu amesema moja ya mkakati wa Wizara ni kutaka watalii wa ndani wawe namba moja kwa kutembelea vivutio vya utalii badala ya kutegemea Watalii wa kutoka nje kama ilivyo sasa.
Aidha, Mhe.Kanyasu amesema pia Wizara yake ipo tayari kupokea na kutoa msaada wa hali na mali kwa mtu au kikundi cha watu kitakacholenga kuhamasisha utalii wa ndani.
''Tunataka akili mpya na mawazo mapya ya namna ya kusukuma na kujenga utamaduni wa watu wetu Wawe wa kwanza kutalii kama ilivyo kwa China'' Alisisitiza Kanyasu
Ameongeza kuwa Idadi ya watalii wa ndani hairidhishi hivyo kunahitajika mkakati wa pamoja katika kuhamasisha utalii wa ndani kwa Watanzania ili waweze kutembelea vivutio hivyo.
Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amesema kama nchi haiwezi kuifanya sekta ya utalii kama injini ya uchumi endapo Wazawa wenyewe wataendelea kuwa nyuma huku utalii wa ndani ukiwa na mwitikio mdogo.
" Kama taifa na kwa Mwananchi mmoja mmoja bado hatujaitendea hali sekta ya Utalii ni sekta ambayo haijaguswa hata kidogo ni lazima wananchi wawekeze na wakati huo huo wananchi watembelee vivutio vya Utalii.Amesisitiza Kanyasu
Naye, Emma David ambaye ni Mratibu wa kundi hilo la watalii wa ndani amesema wamejipanga kuhamasisha idadi kubwa zaidi ya watalii wa ndani kwa kupitia mitandao ya kijamii ili waweze kutembelea vivutio mbalimbali vilivyoppo nchini.
''Sisi tumejipanga kutembelea mikoa yote lengo letu ni kuunga mkono jitihada za Wizara katika kuhamasisha Utalii wa ndani, Alisisitiza Emma.
Aidha, Ameishukuru Wizara kwa jitihada inazozifanya za kutengeneza mazingira rafiki kwa watu wenye nia ya kutaka kuwekeza kwenye utalii wa ndani.
Naye, Meneja wa Magoroto, Jeremia Mchechu amesema mwitikio wa wa watalii kutoka ndani na nje ya nchi umekuwa mkubwa tangu walipoanzisha eneo hilo kama kivutio cha Utalii na eneo la ziwa ambalo ni la kutengeneza limekuwa kivutio kikubwa cha Utalii.
Amesema watalii wengi wanaofaika katika eneo hilo wamekuwa wakipendelea kupanda milima, kuapnda baiskeli milimani pamoja na kutembelea vijijini kwa ajili ya kujifunza tamaduni ya wakazi wa Tanga.
0 comments:
Post a Comment