Monday, 1 July 2019

Maamuzi ya IGP Sirro na IGP wa Msumbiji kuhusu mauaji ya Watanzania 10

...
Mkuu  wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amekutana na kufanya mazungumzo ya kina na Mkuu wa Jeshi la Polisi wa nchi ya Msumbiji, Bernardino Rafael kuhusu mauaji ya Watanzania 10 yaliyotokea Juni 26, mwaka huu, katika kijiji cha Mtole nchini Msumbiji.

Watanzania hao waliuawa kwa kupigwa risasi na wengine kushambuliwa kwa mapanga katika kijiji hicho kilichopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji pembezoni mwa mto Ruvuma, ambapo mkuu huyo wa jeshi la Msumbiji amekiri kuwepo kwa wahalifu nchini mwake.

Baada ya kikao hicho, IGP Sirro aliwaambia waandishi wa habari mjini Mtwara kuwa kwa pamoja wameweka mikakati ili kuhakikisha kuwa matukio kama hayo hayatokei tena, kwa lengo la kuendelea kukuza uhusiano na ujirani mwema baina ya mataifa hayo mawili.

Kikao hicho kilikuwa na lengo la kuweka mikakati ya pamoja kati ya nchi hizi mbili na kuweza kupambana na wahalifu, wanaofanya vitendo vya kuwatia hofu wananchi wa nchi zetu hizi mbili.

“Kama nilivyowaambia jana kuwa IGP wa Msumbiji atakuja tukae pamoja na tupange mikakati ya kuweza kupambana na hawa wahalifu wanaotusumbua Watanzania, lakini pia wanawasumbua watu wa Msumbiji,” alisema IGP Sirro.

Alisema katika kikao hicho wamekubaliana mambo yanayoweza kufanyika katika kukabiliana na wahalifu, ambao siku zote huwa hawana mipaka kwa hiyo isiwe sababu ya kuzifanya nchini hizi mbili kushindwa kupambana nao.

“Ili kukabiliana na uhalifu wa kuvuka mipaka ni lazima kuwe na ushirikiano wa nchi hizi mbili na kikubwa ni kubadilishana taarifa na kufanya doria za pamoja ili kundi hili la watu wachache ambao wamekuwa wakisumbua na kufanya uhalifu kwa watanzania watiwe mbaroni na sheria ziweze kuchukua mkondo wake na kuleta majibu yaliyokuwa sahihi.

“Hivyo tumeweka mikakati ya kuhakikisha wale wote waliohusika na mauaji ya Watanzania na watu wa Msumbiji wanakamatwa haraka sana na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.”


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger