Wednesday 17 July 2019

Kanyasu Awashauri Wakulima Wa Pamba Wasiuze Pamba Kwa Walanguzi

...
Mbunge wa Geita mjini ambaye pia ni  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amewashauri  Wakulima wa zao la pamba wawe wavumilivu badala ya kuuza pamba hiyo kwa walanguzi kwa bei ya chini  huku Serikali ikiendelea kuwatafutia soko zuri.

Amesema Serikali ilishaahidi kuwa kama pamba hiyo haitanunuliwa  kwa bei elekezi ya kilo moja kwa shilingi 800 hadi mwezi Agosti mwaka huu basi Serikali itainunua pamba hiyo ili kuwafidia wakulima hao.

Hatua  hiyo inakuja kufuatia Wafanyabiashara wengi  kushindwa kununua kwa bei hiyo  kutokana bei ya soko la pamba duniani kuporoka.

Akizungumza kwenye mkutano uliofanyika katika eneo la Kasamwa mkoani Geita, Mhe.Kanyasu amesema   wafanyabiashara wameshindwa  kukopa pesa benki kwa ajili ya kuinunua pamba hiyo kutokana na kukosekana kwa soko la kuiuza.

Mhe.Kanyasu amesema kufuatia hali hiyo baadhi ya wakulima wamekuwa wakiiuza pamba hiyo kwa shilingi 500 kwa kilo moja kwa walanguzi hali inayowadidimiza kiuchumi.

Ametaja mikakati ambayo tayari Serikali imeshaichukua ikiwemo kuzungumza na Serikali ya Vietnam ambao tayari wameonesha nia ya kununua pamba hiyo kwa Wakulima.

Aidha, Mhe Kanyasu amewaeleza Wakulima hao kuwa Waziri wa Kilimo anatambua tatizo hilo na ameahidi kutembelea mkoa huo kwa ajili ya kuzungumza na Wakulima hao.

Naye Juma Kaludushi ambaye ni mkulima wa zao pamba amesema wakulima walio wengi akiwemo na yeye wamekuwa wakiuza pamba hiyo kwa walanguzi kwa bei ya chini kwa hofu kuwa pamba hiyo itaharibika mikononi mwao.

"Pamba ipo majumbani mwetu muda unakwenda bora tuuze tu kwa Walanguzi ili isiharibike kuliko tukapata hasara kabisa" Amesema Mkulima huyo.

Kwa upande wake, Ester Nalamo, ambaye ni Mkulima wa pamba amesema  amelazimika kuuza pamba  kwa bei ya chini ili aweze kuwalipia ada watoto wake kwa vile yeye hana chanzo kingine cha mapato zaidi ya kuuza pamba.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger