Thursday, 25 July 2019

DC Lengai Ole Sabaya Akana Tuhuma za Kuomba Rushwa kwa Mfanyabiashara

...
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, ametoa ufafanuzi kuhusu kipande cha video kinachosambaa kwenye mitandao ya kijamii, akituhumiwa kuomba rushwa kwa mfanyabiashara na mmiliki wa Hoteli ya Kitalii ya Weruweru River wilayani huko.

Akizungumzia video hiyo katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Ole Sabaya alisema kiini cha kusambazwa kwake ni uamuzi wake wa kumwondoa mfanyabiashara huyo kwenye eneo la ardhi analodaiwa kumpoka mjane, Mary Diriwa (86).

Kipande cha video hiyo kilianza kusambaa juzi kikimwonyesha mfanyabiashara Curthebert Swai, akidai kuombwa rushwa na kiongozi huyo wa wilaya.

Akijibu tuhuma hizo jana akiwa kwenye ardhi ya mjane anayedaiwa kupokwa eneo la ekari moja na robo na mwekezaji huyo, Ole Sabaya alisema: "Na ninyi waandishi wa habari mnanipigia simu kuniuliza juu ya hiyo 'clip' (kipande cha video), mkitaka maelezo yake chanzo chake ndiyo hiki.

"Kwenye taarifa yake, mliyoiona hiyo clip inayozunguka huko, inazungumzia mtu aliyemwomba pesa ya rushwa mara nne, mara ya kwanza, mara ya pili, mara ya tatu na mara ya nne na akisema kwenye hiyo clip kwamba huyu mtu najua siyo, Rais amemtuma.

"Lakini kuna vyombo vya dola hapa, kuna Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) Wilaya, kuna Takukuru Mkoa na unajua huyo mtu anafanya kwa matakwa yake na toka mwezi wa 11, 2018, leo ndiyo unakuja kuchukua hatua uliyoombwa rushwa, baada ya kuchukua mali za hawa kina bibi.

"Kuna 'clip' mnaipeleka huko duniani, anasema kwa mazingira hayo ametishiwa usalama, usalama umetishiwa kwa sababu na yeye ametishia usalama wa wanyonge, kwa hiyo OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya-Lwelwe Mpina), nakuelekeza kwa sababu na yeye ametoa tuhuma zake hizo akijua kabisa leo (jana) nilikuwa nakuja kufanya uamuzi hapa na ana taarifa hiyo na hata taarifa ya mkutano huu anayo kwamba nitakuja leo tarehe hii."

Akiwa katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Kimashuku, Kata ya Mnadani, Wilayani Hai, Mkuu huyo wa Wilaya amemwagiza Mkuu wa Polisi wa Hai, Lwelwe Mpina, kumhakikishia usalama mfanyabiashara huyo ili haki yake naye itendeke wakati vyombo vya dola vikifuatilia ukweli wa madai yake.

"Kwa hiyo kwanza OCD, fanya hivi mhakikishie Curthebert Swai usalama wake mwenyewe na kwa kuwa wewe ndiyo chombo cha kuhakikisha usalama wake na wewe ili wawe salama," alisema.

"Bibi (mjane aliyedai kunyang'anywa eneo lake), kuanzia tarehe ya leo, tutakuandikia barua, eneo hili ni la kwako na mtu yeyote haruhusiwi kuingilia.

"Zile fedha Sh. milioni 16.3 mlizopatiwa na upinzani kwa ajili ya kusaidia kuandikisha wapigakura wao mngezitumia kuwasaidia watu wanyonge badala ya kuzitumia kuzitumia kunyanyasa wanyonge kama bibi huyu mjane."

Swai akizungumza katika mkutano na TRA, alidai mkuu huyo wa wilaya amekuwa ni kikwazo kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

Alisema licha ya kulipa kodi serikalini, kiasi cha Sh milioni 148 kwa mwaka, lakini amekuwa akipokea vitisho na manyanyaso kutoka kwa mkuu huyo wa wilaya na kumlazimisha kumpa fedha.

Alidai mara kwa mara Sabaya amekuwa akivamia katika hoteli yake ya kitalii ya Weruweru River Lodge usiku kwa madai kuwa anakusanya kodi.

Swai alisema Sabaya akiwakuta wafanyakazi na wakashindwa kumpa majibu, huwachukua na kuwaweka mahabusu bila sababu za msingi.

“Amekuwa akija usiku hotelini na ile ni hoteli ya kitalii na alipomkuta meneja na akimuuliza maswali akashindwa kumjibu maana siyo kazi yake, alimchukua na kumweka ndani na kumtoa asubuhi, nilipomfuata kufahamu shida nini, alisema anataka Sh milioni tano, ametumwa na anafanya kazi ya Serikali,” alidai.

Swai alidai kuwa Sabaya alimweleza kwamba anaweza kuitafsiri kauli hiyo kama ni sawa na ya mkuu mmoja wa mkoa nchini ama rushwa.


“Alisema anahitaji hiyo fedha na anaripoti moja kwa moja juu.
Nilimpa milioni mbili, lakini bado alininyanyasa, na nilimfuata mfanyabiashara mwenzangu kuomba ushauri, alinishauri nimpe tu hizo fedha na kuniambia nikicheza na mjinga atanipasua jicho,” alidai.

Alidai baada ya kumpa fedha hizo, alikuja tena na kumpa milioni mbili kwa mara ya pili na mara ya tatu milioni mbili na akarudi tena kuvamia hoteli hiyo na kufanya fujo huku akiambatana na walinzi wake wawili.

“Nimesema haya nikiwa sijui hatima yangu itakuwaje, lakini mpaka sasa nimeshampa Sh milioni 10 na alikuja na kufanya fujo ambapo nilikuwa na mteja wangu mwenye wafuasi zaidi ya elfu 30,000, alimsumbua sana,” alidai.

Alidai mbali na hilo, alikuwa akiwachukua wasanii wa kucheza na nyoka kutoka Kanda ya Ziwa na kuwaleta hotelini hapo na kuwalipa, lakini Sabaya alikwenda na kuwafukuza huku wakiwa wameingia makubaliano ya kufungua bustani ya nyoka (snake park).

“Sijui hatima yangu itakuwa nini lakini nimeamua kuzungumza kwamba tunanyanyaswa tena sana, hatuna amani na kitakachonipata ni yeye, lakini sifikirii kama hata Rais anaweza kukubaliana na jambo kama hili, sisi tunalipa kodi ya Serikali na hatudaiwi kwanini tuteseke?” alisema.



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger