Ni vita ya maneno ya hoja kati ya Mchungaji Peter Msigwa na Askofu Mstaafu Donald Mtetemela Mjumbe
wa Bunge la Katiba, Mchungaji Petaer Msigwa amemvaa Askofu Donald
Mtetemela na kumtaka avae rasmi magwanda ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na gazeti hili, Msigwa
ambaye pia ni Mbunge kupitia Chadema alisema Askofu Mtetemela alionyesha
upendeleo wa wazi kwa CCM alipokuwa akichangia bungeni mjini Dodoma
Alhamisi iliyopita.
Katika mchango wake, Askofu Mtetemela
alikemea tabia ya wajumbe wa Bunge hilo kuwakashifu waasisi wa Taifa
aliosema wana heshima kubwa kwa jamii na mbele za Mungu.
Hata hivyo, Msigwa alisema:“ Askofu
ameonyesha upendeleo wa wazi wazi japokuwa anasema anasimamia katikati
(hana upande kisiasa). Hakuona kejeli, ubaguzi na matusi yaliyokuwa
yakiendelea ndani ya Bunge?”
Mchungaji Msigwa alisema yeye ni
mchungaji lakini amejitokeza wazi kusimamia Chadema tofauti na askofu
huyo ambaye ameonyesha wazi upande anaousimamia wa CCM, wakati awali
walidhani ni mtu mwenye msimamo wa kati.
“Mimi sina ugomvi kama ameamua kuwa
mwanasiasa kama mimi lakini awe wazi kwa kusimama na kujionyesha wazi
upande aliopo,”alisema.
Kauli ya Askofu Mtetemela
Katika mchango wake, Askofu Mtetemela
alilieleza kukerwa na kauli ya Profesa Lipumba kuliita Bunge la Maalum
la Katiba kuwa linafanana na kundi ovu la Italahamwe.
“Nasikitika kwamba sijaweza kumuona yeye
binafsi Profesa Lipumba ili niweze kumwambia masikitiko yangu, na
naamini ni masikitiko ya wengine. Mshtuko wangu ni kwamba alilinganisha
Bunge hili na kundi la Intarahamwe la Rwanda,” alisema.
Alibainisha kwamba kihistoria
inajulikana Intarahamwe ni wauaji, hivyo sio busara kabisa kuwafananisha
wajumbe wa Bunge Maalumu na kundi hilo.
“Hatuko hapa kumuua mtu yeyote, kutuita
sisi wauaji si jambo jema, ni baya lakini pia kauli hiyo inaweza kufufua
maumivu ya wenzetu wa Rwanda ambao hawataki hali hiyo ijirudie tena
katika nchi yao,” alisema.
Alieleza kuwa kauli hiyo pia inaweza
kuibua hisia tofauti hata kwa Serikali ya Rwanda inayoweza kufikiri kuwa
Tanzania inalifanyia mzaha jambo lililowaumiza kwa kiasi kikubwa.
-mwananchi
0 comments:
Post a Comment