Tuesday, 22 April 2014

MAASKOFU WATIA NENO BUNGE LA KATIBA

...
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

MAASKOFU wa Madhehebu ya Kikristo mkoani hapa wamelionya  bunge la katiba na kuwataka wajumbe wake kuzingatia mahitaji ya wananchi wakati wa kuandika katiba mpya.
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa.
Viongozi hao walikuwa wakitoa salama za Sikukuu ya Pasaka iliyofanyika Jumapili iliyopita duniani kote.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdenburg Mdegela alisema kuwa Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) warudi bungeni kuendelea na mjadala wa katiba na wasiende kwa wananchi.
Akitoa salamu za Sikukuu ya Pasaka kwenye ibada ya pili katika kanisa kuu la KKKT, Dk. Mdegela alisema kwa hali iliyofikia ni vema Ukawa wakarudi bungeni na si kwenda kwa wananchi kwa kuwa wameona kila kitu kinachoendelea bungeni.
“Ukawa warudi bungeni au wanyamaze kimya la sivyo tutaandamana nchi nzima tukipiga madebe na sufuria kuwapinga,” alisema na kuongeza kuwa ni vema wananchi wakamkataa yeyote anayetaka kuivunja amani ya nchi bila kujali itikadi za dini wala siasa.
Alisema wabunge wa bunge la katiba wanaodharauliana, kuchukiana, kubaguana, kuoneana wivu na kuona wenzao kuwa hawana maana na uwezo wa kuchangia mbele ya jamii wajiuzuru na kurudi nyumbani badala ya kuendelea kutumia mabilioni ya Watanzania Dodoma.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdenburg Mdegela.
Alisema hana imani na Bunge la Katiba linaloendelea kwakuwa linakwenda ovyoovyo na huenda wakaleta katiba ya ovyoovyo, akaongeza ni afadhali kuwa na serikali moja ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuwa wanaotaka muundo wa serikali tatu ni walafi na wanataka kuirudisha nchi nyuma kimaendeleo.
Alisema mambo yanayotakiwa kujadiliwa na aliyotegemea yangepewa kipaumbele katika Bunge la Katiba ni pamoja na umaskini, huduma za jamii na kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri na kufikia hata 20 badala ya kuwa na zaidi ya 60.
Naye Askofu Tarricisius Ngalalekumtwa akitoa salamu za Pasaka kwa waumini wa Katoliki alisema Watanzania wahubiri amani na kuacha chuki, fitina na kudharauliana kwa kuwa nchi ya Tanzania ni moja na ni ya watu wote .
Alisema wabunge wa Bunge la Katiba linaloendelea wanatakiwa kujadili masuala ya msingi kwa Watanzania ikiwemo umaskini, huduma za jamii na maendeleo mambo ambayo yanatija kwa maisha ya kila siku.
Alisema tayari makundi yote yanaliyoibuka bungeni lile la wanaotetea serikali mbili na hata hili la serikali tatu yote yanamapungufu, hivyo si busara kuendelea na mchakato wa katiba mpya na bunge la aina hiyo.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger