Sunday, 1 May 2022

HUYU NDIYO BILIONEA ALIYEUNUNUA MTANDAO WA TWITTER KWA FEDHA ZA KUFURU

...

Elon Musk.

MIONGONI mwa habari zilizoshtua Dunia mapema wiki hii ni kuhusu mtu anayeitwa Elon Musk kuununua Mtandao wa Twitter kwa pesa za kufuru.

Amefikia makubaliano ya kuinunua Twitter kwa pesa taslim Dola za Kimarekani bilioni 44.Wengi wameshtushwa na kiasi hicho cha pesa hivyo kujiuliza huyu Elon Musk ni nani hasa?


Huyu ni mtu tajiri mno duniani ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tesla inayotengeneza magari ya umeme yaliyopata soko kubwa kwa sasa duniani.

Mei 30, 2020 ilikuwa ni siku ya kukumbukwa katika historia ya sayansi ya anga, astronomy duniani kote na hiyo ilikuwa ni baada ya kufanikiwa kwa chombo maalum kiitwacho Falcon 9 kuwapeleka salama wanasayansi wawili, Doug Hurley na Bob Behnken kwenda kwenye kituo cha anga cha kimataifa, International Space Station.



Waliowezesha safari hiyo ya kihistoria, ni kampuni ya Space X inayomilikiwa na Elon Musk! Ndiyo, Elon Musk, mfalme wa sayansi ya kizazi kipya.



Sasa; kwa nini Elon Musk anatukuzwa kama mfalme wa sayansi ya kizazi kipya? Kwa taarifa yako, jamaa anatisha kwelikweli kwenye ubunifu wa hali ya juu wa kisayansi, pengine kuliko binadamu mwingine yeyote aliyewahi kuishi duniani.

Falsafa kuu ambayo imekuwa ikimuongoza, ni kuibadili Dunia na hiyo imemfanya kutajwa kuwa miongoni mwa watu wachache wenye akili, wanaoishi katika karne ya 21.

Amezaliwa Juni 28, 1971 kutoka kwa baba yake, Errol Musk, mhandisi na tajiri mkubwa kwa wakati huo, raia wa Afrika Kusini na mama Maye Musk, mwanamitindo mwenye asili ya Canada, alipewa jina la Elon Reev Musk FSR.

Hiyo ilikuwa ni Pretoria nchini Afrika Kusini, ambako baba yake alikuwa akifanya kazi za uhandisi wa vifaa vya kielektroniki, rubani na nahodha. Hapo ndipo safari ya maisha ya Musk ilipoanza, akilelewa pamoja na kaka yake, Kimbal na dada yake, Tosca.

Katika umri wake wa utoto, inaelezwa kwamba Musk alikuwa akipenda kucheza peke yake, akiwa kimya kabisa kiasi kwamba kuna wakati wazazi wake walihisi kwamba pengine alikuwa na matatizo ya kusikia, akapelekwa kwa daktari kufanyiwa uchunguzi lakini hakubainika kuwa na tatizo lolote.


Alianza shule, lakini akakutana na changamoto nyingine! Licha ya uwezo wake mkubwa darasani, Musk alikuwa na umbo dogo kuliko watoto wengine wa umri wake, alikuwa mkimya na alipenda kujisomea vitabu, jambo lililosababisha awe anaonewa.

Wakati f’lani amewahi kupigwa na kundi la watoto wenzake, wakamsukumia kwenye ngazi alikoporomoka na baadaye kupoteza fahamu.


Alipofikisha umri wa miaka 10, wazazi wake walitengana, akachukuliwa na mama yake na kwenda nchini Canada.

Ni katika kipindi hicho, alianza kuonesha mapenzi kwenye elimu ya kompyuta, akawa anajifunza mwenyewe mambo mbalimbali ikiwemo programming na alipofikisha umri wa miaka 12, tayari alikuwa na uwezo wa kutengeneza program mbalimbali za kompyuta.


Akafanikiwa kutengeneza gemu akiwa na umri wa miaka 12 na kuvunja rekodi ya mtaalam wa kompyuta mwenye umri mdogo zaidi baada ya kugundua video-game iliyopewa jina Blastar.


Alipofikisha miaka 15, alichoshwa na uonevu wa wanafunzi wenzake, akaamua kuanza kujifunza kareti na miereka, sasa akaanza kuwa tishio miongoni mwa waliokuwa wakimuonea.


Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Queen’s University. Miaka mitatu baadaye, alihamia nchini Marekani alikokwenda kujiunga na Chuo Kikuu cha Pennsylvania ambako alifanikiwa kuhitimu masomo ya Fizikia (Physics) na biashara.


Hizo ndizo zilizokuwa ndoto za Musk, kwenda kusoma Marekani. Baada ya kuhitimu Chuo Kikuu cha Pennsylvania, alijiunga na Chuo Kikuu cha Stanford, nacho cha Marekani, lakini baadaye aliamua kuachana na masomo ya chuo ili atimize ndoto kubwa zaidi.


Inaelezwa kwamba kipindi anaacha chuo, tayari alikuwa amefungua kampuni yake ya Zip2 Corporation kwa kushirikiana na kaka yake na hakuacha chuo ili akazurure, aliacha ili apate muda wa kuisimamia kampuni hiyo.


Kampuni aliyoifungua na kaka yake, Zip2 Corporation, ilikuwa ni maalum kwa ajili ya kuwezesha malipo ya kimtandao! Ni katika kipindi hicho cha mwishoni mwa miaka ya tisini, ndipo matumizi ya kompyuta yalipoongezeka.


Watu wengi walikuwa wakitaka kununua vitu mtandaoni na hakukuwa na mfumo ambao ungerahisisha kazi hiyo, lakini kwa Elon Musk na kaka yake ilikuwa ni fursa ya kupiga pesa.


Hilo lilifanikiwa kwa sababu Kampuni ya Zip2 iliwezesha wateja kuwa na uwezo wa kulipia bidhaa mbalimbali mtandaoni, jamaa wakaanza kuogelea kwenye utajiri ndani ya muda mfupi.


Baadaye Elon Musk aliamua kuuza hisa zake katika Kampuni ya Zip2, pesa alizozipata akaanzisha kampuni nyingine ambayo ilikuwa ikihusika na miamala ya kielektroniki, X.com.


Kampuni hiyo ilikuja kubadilisha mfumo wa utendaji kazi na jina na hapo ndipo ilipozaliwa PayPal; mtandao mashuhuri duniani wa kufanya manunuzi.

Jamaa aliendelea kutengeneza pesa ndefu, baadaye akaja kuiuza PayPal kwa kampuni nyingine kubwa, eBay kwa gharama ya Dola za Kimarekani, bilioni 1.5 (zaidi ya shilingi trilioni 3.5 za Kitanzania).


Inaelezwa kwamba mkwanja huo sasa ulimpa nguvu Musk ya kuibadili dunia kadiri awezavyo na hapo ndipo miradi mikubwa ya mabilioni ya pesa yalipoanza kutekelezwa, ikiwemo kutengeneza roketi, kurisha satelite, kutengeneza magari ya umeme na kufuru nyingine nyingi anazoendelea kuzifanya.

Mwaka 2002, Elon alianzisha kampuni nyingine ya SpaceX, ambayo mwanzo wa makala haya nimekueleza kwamba ndiyo iliyofanikisha safari ya kwanza binafsi kwenda kwenye kituo cha anga za juu cha kimataifa, International Space Station.


Pia mwaka 2003, Musk alianzisha kampuni nyingine ya Tesla Motors ambayo baadaye ilibadilishwa na kuwa Tesla Inc. Kwa taarifa yako, kampuni hii ni miongoni mwa kampuni zinazoongoza kwa ugunduzi wa teknolojia mpya duniani.

Tesla ndiyo waliogundua magari ya kisasa yanayotumia umeme, ndiyo waliogundua magari yanayojiendesha bila dereva, ndiyo waliogundua treni yenye kasi ya ajabu, Hyperloop na mengine mengi.


Ni Elon Musk huyu ndiye ambaye baada ya kuchoshwa na foleni za magari kwenye miji mikubwa, alikuja na wazo jipya, la kutengeneza barabara za chini ya ardhi, kupitia kwa kampuni yake ya The Boring Company.

Bila shaka sasa umeanza kumuelewa Elon Musk, lakini hiyo ni kama tone tu ndani ya bahari, ana mengi.

Sasa; jamaa ameinunua Twitter na anasema anataka kuona Twitter ina uwezo wake wa ajabu na hata hataki kutengeneza pesa kwa njia ya Twitter. Anazo za kutosha tayari na anaweza kuwa na vipaumbele tofauti vingine vya kumpatia pesa.

Makala; Hash Power na Mtandao
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger