Monday, 12 December 2016

Sheikh Ponda Amtembelea Godbless Lema Gerezani,Lema Aandika Barua Nzito Akiwa Gerezani

...


Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda amemtembelea Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema katika Gereza Kuu la Mkoa wa Arusha la Kisongo. 
Kwa mujibu wa Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), Noel Olevaroya, Sheikh Ponda alizungumza na Lema kwa muda usiopungua saa moja. 

“Sheikh Ponda amekutana na Mbunge wetu Lema na amekuja mahususi kumjulia hali na amemuambia hampi pole bali anampongeza kwa kukaa mahabusu muda wote licha ya kuamini anastahili kupata dhamana,” alisema Olevaroya. 
Alisema katika mazungumzo yake alimtaka Lema kuwa sauti ya wanyonge kwa kuzungumza hata kama itamfanya awe sehemu alipo hivi sasa, kwani kuna mambo mengi yanayohitaji kusemwa na hakuna wa kuyasema. 
Pia, alimsihi kutokuona kama ametengwa bali hiyo ndiyo njia ya wapigania haki na demokrasia wanayopitia, akijitolea mfano yeye binafsi.
 Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa alipotafutwa kwa njia ya simu hakupokea na alipotumiwa ujumbe mfupi hakuweza kujibu iwapo chama chake kilikuwa na taarifa ya ugeni wa Sheikh Ponda au ilikuwa ni safari binafsi. 
Atuma salamu za harusi 
Katika hatua nyingine Lema aliandika barua yenye kumbukumbu namba 76/AR/I/I/36 akimtakia heri ya ndoa, Wakili wa chama hicho, John Malya. 
Katika barua hiyo iliyowekwa muhuri na Ofisa wa gereza hilo, Lema alimtumia Malya salamu hizo katika ndoa yake iliyofungwa juzi, Jumamosi. 
“Harusi yenu ni Jumamosi tarehe 10/12/2016 na kwamba nadhani sitaweza kuhudhuria, ningependa sana kuwepo, nimeshindwa kusimamia na hata keki sili? Niko gerezani Arusha,” ilinukuliwa sehemu ya barua hiyo. 
Barua hiyo iliendelea: “Natamani kuona jinsi mlivyovaa kwani nilikuwa nimepania sana, lakini najua mtakuwa mmependeza sana ninawaombea kwani huku jela nina nafasi sana ya kuomba kwa kweli, naomba hadi Mungu anafurahi.”

Lema ambaye alikamatwa Novemba 2, akiwa Dodoma, hadi sasa anashikiliwa katika gereza hilo kutokana na kusudio na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) la kupinga uamuzi wa hakimu mkazi, Desdery Kamugisha aliyempa dhamana Lema katika kesi namba 440 na 441/2016 ya kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli. 

Katika kesi hiyo, ambayo huvuta umati, Lema anatuhumiwa kati ya Oktoba 23 hadi 26 kutoa kauli za uchochezi dhidi ya Rais Magufuli katika maeneo tofauti na mikutano yake ya hadhara. 
Lema anadaiwa katika maeneo matatu tofauti alitoa maeneo ya uchochezi kuwa: “Nchi itaingia katika machafuko kama haitafuata misingi ya katiba na sheria na pia Rais Magufuli asipobadilika.” 
Lema pia akiwa katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Baraa anadaiwa kutoa kauli kuwa: “Kiburi cha Rais akiendeea kujiona yeye ni Mungu, hatafika 2020, Mungu atakuwa amechukua maisha yake, Rais ni mbabe na watu anawaonea, wafanyakazi wa Serikali hawana amani, wafanyabiashara hawana amani.” 
Alisema Lema akiwa katika Uwanja wa Kambi ya Fisi Kata ya Ngarenaro alitoa kauli kuwa: “Rais akiendelea tabia ya kud- halilisha demokrasia na uongozi wa upinzani ipo siku taifa litaingia kwenye umwagaji wa damu, Rais yoyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria, katiba, atakuwa ameliingiza taifa katika majanga na umwagaji wa damu, watu wamejaa vifua wakiamua kulipuka polisi hawana uwezo na jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu utakapotea.”
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger