Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),
George Simbachawene amesema kipimo cha wakuu wa mikoa na wilaya itakuwa
ni utekelezaji wa agizo la kuhakikisha hakuna mwanafunzi atakayekaa
chini kwa uhaba wa madawati.
Rais
John Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa wakati akiwaapisha Ikulu,
jijini Dar es Salaam, kuhakikisha shughuli ya madawati inakamilika
ifikapo Juni 30.
Tangu
kutolewa kwa agizo hilo wakuu wa mikoa na wilaya wamekuwa wakihangaika
kulitekeleza huku wengine wakilazimika kuitisha harambee ili kuomba
wananchi wachangie.
Akizungumza
baada ya kufungua mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi kuhusu
namna ya kuweka mahusiano mazuri baina ya wawekezaji na wananchi ili
kupunguza migogoro ya ardhi, Simbachawene alisema kila DC na RC ajipime
kwa utekelezaji wa agizo hilo.
“Mkuu
wa mkoa au wilaya asiyetimiza agizo la kuhakikisha wanafunzi wote
wanakaa kwenye madawati hatoshi, hivyo wanapaswa kujitafakari na kutumia
siku zilizobaki kuhakikisha wanatekeleza,” alisema.
Alisema
zipo wilaya zilizofanikiwa kutekeleza agizo hilo huku baadhi ya mikoa
ikifikisha asilimia 80 na mingine ikiwa bado kwenye hatua za mwanzo.
Simbachawene
alisema Serikali imeruhusu raslimali za misitu kutumika kwa jili ya
kutekeleza agizo hilo na baadhi ya vibali vimeshatolewa kwa ajili ya
uvunaji wa misitu.
“Nitashangaa
kama kutakuwa na mkoa bado unasuasua wakati Serikali imesharuhusu
raslimali zilizopo zitumike kwa ajili ya kutengenezea madawati,”alisema.
Aliongeza
kuwa wanatarajia kutoa tathmini ya hali ya madawati nchi nzima,
mwishoni mwa mwezi huu baada ya agizo hilo kufikia ukomo wake.
Hata hivyo, alisema Rais Magufuli ndiye atakayetoa agizo la mwisho kwa wale watakaoshindwa kufikisha adhma hiyo.
Kuhusu
wawekezaji Simbachawene alisema wawekezaji wanalazimika kutengeneza
uhusiano mzuri baina yao na wananchi ili kuepuka migogoro.
Alisema
Serikali haitahusika iwapo wananchi watakataa ardhi yao isiwekezwe
licha ya kuwapo kwa mikataba na sheria zilizowaruhusu kuwekeza.
“Hata
kama kuna mikataba na sheria inawaruhusu wawekezaji hawa bado wananchi
lazima washirikishwe ili nao watoe kibali cha kazi hiyo kufanyika.
Unadhani wakiandamana kwa mabango kuzuia eneo lao lisitumike kwa kutoona
faida nini kitafanyika?Jamii ina umuhimu mkubwa kwenye suala hili,”alisema.
Aliwataka
wawekezaji hususani kwenye sekta ya madini na kilimo, kuwashirikisha
wananchi ili waridhike juu ya uvunaji wa raslimali zao jambo ambalo
litawaondolea vikwazo.
Hata
hivyo alisisitiza kuwa Serikali inaendelea kupitia mikataba ya madini
ili kuhakikisha kuwa inawanufaisha wananchi kwenye maeneo husika.
“Kitu
pekee ambacho huwa kinawaudhi wananchi ni pale wanapoona raslimali zao
haziwanufaishi, na hata hao wawekezaji wakiondoka huwa wanaacha
uharibifu mkubwa wa mazingira, ndiyo maana Serikali tunalazimika
kuwataka wawekezaji kuhakikisha uhusiano baina yao na wananchi
unaimarika,” alisema.
Mtafiti
wa Taasisi ya Uongozi, Dk Godfrey Nyamrunda alisema mdahalo huo
umeandaliwa ili kuongeza uelewa baina ya wawekezaji, Serikali na
wananchi kuhusu uwekezaji.
Mtafiti
Mkuu wa taasisi hiyo, Dennis Rweyemamu alisema migogoro ya ardhi
isipodhibitiwa inaathiri uwekezaji na hivyo kupunguza pato la taifa.
0 comments:
Post a Comment