ABIKANILE
anazidi kuandamwa na misukosuko ya kutisha. Alinusurika kifo siku
waliyouawa wazazi wake na siku aliyouawa mpenzi wake Mathius, lakini pia
katika hali ambayo hakuitegemea usiku wa siku hiyo aliyouawa Mathius
aliingia mikononi mwa vijana wanne waliompeleka kwa mganga wa kienyeji
ndani ya msitu wa Nyika.
Baada ya kumfikisha huko, mganga
huyo alitoa maelekezo kuwa ili vijana hao wawe matajiri ilikuwa ni
lazima wamchinje Abikanile katikati ya usiku, wachukue baadhi ya viungo
kwenye mwili wake ambavyo watavitumia kutengenezea mafuta ambayo
yangewasaidia.
Kwa vijana hao, hilo lilikuwa
jambo jepesi mno kufanya. Baada ya kufuata maelekezo yote aliyoyatoa
mganga huyo, majira ya usiku walielekea katikati ya msitu wa Nyika kwa
ajili ya kazi moja tu, kumchinja Abikanile na kumkata baadhi ya viungo
vyake vilivyohitajika! Je, nini kiliendelea?
SONGA NAYO…
ROELAND Wouda alikuwa
Tanzania kwa ajili ya kufanya uchunguzi dhidi ya samaki wanaoishi kwenye
maji safi, aliichagua nchi hiyo baada ya kusikia sifa kemkem juu ya
ziwa pekee duniani lenye aina nyingi ya samaki wenye rangi
tofautitofauti tena wenye kuvutia, Ziwa Nyasa.
Miongoni mwa watu waliomshawishi
kutembelea ziwa hilo walikuwa ni wazazi wake, tangu watembelee Tanzania
ulikuwa mwaka mmoja umekatika lakini amani ya nchi hiyo, hali nzuri ya
hewa na vivutio vya utalii ni vitu vilivyoishi muda wote ndani ya nafsi
zao.
Baada ya kufika Tanzania, Roeland
alifikia katika Hoteli ya Serena, siku mbili baadaye alisafiri hadi
jijini Mbeya kwa kutumia gari alilokodi kwenye Kampuni ya Utalii Kudu,
kwa ajili ya kuanza kufanya shughuli zake za kiuchunguzi.
“Tanzania inavutia sana!” Roeland
alimwambia James Mpochorwa, dereva kutoka Kampuni ya Kudu wakiwa
wamepumzika kwenye Hoteli ya Savana baada ya kufika Mbeya.
“Kwa nini?”
“Mazingira yake yanavutia, wazazi wangu wanaipenda na mimi naipenda pia!”
Siku hiyo waliitumia kwa kupumzika, pia
Roeland alifanya maandalizi kwa ajili ya kazi ya uchunguzi wa samaki
aliotakiwa kuufanya kuanzia siku iliyofuata katika Ziwa Nyasa.
* * *
Wakati Abikanile analia kwa uchungu
kutokana na kifo cha kinyama kilichokuwa mbele yake, Sanchawa, Moland,
Mateja na Shekidele walikuwa na furaha zisizoelezeka. Walifahamu ulibaki
muda mchache wamalize zoezi hilo la kumchinja binti huyo kwa ajili ya
kafara jambo ambalo lilitafsiri utajiri mkubwa mno kwao.
Akifuata maelekezo ya mganga Kyayera,
Sanchawa alisogea hadi walipokuwa wamemlaza Abikanile, mkononi alikuwa
ameshika kisu chenye ncha kali kwa ajili ya kumchinja msichana huyo.
Bila kupoteza muda, Sanchawa aliinama kisha akakipeleka kisu shingoni mwa Abikanile ili atenganishe kichwa na kiwiliwili.
Alichofanya msichana huyo ilikuwa ni
kufumba macho tu huku moyo wake ukikaribia kupasuka kwa uchungu.
Alizilaani roho mbaya za binadamu, moyoni mwake alizidi kuwasihi wazazi
wake kumpokea wakati ambao angekufa.
“Moja, mbili, taatu…” alisema Sanchawa akitengeneza kisu vizuri shingoni kwa Abikanile.
Ile anataka kumchinja tu, mara ilisikika
sauti kali kutoka kwa mtu mbele yao. Sanchawa nusura afe palepale!
Sauti ile ni kitu ambacho hakukitegemea kabisa. Bila kutegemea alijikuta
akidondoka chini kwa kiwewe, kisu kilidondokea upande mwingine lakini
hata alipojizoa vumbini alianza kutimua mbio yeye na wenzake wote baada
ya sauti ile waliyoisikia kuzaa sauti nyingine.
Abikanile akiendelea kushangazwa na
miujiza hiyo iliyokuwa inatokea katika maisha yake, mara alilishuhudia
kundi la watu waliobeba vizinga vya moto wakimzunguka.
Hao walikuwa vijana waliounda Kundi la
Zikomo. Idadi yao ilifikia vijana wa kiume kumi waliokuwa na umri
ulioendana, usiku huo walikuwa kwenye misitu hiyo ya Nyika kuwinda
wanyama wakali kama ilivyokuwa kawaida yao kila mara walipoagizwa ngozi
na mganga mkuu wa kabila lao la wayao, Lyziuzayan.
Vijana hao hawakupenda kuliacha jambo
hilo liishie hapo tu, walimkamata Abikanile, kisha wengine walianza
kuwakimbiza mganga Kyayera na wenzake, muda mrefu haukupita tayari
walikuwa wamekwishawatia mikononi Sanchawa, Moland, Mateja na Shekidele.
Mganga Kyayera na msaidizi wake waliyeyuka mfano wa moshi.
Hawakujulikana walitokomea wapi!
0 comments:
Post a Comment