Saturday 27 June 2015

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

ABIKANILE anazidi kuandamwa na misukosuko ya kutisha. Alinusurika kifo siku waliyouawa wazazi wake na siku aliyouawa mpenzi wake Mathius, lakini pia katika hali ambayo hakuitegemea usiku wa siku hiyo aliyouawa Mathius aliingia mikononi mwa vijana wanne waliompeleka kwa mganga wa kienyeji ndani ya msitu wa Nyika.

Baada ya kumfikisha huko, mganga huyo alitoa maelekezo kuwa ili vijana hao wawe matajiri ilikuwa ni lazima wamchinje Abikanile katikati ya usiku, wachukue baadhi ya viungo kwenye mwili wake ambavyo watavitumia kutengenezea mafuta ambayo yangewasaidia.
Kwa vijana hao, hilo lilikuwa jambo jepesi mno kufanya. Baada ya kufuata maelekezo yote aliyoyatoa mganga huyo, majira ya usiku walielekea katikati ya msitu wa Nyika kwa ajili ya kazi moja tu, kumchinja Abikanile na kumkata baadhi ya viungo vyake vilivyohitajika! Je, nini kiliendelea?
SONGA NAYO…
ROELAND Wouda alikuwa Tanzania kwa ajili ya kufanya uchunguzi dhidi ya samaki wanaoishi kwenye maji safi, aliichagua nchi hiyo baada ya kusikia sifa kemkem juu ya ziwa pekee duniani lenye aina nyingi ya samaki wenye rangi tofautitofauti tena wenye kuvutia, Ziwa Nyasa.
Miongoni mwa watu waliomshawishi kutembelea ziwa hilo walikuwa ni wazazi wake, tangu watembelee Tanzania ulikuwa mwaka mmoja umekatika lakini amani ya nchi hiyo, hali nzuri ya hewa na vivutio vya utalii ni vitu vilivyoishi muda wote ndani ya nafsi zao.
Baada ya kufika Tanzania, Roeland alifikia katika Hoteli ya Serena, siku mbili baadaye alisafiri hadi jijini Mbeya kwa kutumia gari alilokodi kwenye Kampuni ya Utalii Kudu, kwa ajili ya kuanza kufanya shughuli zake za kiuchunguzi.
“Tanzania inavutia sana!” Roeland alimwambia James Mpochorwa, dereva kutoka Kampuni ya Kudu wakiwa wamepumzika kwenye Hoteli ya Savana baada ya kufika Mbeya.
“Kwa nini?”
“Mazingira yake yanavutia, wazazi wangu wanaipenda na mimi naipenda pia!”
Siku hiyo waliitumia kwa kupumzika, pia Roeland alifanya maandalizi kwa ajili ya kazi ya uchunguzi wa samaki aliotakiwa kuufanya kuanzia siku iliyofuata katika Ziwa Nyasa.
*   *   *
Wakati Abikanile analia kwa uchungu kutokana na kifo cha kinyama kilichokuwa mbele yake, Sanchawa, Moland, Mateja na Shekidele walikuwa na furaha zisizoelezeka. Walifahamu ulibaki muda mchache wamalize zoezi hilo la kumchinja binti huyo kwa ajili ya kafara jambo ambalo lilitafsiri utajiri mkubwa mno kwao.
Akifuata maelekezo ya mganga Kyayera, Sanchawa alisogea hadi walipokuwa wamemlaza Abikanile, mkononi alikuwa ameshika kisu chenye ncha kali kwa ajili ya kumchinja msichana huyo.
Bila kupoteza muda, Sanchawa aliinama kisha akakipeleka kisu shingoni mwa Abikanile ili atenganishe kichwa na kiwiliwili.
Alichofanya msichana huyo ilikuwa ni kufumba macho tu huku moyo wake ukikaribia kupasuka kwa uchungu. Alizilaani roho mbaya za binadamu, moyoni mwake alizidi kuwasihi wazazi wake kumpokea wakati ambao angekufa.
“Moja, mbili, taatu…” alisema Sanchawa akitengeneza kisu vizuri shingoni kwa Abikanile.
Ile anataka kumchinja tu, mara ilisikika sauti kali kutoka kwa mtu mbele yao. Sanchawa nusura afe palepale! Sauti ile ni kitu ambacho hakukitegemea kabisa. Bila kutegemea alijikuta akidondoka chini kwa kiwewe, kisu kilidondokea upande mwingine lakini hata alipojizoa vumbini alianza kutimua mbio yeye na wenzake wote baada ya sauti ile waliyoisikia kuzaa sauti nyingine.
Abikanile akiendelea kushangazwa na miujiza hiyo iliyokuwa inatokea katika maisha yake, mara alilishuhudia kundi la watu waliobeba vizinga vya moto wakimzunguka.
Hao walikuwa vijana waliounda Kundi la Zikomo. Idadi yao ilifikia vijana wa kiume kumi waliokuwa na umri ulioendana, usiku huo walikuwa kwenye misitu hiyo ya Nyika kuwinda wanyama wakali kama ilivyokuwa kawaida yao kila mara walipoagizwa ngozi na mganga mkuu wa kabila lao la wayao, Lyziuzayan.
Vijana hao hawakupenda kuliacha jambo hilo liishie hapo tu, walimkamata Abikanile, kisha wengine walianza kuwakimbiza mganga Kyayera na wenzake, muda mrefu haukupita tayari walikuwa wamekwishawatia mikononi Sanchawa, Moland, Mateja na Shekidele. Mganga Kyayera na msaidizi wake waliyeyuka mfano wa moshi. Hawakujulikana walitokomea wapi!
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger