Saturday, 31 December 2016

MAGAZETI YA LEO TZ NA NJE,DEC 31 2016

Share:

Basi la National Express lapata ajali Singida....Wawili Wafariki, 26 Wajeruhiwa

Watu wawili wamefariki dunia na wengine 26 kujeruhiwa kwenye ajali iliyohusisha basi la kampuni ya National Express T.662 DEF, baada ya kuacha barabara na kupinduka zaidi ya mara tatu katika eneo la kijiji cha Tumuli, wilaya ya Mkalama mkoani Singida.

Waliofariki ni dereva wa basi hilo Athumani Idd (47) mkazi wa Mabibo jijini Dares Salaam na mwalimu wa shule ya msingi Malunga aliyefahamika kwa jina moja la Janet (anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 29).

Habari zilizopatikana jana eneo la tukio, zimedai kuwa katika siku za hivi karibuni mwalimu Janet alimpeleka mama yake jijini Dar es salaam kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Imedaiwa kuwa baada ya kufika Dar es Salaam, aligundua kuwa amesahau kuchukua kadi ya bima ya afya, na hivyo akalazimika kurudi Iramba.

Jana asubuhi Janet alichelewa basi la National Express katika kituo cha Kyengenge na kuamua kukodi bodaboda kulifukuzia basi hilo na kufanikiwa kulikuta kituo cha Malunga. Baada kupanda basi hilo, dakika chake baadae, basi hilo lilipata ajali na kulaliwa na basi kichwani.

Watu hao wamefariki dunia papo hapo na miili yao ipo katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya mkoa mjini Singida. Basi hilo lilikuwa linatokea New Kiomboi, likielekea jijini Dar.

Akizungumza kwenye eneo la tukio, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Singida , ACP Debora Daudi Magiligimba, alisema ajali hiyo imetokea Desemba, 30 saa 12.45 asubuhi katika eneo la kijiji cha Tumuli.

Alisema ajali hiyo pia imesababisha majeruhi 26 ambao wamelazwa katika hosipitali ya mkoa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Kamanda Magiligimba alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa ajali hiyo kwa kiwango kikubwa imesababishwa na mwendo kasi na uzembe.

“Eneo hili ilipotokea ajali hii kuna mteremko na kona kali. Kutokana na mwendo kasi, dereva alishindwa kulimudu na hivyo kuacha barabara na kuingia kwenye korogo la mto, na kuruka juu kisha kupinduka mara tatu,” alisema.

Kwa upande wake mganga mkuu mkoa wa Singida, Dk. John Mwombeki, alikiri kupokea miili ya watu wawili waliofariki dunia kwenye ajali ya basi la National Express, pamoja na majeruhi 26.

“Kati ya majeruhi hawa, mmoja dada Joyce tumempa rufaa kwenda hospitali ya taifa Muhimbili kutokana na sehemu yake ya mwili ya chini kutokufanya kazi. Majeruhi 10 wao tunaendelea kuwafanyia uchunguzi” alisema Dk. Mwombeki.

Mmoja wa majeruhi hao mfanyakazi wa shirika la TBC jijini Dar es Salaam, Victor Elia, alisema pamoja na kupoteza kila kitu, anamshukuru Mungu kwa kupona kufa kwenye ajali hiyo mbaya.

“Kilichonisaidia ni kufunga mkanda … abiria wenzangu wote ambao hawakufunga mikanda ndio walioumia zaidi wakiwemo waliopoteza maisha. Ajali hii kwa vyovyote imechangiwa na mwendo kasi,” alisema Victor ambaye ni mtayarishaji na mtangazaji wa TBC.

Kondakta wa basi hiyo, Nicolaus Apolinari (23) mkazi wa jijini Dar es Salaam, alisema ajali hiyo imechangiwa na utelezi uliosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha katika eneo hilo.
Share:

Kamanda Sirro Katoa Tathmini ya Uhalifu Dar kwa Mwaka Mmzima wa 2016

KIKOSI cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imekamata jumla ya watuhumiwa 13,626 na kuwafikishwa mahakamani kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo dawa za kulevya na ujambazi wa kutumia silaha kwa kipindi cha mwaka mmoja wa 2016.

Aidha, hali ya uhalifu wa kutumia silaha katika jiji la Dar es Salaam umepungua, ukilinganisha na mwaka uliopita wa 2015 na matukio yanayoongezeka kwa wingi ni ya ubakaji na ulawiti.

Akitoa tathmini ya mwaka mmoja, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema jana kuwa matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha yamepungua kutoka 204 mwaka jana hadi 127 mwaka huu.

Idadi hiyo ni pungufu ya matukio 77, sawa na asilimia 37.7 huku matukio ya kutumia nguvu yamepungua kutoka 1,181 mwaka jana hadi 874 sawa na asilimia 26.

Kamishna Sirro alifafanua kuwa matukio ya mauaji, yamepungua kwa asilimia 11 ukilinganisha na mwaka jana, ambapo kulikuwa na jumla ya matukio 327 wakati kwa mwaka huu ni matukio 291 pungufu ya matukio 36.

Alisema matukio ya ubakaji, yameongezeka kutoka 972 mwaka jana hadi 1030 mwaka huu, sawa na asilimia sita wakati matukio ya ulawiti yameongezeka kutoka 310 mwaka jana hadi 383 mwaka huu sawa na asilimia 23.5.

‘’Kwa matukio ya ubakaji yaliyoongezeka ni 58 na ulawiti matukio yaliyoongezeka ni 73. Lakini wizi wa watoto umepungua kutoka 26 mwaka jana hadi matukio 19 mwaka huu sawa na asilimia 27,’’ aliongeza.

Kwa mujibu wa Sirro, matukio ya uvunjaji yamepungua kwa asilimia 5.7 ambapo kwa mwaka jana kulikuwa na matukio 5,677 na mwaka huu matukio 5,355 sawa na upungufu wa matukio 322.

Kwa upande wa wizi wa magari, umepungua kwa asilimia 18.1 kutoka matukio 392 hadi 321 mwaka huu huku wizi wa pikipiki ukipungua kutoka pikipiki 2,644 mwaka jana hadi 2,191 ambapo matukio 453 yamepungua sawa na asilimia 17.1.

Wizi wa mifugo umepungua kutoka 197 mwaka jana hadi 163 mwaka huu sawa na asilimia 17.3 ikiwa ni pungufu ya matukio 34.

“Sababu za kuongezeka au kupungua kwa matukio hayo kumetokana na juhudi za polisi wa kuzuia na kupambana na uhalifu kwa kufanya doria pamoja na misako mbalimbali iliyosaidia kukamatwa kwa wahalifu wa makosa mbalimbali pamoja na raia wema ambao wametoa taarifa za siri ili kugundua makosa hayo,’’ alieleza Sirro.

Akielezea watuhumiwa hao, Sirro alisema kuwa kati yao 52 walikutwa na silaha za kivita 67 na risasi 1,076, na watuhumiwa 126 walikutwa na dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 75 na gramu 254.

Pia alisema kuwa watuhumiwa 7,625 walikutwa na bangi kilo 2,843 na gramu 78 huku watuhumiwa 269 walikutwa na cocaine kilo tatu na gramu 255 na heroine kilo moja na gramu 654.

‘’Watuhumiwa 5,627 walikutwa na pombe haramu ya gongo lita 8,547 na mitambo 34 na tuliwafikisha mahakamani. Pia tumekamata wahamiaji haramu 105 kutoka mataifa mbalimbali ambao hawana kibali cha kuingia na kuishi nchini,’’ alisema Sirro.

Katika hatua nyingine, Sirro alisema kuwa jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watu wanne wakiwa na gari moja aina ya Noah lenye namba za usajili T 188 CZN rangi nyeupe ambalo liliibwa mkoani Kilimanjaro.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Erasto Edward (36), mkazi wa Kawawa Moshi, Wilson Kapori (37) mkazi wa Njia Panda Himo mkoani Kilimanjaro, Hussein Issah (32) mkazi wa Chanika na David Marwa mkazi wa Pugu Kajiungeni.

Watuhumiwa hao walikamatwa Desemba 21 mwaka huu, saa 5 asubuhi katika misako maeneo ya Tabata Bima. Watuhumiwa walitumia ufunguo bandia kuiba gari hiyo.
Share:

Friday, 30 December 2016

UTAFITI: Mwanamke Huota Tofauti Na Mwanaume

Wanasema mwanamke na mwanaume ni tofauti kwenye baadhi ya mambo, kimaumbile. Lakini, sio yale mambo yenye kuonekana peke yake, kwani imebainika sasa ni kwamba, tofauti huenda hadi kwenye usingizi. Ni kwamba mwanamke na mwanaume huota tofauti.

Kwa hiyo, hata wakiwa usingizini, mwanamke na mwanaume wanaendelea na tofauti zao.
Dk. Mark Blagrove, ambaye ni mtaalamu wa saikolojia, anasema kwamba, yeye pamoja na mwenzake wamefanya utafiti kwa watu zaidi ya 100,000 na kubaini kwamba, kuna tofauti kati ya mwanamke na mwanaume hasa linapokuja suala la kuota ndoto.

Utafiti uliofanywa na Blagrove na wenzake umehusisha watu wa dunia nzima, sio ulaya na marekani peke yake.

Hivyo, ni utafiti ambao unazungumzia jambo linalohusu dunia nzima, siyo upande fulani tu wa dunia.

Katika utafiti huo, wamegundua kwamba, wanandoa ambao wamelala kitanda kimoja, ubavu kwa ubavu, wanakuwa na ndoto tofauti kabisa, ingawa wanaweza wakawa wanaota wakati mmoja.

Ndoto za wanawake zinaonekana wazi zinahusu kazi, zimejaa hisia sana ndani yake na huchukua muda mrefu zaidi.

Mwanamke anaweza kusimulia kuhusu ndoto yake, ukadhani imechukua saa kadhaa kuota kwa jinsi ilivyo ndefu. Huwa wanaota ndoto moja kwa muda mrefu zaidi.

Ndoto za wanawake zimejengwa kwenye msingi wa nyumbani na kuhusisha watu wengi na hasa wa familia zaidi, kuliko watu wa nje ya familia.

Kwa upande wa ndoto za wanaume, kuota wageni ni jambo la kawaida sana kwao. Wageni, ina maana watu ambao hawawafahamu. Ndoto za wanaume zimejengwa kwenye msingi wa maeneo ya barabara, magari na vurugu.

Hauwezi kupita muda mrefu kabla mwanaume hajaota kuhusu gari, barabara au vurugu za aina fulani.

Huhusisha pia tendo la ndoa na wanawake wasiowajua, mara nyingi.
Ndoto za wanaume pia zimejengwa pia kwenye mazingira ya kazi, na kuhusiana na hofu za kipato na hofu za kupoteza kazi au kufilisika. Zimejaa masuala ya kazi au shughuli.

Mwanasaikolojia aliyeandika pia vitabu kadhaa kuhusu ndoto, Veronica Tonay, anasema, utafiti huu unathibitisha tafiti za siku nyingi ambazo zilikuwa zinadai kwamba, wanawake huota tofauti na wanaume.

Hivi sasa, inaweza kusemwa kwamba, suala hilo halina utata tena. Inaonyesha pia kwamba, zaidi ya nusu ya watu wote wanapata ndoto mbaya angalau mara moja kwa wiki.

Kuna wengine ambao ndoto mbaya ni sehemu ya maisha yao ya kindoto,yaani karibu kila siku zinawatokea.

Inaelezwa kwamba, kazi anayofanya mtu inaweza kuchangia kwenye kuwa kwake na ndoto za jinamizi au ndoto mbaya.

Kwa mfano, wauguzi wahasibu na watumishi kwenye vyombo vinavyohusiana na mawasiliano, ndiyo ambao hukumbwa sana na ndoto hizi mbaya.

Soma; Ili ufanikiwe zaidi, unahitaji kuishi na watu hawa.
Kukimbizwa, meno kudondoka, kuanguka, kutegewa au kuwekewa kizuizi, ni miongoni mwa mada zinazootwa sana, hasa na wale wanaoota majinamizi.

Wanasaikolojia wanasema, ndoto zinahusiana na shughuli ambazo hatujazimaliza kwenye mpangilio wetu wa kazi wa siku au kujaribu kufanya kile ambacho tulishindwa kukifanya tukiwa macho.

Kwa mfano, kuota kupata fedha, jambo ambalo katika hali ya kawaida, limekuwa gumu kwetu.
Watafiti hapo wanazidi kuchambua ndoto kwa kusema kwamba, ndoto zinazohusu mambo mabaya ndizo ambazo zinaotwa zaidi kuliko zile zinazohusu mambo mazuri.

Hata wale watu wenye furaha maishani, wanaonekana kuota ndoto zenye mada zisizopendeza kuliko mada zenye kupendeza.

Ingawa wataalamu wa ndoto wanasema, kila ndoto ina maana kutegemea na mtu aliyeota, utafiti huu unaonyesha kwamba, pamoja na kuwa hilo ni kweli, kuna mambo ambayo mtu mmoja akiyaota , maana yake ni ile ile kwa mtu mwingine yeyote.

Kwa mfano, kuanguka, kwenye ndoto ina maana ya mtu kukosa uhakika wa usalama.
Kukimbizwa au kufukuzwa, bila kujali ni nani anaota, inaweza kuwa na maana ya kukimbia matatizo.

Ndoto ya kupoteza au kung’oka meno inahusiana na mtu kujali namna anavoonekana au sura.
Ndoto ya mtu kukimbia, lakini lakini akajikuta bado yupo pale pale, yaani hasogei, ina maana au inahusiana na mtu kuwa na kazi nyingi kumzidi uwezo.

Ndoto ya mtu kuwa uchi, ina maana kwamba, mhusika ana matamanio ya kuwasiliana na mwingine au wengine.

Kile ktiendo cha kuvua nguo ndotoni kina maana ya mtu kuondoa vikwazo vinavomkabili kwenye maisha ake.

Pamoja na kwamba, lengo la utafiti huu lilikuwa ni kuona kama mwanamke na mwanaume wanaota tofauti, bado umezaa masuala mengine muhimu ynayohusiana na ndoto. Moja ya hili lilozaliwa ni maana ya ndoto, ambazo hazibadiliki, bila kujali ni nani ameziota.
Share:

Jinsi ya kuishi na Watu wenye Tabia Ngumu

Ni ngumu na kamwe siyo rahisi kumbadilisha mtu mwenye tabia ngumu awe rafiki. Badiliko hili lawezekana ikiwa mhusika (mwenye tabia ngumu) atadhamiria na kuwatayari kushughulika ili kubadilika.

Kwa hiyo kama ni ngumu au haiwezekani kumbadilisha basi jaribu kubadili mtazamo wako na jinsi unavyoishi naye au nao, kwasababu mara nyingi wewe ndiye unaye kwazika au kuumizwa wakati yeye (yule anayekuudhi) anafanikiwa na anaendelea na furaha yake tu.

Mawasiliano baina yetu na watu wengine yanajumuisha jinsi tunavyowafanyia wengine na jinsi wao wanavyotufanyia sisi (reaction and counter reaction). Kwa kubadili jinsi sisi tunavyowatendea wengine inaweza kubadili jinsi wao wanavyotutendea sisi. Hata kama ni kwa muda au kitambo kidogo tu. Hata kama hali hii haibadili hali kwa kudumu ila inaweza kurahisisha mazingira ya kuishi na mtu au watu wenye tabia ngumu.

Kila wakati lazima uwe na akili sana katika kuishi na watu wenye tabia ngumu, kama hutoweza kujizuia, na ukaanza kuwabwatukia basi itakuwa unaleta tatizo hasa pale ambapo mwenye tabia hii ngumu ni bosi wako. Je, utaropoka au kutukana kama ulivyozoea?

Hata kama mtu au watu wenyetabia hii wako ndani ya familia na yamkini ni wadogo kwako kiumri, bado kuropoka na kuwapayukia siyo suluhisho, hali hii yaweza kukugharimu.

Najua kila mmoja wetu anajinsi anavyofanya kwa mtu au watu wenye tabia ngumu. Wote hatuna namna moja, mmoja anaweza kuwa ni mkimya na mwenye ujasiri hata anapoudhiwa, mwingine hupayuka na kumjibu yule anaye muudhi, mwingine anaamua kulia tu anapoudhiwa, wako wanaozira na kuamua kutozungumza tena na aliyewaudhi, wapo ambao husambaza habari mbaya kuhusu huyo mwenye maudhi, wako ambao huamua kumwambia uso kwa uso jinsi walivyo kwazika, sijui staili yako ni ipi.

Ni rahisi sana kuumizwa au kuudhiwa na maneno au matendo ya mwingine, na mara mtu huyo anapojua kuwa unaumia yeye hupata nguvu, hii huwa ndiyo silaha yake muhimu pale mnapopambana.

Unachotakiwa kufanya ni kuwaachia wakati wote wao wawe washindi, kamwe usitafute kushindana nao, utaumia mwenyewe. Njia pekee ni kujitahidi kuwa mjanja na mwenye akili kuliko yeye na pia kuwa na ushawishi katika yale wanayotaka kuyatenda hata pasipo wao kugundua.

Je, unawajibu vipi watu hawa (How do you react?)
Ni jambo jema kuanza kujitazama jinsi unavyowatendea wengine na jinsi tunavyoshughulika na wale wanaotukwaza. Kumbuka kuwa jinsi unavyoikabili hali hiyo katika mazingira fulani inawezekana isiwe hivyo katika mazingira mengine.

Watu wenye tabia ngumu na zinazotatiza mara nyingi huweka mitego ya maneno au matendo na kwa kiasi kikubwa unaweza kunaswa na kuwaruhusu wakuchezee jinsi watakavyo, na kati ya vitu wanavyo vipenda na kuvitamani ni kukuona unalia na kuumia na kuchanganyikiwa. Kwahiyo fikiri kwanza kabla hujafanya chochote mbele yao.

Watu watabia hii mara zote huwachukulia na kuwatendea watu wote sawa kwa hiyo usifikiri kila alichosema au alichofanya kwako ni cha kibinafsi sana na alikikusudia kwako. Angeweza kufanya au kusema hivyo hivyo hata kwa mwingine aliye karibu naye wakati ule. Kwa kufahamu hili itakusaidia kupunguza maumivu yanayoletwa na hisia zako kwake.

Hembu jiulize ni jinsi gani umewahi kukabiliana na mtu au watu wa jinsi hii, na je ilikuwa ni kwa jinsi ya kuumiza au kuelemisha? Fahamu kwamba kujibu kwa kupayuka, kutukana au kubishana haisaidii, bali kunakushusha chini ya miguu ya yule aliye kusababishia maumivu hayo, na sasa atakuwa anafurahia na kukuona wewe mjinga.

Ni chaguo lako, la ni jinsi gani utakabiliana na mtu au watu wa aina hii, ingawa unaweza kuchagua njia bora itakayoweza kukusaidia kukuimarisha na kupunguza udhaifu wako, zaidi ya kuamua kuchagua njia ambayo itakuacha umeumia, umechoka, umekatishwa tamaa na umejeruhika moyo.

Hii haimaanishi uwe mtu wa kusema ndiyo tu kwa kila kitu na kila mtu, na haimaanishi kuwa hutakiwi kukasirika HAPANA, hasira ni asili na haina tatizo lolote hapa, ila tu matokeo ya hasira hiyo ndiyo yanayoweza kuleta shida. Je ni jinsi gani unakabiliana na hasira yako na unaionyeshaje? Kwa fujo, kupayuka kubishana, kulia, kuvunja vitu, kunyamaza n.k.

Ili Kujua jinsi watu wenye tabia ngumu wanavyokuathiri. Jiulize maswali yafuatayo:

Je, ni unataka kutawaliwa na wengine?
Najua jibu ni kwamba hakuna nayetaka kutawaliwa na mwingine, na ndiyo maana unaweza kujikuta unabishana au kushindana na huyo anaye kukwaza.

Tatizo ni kwamba mwisho wewe ndiyo unaumia na yeye anabaki kufurahia kwa kukushinda mfano; tazama fujo za madereva barabarani hususan wale wa daladala.
Nikweli unahasira naye, lakini je hiyo ni njia muafaka ya kumkabili? kumbuka mwishoni atakayeumia ni wewe.

Fikiri kama unatatizo la shinikizo la damu kama utakubali kuyumbishwa kihisia na tabia mbovu za mwingine wewe ndiyo utabaki unaumia na siyo tu kama hutoweza kufanya vile moyo wako utakavyo bali pia utaachwa ukijihisi kuchoka, kuumizwa kwa hisia zako mwenyewe na kukatishwa tamaa na tabia yako wewe mwenyewe.

Nini Mwitikio wako pale unapoudhiwa? (Haswa na yule mwenye hasira na wewe)

  • Je, unalipa hasira kwa hasira?
  • Je, unajitetea na kuukimbia ukweli (being defensive)
  • Au unajificha kutoroka au kumkwepa?

Njia zote hizi hapa juu siyo nzuri.
Hata kama una haki ya kukasirika, lakini bado atakayeumia unabaki kuwa ni wewe. Na siyo tu utaumizwa na kukasirishwa kwa tabia yake mwenye kukuudhi bali utaumizwa moyoni mwako kwa vile wewe ulivyotenda, dhamiri itakushtaki zaidi (guilty conscious).

Je, unajizumgumziaje wewe mwenyewe, vibaya au vyema?
Mfano: Ukweli mimi najichukia haswa ninapofikia kipindi cha mitihani au usaili.
Hivi mimi nikoje?
Hivi kwa nini nimeumbwa hivi?
Kamwe mimi siwezi kufanya lolote jema!
Wakati wote mimi ni mtu wa bahati mbaya tu!

Wala huhitaji kujichukia unapofikia wakati wa mitihani au usaili, unachohitaji kufanya ni kujiandaa mwenyewe vizuri na kuwahi mapema katika eneo la tukio.
Hisia potofu na zisizojenga ambazo tunajiwazia wenyewe mara nyingi hutupotezea muda na mara tunapoziruhusu hutuharibia siku yetu nzima.

Unafanya nini unapopingwa? (what do you do when you are criticized)
Wako watu wanaopendelea kupinga wengine katika kila kitu, hata katika vile visivyostahili kupingwa,hakuna chochote chema kinachoweza kusemwa na yeyote, bali yeye peke yake. Hata kama kilichosemwa kina ukweli kwa asilimia kubwa basi mtu huyu atajitahidi walau kurekebisha hata lugha tu, ili mradi kisipite hivihivi bila yeye kukipinga japo kidogo (hawa ndiyo wale wenye tabia ngumu).

Hali hii huwapa kufurahi na kujijengea nguvu kwa jinsi wanavyopinga wengine.
Ni kweli upinzani mwingine ni wa ukweli na unajenga lakini hapa nakazia wale wanaopinga ili tu kujifurahisha nafsi zao na kuwafanya wale wanaowapinga waumie mioyo.

Je, unapopigwa, unajibuje?
Je, unajitetea au unajishusha na kukubali kila kinachopingwa kwa kuamini kwamba anayekupinga yuko sawa na kwa hiyo unayameza maoni yako yote, bila kuchambua kwa kina mapingamizi hayo.

Kuna jinsi ambavyo unaweza kumkabili au kumjibu anayekupinga na ikawa kama umeweka petroli kwenye moto, upinzani utawaka na hata kuleta ugomvi, lakini pia iko njia ambayo unaweza kumjibu mtu huyu na ukanyamazisha fukuto lote.

Je, una mtazamo hasi (mtazamo usiofaa) na wa kudumu katika kitu fulani?
Mfano; Labda unasema “Mambo yangu hayaendelei tangu nihamie katika nyumba hii, au mambo yangu yanakwama tangu nimuoe au niolewe na huyu, ni matatizo tu tangu tuoane, watoto hawa hasara tupu.” n.k.

Mtazamo huu hasi, waweza kukugharimu siyo tu kukunyima raha bali pia waweza kuharibu hisia zako na za wengine pia.

Ukijikuta katika hali hii ni vyema kujifahamu na kujitahidi kuelewa nini tatizo husika na jitahidi kubadilisha mtazamo wako.

Tafuta vile vitu ambavyo unaweza kuvitazama katika mtazamo chanya hata kama ni vidogo. Tafuta kuviongelea vile unavyovipenda zaidi ya vile usivyovipenda.
Je, unazimeza hisia zako zote, nzuri na mbaya?

Je, unaona ni ngumu sana kusema “nakupenda” “umependeza” “umeniudhi” n.k. labda unaweza kusema neno moja tu na siyo lingine. 
Wengi wetu tumekuzwa katika mazingira ambayo tunahofu kusema chochote ili tu tusije tukamkwaza mtu, hata kama tunaumizwa au tunajisikia vyema kusema kitu fulani, lakini tunajizuia.

Badala yake tunakwenda kusemea pembeni. Yamkini kunyamaza kunaweza kuwa na faida katika baadhi ya mazingira lakini siyo hata katika kukubali vitu visivyofaa. Hakuna ubaya wowote katika kuelezea jinsi unavyojisikia moyoni mwako ili mradi tu unaeleza kila unachokihisi kwa hali njema na siyo kwa hasira au shari. Katika hali hii kamwe hutowapoteza marafiki zako, na kama kuna yeyote aliye rafiki atasumbuliwa na hili basi usihofu, kubali tu kumpoteza kwa kuwa hakuwa wa muhimu au wa msaada sana kwako.

Hali ya kujifanya hujaumia au hujakwazika na wakati umekwazika na unalia ndani kwa ndani inaumiza na kufanya ujisikie vibaya sana. Inakufanya uzidishe mazingira ya msongo wa mawazo (stress) hasa pale unapojiwazia wewe mwenyewe zaidi ya kushughulika na wale waliokuudhi.

Mtazamo wako jinsi unavyojiona wewe mwenyewe huathirika sana, na pia waweza kujisababishia tatizo hasa pale wale wenye tabia ngumu watakapo kugundua kuwa huwezi kusema chochote hata ukiumizwa na hii itawafanya wakugeuze mpira wa kuchezea.

Je, wewe ni kati ya wale wanaojiamini kusema chochote wanachokifikiri bila kujali matokeo yake?
Hebu fikiria jinsi unavyojisikia pale ambapo mtu au watu wengine wangefanya hivyo hivyo kwako. Je, unataka kuwasababishia wengine maumivu ya moyoni? Kusema chochote kinachoshuka toka kichwani mwako kupitia kinywani mwako bila kufikiri juu ya matokeo au athari zake kwa wale wanaokusiliza au waliokuzunguka kunaweza kukupotezea marafiki na kuishusha hadhi yako kwa urahisi sana.

Mara nyingi mtu wa jinsi hii huweza kujikuta akiwa pweke na anayepingana na ulimwengu (kila mtu anamchukia). Hii ni kati ya hisia za kuhuzunisha na kuumiza sana muda wote, lakini pia huumiza zaidi pale unapogundua kuwa ni maumivu uliyojitakia mwenyewe. Peke yako unajikuta umetengwa na mtego wa kihisia na kukuzamisha usipoweza kujikwamua tena.
Share:

Feri wanasa 13 waliovua samaki kwa mabomu

UONGOZI wa Soko la Samaki la Kimataifa la Feri, Dar es Salaam umewakamata watu 13 wanaohusishwa kuvua shehena ya samaki 473 karibia tani 1.3 wenye thamani ya Sh milioni 13 kwa kutumia mabomu.

Samaki hao aina ya kolekole, jodari, changu, pono, sehewa na nguru waliingizwa sokoni hapo Desemba 16, mwaka huu na baada ya ukaguzi, ikabainika kuingizwa kwa samaki hao, huku wahusika wakidaiwa kutoroka.

Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alimtaka Mwenyekiti wa Bodi ya soko hilo, kupitia upya mfumo wa mapokezi, ulinzi na usimamizi ili kujiridhisha kama uko safi. Kuhusu kukamatwa kwa watuhumiwa hao,

Meneja wa Soko hilo, Eliakim Mniko alisema jana kuwa, walikamatwa sokoni hapo na wamefikishwa polisi kutoa maelezo na kufunguliwa kesi itakayoanza kusikilizwa mapema mwakani.

Akiwa katika ziara sokoni hapo Desemba 19, 2016, Dk Tizeba alisema ni aibu kwa kitendo hicho kufanyika meta chache kufika Ikulu na kwamba kama suala la ukaguzi limewashinda, Bodi ya soko iachie jukumu hilo kwa mamlaka nyingine ifanye kazi sokoni hapo.

Pia aliagiza wahusika wakamatwe na kuchukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kutangazwa kuwa ndio wanaoharamisha uvuvi na kulitia hasara taifa.
Share:

Mto Ruaha Mkuu wakauka

MTO Ruaha Mkuu unaopita ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (Runapa) umekauka maji. Hali hiyo inatishia uhai wa wanyama waliopo katika hifadhi hiyo kubwa kuliko zote nchini.

Gazeti hili lilitembelea hifadhi hiyo wiki iliyopita na kushuhudia wanyama wakihangaika kutafuta maji huku samaki, viboko na mamba ambao maisha yao yanabebwa na mto huo, wakiathiriwa kwa kiasi kikubwa na hali hiyo.

Baadhi ya miti inayoelezwa kuwa na majimaji ilishuhudiwa ikiwa imeanguka ndani ya hifadhi hiyo na maelezo yaliyotolewa na Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Runapa, Moronda Moronda ni kwamba imeharibiwa na Tembo wanaotumia miti hiyo kutuliza kiu ya maji.

Baadhi ya wadau wa mto huo, wamekosoa utekelezaji wa mikakati ya kuunusuru mto huo, wakisema haileti tija pamoja na kurejewa mara kwa mara.

Ofisa wa Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Malima Mbigima aliiomba serikali iingilie kati kwa kuyashughulikia masuala yote yanayosababisha mto huo ukauke.

Mbigima alisema nje ya hifadhi hiyo, mto huo umekuwa tegemeo kwa wakazi wengi ambao wamekuwa wakitumia maji yake kwa shughuli za uvuvi na kilimo.

“Hali kadhalika uzalishaji wa umeme katika mabwawa ya Mtera na Kidatu unategemea maji ya mto huu. Licha ya umuhimu huo, kiwango cha maji katika mto huo kimeendele kupungua siku hadi siku,” alisema.

“Mto Ruaha Mkuu wenye urefu wa kilomita 475 unaanzia katika Mlima Kipengere wilayani Makete mkoani Njombe, ukimwaga maji katika ardhi oevu ya Usangu wilayani Mbarali mkoani Mbeya kupitia Runapa hadi katika Mto Rufiji. Mto huu unachangia asilimia 22 ya maji ya Bonde la Rufiji ukiwa na zaidi ya aina 39 za samaki,” alisema.

Alitaja sababu kubwa ya mto huo kukauka kuwa ni shughuli za kibinadamu zinazofanywa kandokando ya vyanzo vya maji ya kwenye vyanzo vya maji vinavyopeleka maji katika mto huo.

Hivi karibuni, wadau wa mto huo waliafikiana katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza kupanga mpango wa pamoja utakaotekelezwa kwa pamoja kurejesha mtiririko wa maji katika mto huo kwa mwaka mzima.

Katika Kikao hicho kilichofanywa kwa ushirikiano na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira na Mali Hai Duniani (WWF), kwa mara nyingine wadau hao walikiri ni hatari kubwa kwa mto huo kuachwa uendelee kukauka.

Kaimu Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Mtera, Lewis Loiloi alisema ikiwa Mto Ruaha utakauka kabisa, basi gridi ya Taifa itaondokewa na megawati 284 za umeme.
Share:

New AUDIO | Aslay - Rudi | Download

Share:

MAGAZETI YA LEO IJUMAA DEC TAREHE 30.12.2016

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger