HIGHER EDUCATION STUDENTS’ LOANS BOARD
Plot No. 8, Block No. 46, Sam Nujoma Road, Mwenge; P.O. Box 76068, Dar es Salaam, Tanzania
Tel: (General) +255 22 2772432/2772433; Fax: +255 22 2700286; E-mail: info@heslb.go.tz Website: www.heslb.go.tz
TAHADHARI KWA WAOMBAJI WA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU KUHUSU KUZUKA KWA GENGE LA MATAPELI WANAODAI FEDHA KUTOKA KWA WAOMBAJI MIKOPO
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inapenda kuwatahadharisha waombaji wa mikopo na umma kwa ujumla, juu ya kuibuka kwa genge la matapeli wanaowalaghai wananchi ambapo hujitambulisha kuwa wao ni wafanyakazi wa Bodi ya Mikopo.
Mbinu zinazotumiwa na genge hilo la matapeli ni kuwatumia ujumbe mfupi wa simu waombaji wa mikopo ukiwatahadharisha kuwa fomu zao za maombi ya mikopo zina dosari na hivyo wanatakiwa watume sh. 15,000.00 kwa kutumia utaratibu wa kutuma Fedha kwa njia ya mitandao ya simu kwenda kwenye namba za simu za matapeli hao ili fomu zao za mikopo ziweze kufikiriwa.
Katika utapeli huo, matapeli hao wanawatishia waombaji wa Mikopo wanaoendelea na masomo kuwa wasipohuisha taarifa zao za kuendelea kupokea Mikopo mwaka ujao wa kitaaluma 2014/2015 hawatapata Mikopo.
Bodi ya Mikopo inapenda kuwafahamisha waombaji wa Mikopo na umma kwa ujumla kwamba:
(i) Waombaji mikopo wanatakiwa kutuma fomu zao au taarifa zilizokosekana kwa njia ya Posta tu. Bodi haijaweka wakala mwingine yeyote anayetoza ada kwa ajili hiyo.
(ii) Ada zote za maombi ya mikopo zilielekezwa kulipwa kwa njia ya M-Pesa kwa utaratibu ambao umeelekezwa bayana kwenye ukurasa wa maombi kwa njia ya mtandao (http://olas.heslb.go.tz) na si vinginevyo.
(iii) Waombaji wa Mikopo wanaoendelea na masomo hawatakiwi kujaza fomu za maombi ya Mikopo kama ilivyokwisha kufafanuliwa katika Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa mwaka wa masomo 2014/2015.
(iv) Waombaji mikopo watakaopokea simu au ujumbe mfupi wa simu unaowataka watume Fedha ili wapatiwe huduma ya kuhuisha taarifa zao za mkopo watoe taarifa kuhusu matapeli hao kwa Polisi au TAKUKURU kusudi hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahalifu hao.
IMETOLEWA NA:
KAIMU MKURUGENZI MTENDAJI
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
0 comments:
Post a Comment