Hatimaye lile sakata lililoibuliwa na Spika Job Ndugai la kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kufika mbele ya Kamati ya Bunge kuelezea kauli yake kuhusu, 'Udhaifu wa Bunge', leo ndio maamuzi rasmi ya sakata hilo.
Katika mkutano wake na wanahabari, Spika Ndugai alimtaka CAG Prof. Mussa Assad kufika mbele ya kamati ya maadili leo Januari 21, jijini Dodoma na kufafanua juu ya kauli yake ya 'Udhaifu wa Bunge', jambo ambalo Spika alidai ni kulidhalilisha Bunge.
CAG alitumia neno “udhaifu” wa Bunge alipokuwa akieleza sababu za kutofanyiwa kazi kwa ripoti zake ambazo zimekuwa zikibainisha ufisadi.
Wakati hayo yakiendelea, Ndugai amesitisha kufanya kazi na ofisi ya CAG na kuwatawanya wajumbe wa kamati mbili; ya Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na kuongeza nguvu kwenye kamati nyingine wakati huu ambao zitakuwa hazina majukumu.
PAC na LAAC zinazoongozwa na wenyeviti kutoka vyama vya upinzani, ndizo zimekuwa zikifanyia kazi ripoti za CAG na ratiba ya awali ya Bunge ilionyesha kamati hizo zingetakiwa zikijadili ripoti ya sasa.
Hata hivyo, Januari 17, Profesa Assad aliita waandishi wa habari na kueleza nia yake ya kwenda mbele ya Kamati ya Maadili, akieleza kusikitishwa na jinsi kauli yake ilivyozua mjadala na kutia doa uhusiano baina ya ofisi yake na Bunge.
Mbali na kukubali wito huo CAG, amesema kauli yake haikulenga kulidhalilisha Bunge na kwamba neno udhaifu ni la kawaida hasa kwenye kada hiyo ya ukaguzi na amekuwa akilitumia hata katika ripoti zake.
CAG Assad aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, Desemba Mosi mwaka 2014 ameitwa mbele ya kamati hiyo kujieleza kuhusu kauli aliyoitoa wakati alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa (UN) akiwa New York, Marekani alikokuwa akihudhuria mkutano.
Chanzo: Eatv
0 comments:
Post a Comment