Mkazi wa Busale, Zawadi Daudi (41) anayetuhumiwa kumuua mke wake, Hawa Kamwela (32), amekamatwa akiwa chini ya uvungu wa kitanda cha wazazi wake na jeshi la polisi kwa kushirikiana na raia wema.
Daudi anadaiwa kumuua mkewe baada ya kutakiwa afanye maandalizi ya kumpeleka shuleni mtoto wao, Siri Zawadi, aliyechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.
Baada ya kudaiwa kutenda mauaji hayo mapema wiki hii kwa kutumia panga, Daudi alikimbilia kusikojulikana na baada ya mwili wa marehemu kupelekwa mochwari, ndugu wa mwanaume na wa mwanamke walianza kugombania maiti na hatimaye upande wa mkewe kupewa haki ya kuuzika.
Sanke Mwakajila, mkazi wa Busale, alisema jana kuwa baada ya tukio hilo, wananchi walianza msako wa kimya kimya kujua mahala alipo mtuhumiwa na baadaye wakaenda kitongoji cha Kabale.
Alisema baada ya kufika kitongoji hicho, mahala alikozaliwa mtuhumiwa, walifika katika nyumba ya wazazi wake saa 10 usiku na baada ya kubaini kuwa amejificha katika nyumba hiyo, walipiga lamgambo (ngoma) kuwakusanya wanakijiji.
Mwakajila alisema baada ya wanakijiji kufika eneo hilo, walimwita mwenyekiti wa kijiji na diwani ili wahudhurie tendo hilo, ndipo walipoingia ndani ya nyumba na kuanza kupekua na kumkamata akiwa chini ya uvungu wa kitanda wanacholalia wazazi wake.
Aida Maonwa, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, alisema alipata mshtuko baada ya kupigiwa simu na wanakijiji wakimweleza kuwa mtuhumiwa amejificha kwenye nyumba ya wazazi wake na alipofika eneo la tukio, alikuta wamemtoa nje ndipo alipopiga simu polisi.
Alisema baada ya polisi kufika hapo alfajili ya jana, walimchukua mtuhumiwa huyo akiwa salama na sasa ametiwa mbaroni polisi wakiendelea na uchunguzi na kwamba anawapongeza wananchi kwa ushirikiano wao kwa kuwa hawakutaka kumpiga bali walitaka sheria ifanye kazi yake.
Adam Kapeta, Diwani wa Kata hiyo, alikiri kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kusema baada ya kukamatwa aliwasihi wananchi wawe watulivu na polisi walipofika walimchukua na kuondoka naye kisha wakaendelea na kuwahoji wazazi waliomhifadhi mtuhumiwa.
Baada ya kukamatwa mtuhumiwa huyo, alisema yeye na viongozi wengine wa kijiji na kata, wanapanga kwenda kuzungumza na wazazi wa mtuhumiwa kujua sababu ya kumficha mtoto wao ilhali wanafahamu kuwa amefanya mauaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, alikiri kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kuwapongeza wananchi kutokana na ushirikiano wao kwa jeshi la polisi na kwamba mtuhumiwa atapandishwa kizimbani baada ya uchunguzi kukamilika.
0 comments:
Post a Comment