Wakuu wa mikoa wote nchini Tanzania wameitwa jijini Dar es Salaam kupeana mbinu mbalimbali kuhusu ugawaji vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo.
Imeelezwa kuwa vitambulisho hivyo vilivyotolewa na Rais John Magufuli ugawaji wake katika mikoa mbalimbali nchini ni wa kusuasua.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Januari 26, 2019 mjini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo katika ufunguzi wa mkutano wa siku moja kwa ajili ya mikakati ya uanzishwaji wa masoko ya madini.
Washiriki wa mkutano huo walikuwa maofisa na wafanyakazi wa wizara ya madini, wakuu wa mikoa na makatibu tawala mikoa.
Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Jafo amesema kuna mikoa inasuasua zaidi katika zoezi hilo licha ya kuwa baadhi ya mikoa imeshafikia hadi asilimia 94.
Bila kuitaja mikoa iliyofanya vizuri na ambayo inasuasua, amesema kitendo hicho hakifurahishi kwani kinarudisha nyuma juhudi za Rais Magufuli.
"Niwatangazie kuwa Jumatatu tunatakiwa Dar es Salaam na Rais kwa ajili ya maelekezo zaidi na mbinu za kufanya katika kazi hii," amesema Jafo.
0 comments:
Post a Comment