Wednesday, 30 January 2019

MUSWADA WA VYAMA VYA SIASA WAPITA WABUNGE WA CCM, UPINZANI WAKIVUTANA

...

Na Sharon Sauwa, Mwananchi 
 Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018 jana ulipitishwa bungeni, Dodoma.

Kabla ya kupitishwa kwa muswada huo uliowasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama aliyeuita kuwa ni kiboko, kuliibuka mvutano mkali kati ya wabunge wa upinzani na CCM.

Baada ya kupitishwa, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema, “Kilichobaki tutaupeleka kwa Mheshimiwa Rais ili akiridhia ausaini uwe sheria.”

Awali, Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria ilipendekeza kurekebishwa au kufutwa kwa maeneo saba makubwa huku Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ukiwataka wabunge kuukwamisha.

Muswada huo umepita huku Taasisi sita za kiraia zikiongozwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), zikiwa zimetoa onyo kuwa hakuna mtu aliye salama endapo utapitishwa.

Taasisi hizo zinajumuisha Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Twaweza, Baraza la Habari Tanzania (MCT), Center for Strategic Litigation na Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (Wahamaza).

Waziri Mhagama alisema pamoja na mambo mengine, muswada unalenga kumpa uwezo Msajili wa kuhakiki chama cha siasa wakati wowote. “Lengo ni kuhakikisha chama cha siasa kinakuwa na sifa za usajili muda wote wa uhai wake na kueleza bayana mamlaka ya msajili wa vyama vya siasa kuhakiki muda wowote utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa ili kuhakikisha chama cha siasa kinazingatia na kutekeleza masharti ya usajili,” alisema.

Hata hivyo, Ester Bulaya akisoma maoni ya kambi ya upinzani alisema kifungu kinachompa mamlaka msajili wa vyama vya siasa kuingilia mfumo wa uchaguzi ndani ya chama kitapunguza uhuru wa vyama kufanya chaguzi bila mashinikizo.

Alisema kifungu kingine ni kinachotoa masharti ya namna ya utoaji wa elimu ya uraia hakikutilia maanani kuwa vyama vya siasa vina uhusiano wa kiitikadi na vyama rafiki kutoka nje ya nchi.

Bulaya ambaye ni mbunge wa Bunda Mjini (Chadema) alisema Katiba inatoa masharti ya mtu anayetaka kugombea urais na umakamu wa Rais wa Tanzania kwamba anatakiwa kuwa raia kwa kuzaliwa lakini masharti hayo hayakuwekwa kwa wazazi wake.

“Kambi ya upinzani inahoji kwa nini mtu anayegombea nafasi ya juu kabisa ya uongozi wa Taifa hili wazazi wake hawawekewi masharti ya uraia na Katiba iweje mtu anayetaka kusajili chama cha siasa awekewe masharti hayo?” alihoji.

Mvutano ulivyokuwa

Mbunge wa Kawe (Chadema) Halima Mdee, akichangia muswada huo alisema katika ibara ya 8 c ya muswada huo kuna uvunjwaji wa Katiba.

Alisema muswada huo unataka kufutwa kwa chama ambacho kitashindwa kuwa na kumbukumbu ya wanachama wake wakati Katiba imeeleza mazingira ambayo yanaweza kukifanya chama kufutwa.

Mdee aliungwa mkono Mbunge wa Tanga Mjini (CUF) Mussa Mbarouk aliyewataka wenzake wa CCM kutambua kuwa ipo siku nao watakuwa chama cha upinzani na kwamba sheria hiyo itawahusu.

Hata hivyo, Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Sixtus Mapunda alisema muswada huo ndio mwarobaini wa kuondoa uhasama unaotokana na vyama vya siasa, “Ilifika hatua vijana wetu badala ya kutulinda wanageuka kuwa wana migambo au Al Qaeda, tunakwenda katika uchaguzi vijana wanamwagiana tindikali, wanakatana masikio, migongo. Hii sheria inakwenda kuondoa hawa Mungiki,” alisema.

Mbunge wa Madaba (CCM) Joseph Mhagama aliwataka wabunge wa upinzani kuacha upotoshaji juu ya muswada huo akisema unalenga kuweka uwazi na uwajibikaji katika uendeshaji wa vyama vya siasa.

Via Mwananchi
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger