Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kambi ya Suku Mikumi, wilayani Kilosa mkoani Morogoro, Godlisten Remngstone (46), anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya mapenzi na binti wa miaka 17, mwanafunzi wa kidato cha nne.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbrod Mutafungwa, alisema askari huyo alikamatwa Januari 23, mwaka huu, majira ya alasiri maeneo ya Kikwalaza, Mikumi Wilaya ya Kilosa.
Alisema kuwa askari huyo alikamatwa na wananchi na kufikishwa katika kituo cha polisi Mikumi baada ya kumwita mwanafunzi huyo na rafiki yake nyumbani kwake kwa nia ya kufanya naye mapenzi.
Katika tukio lingine Paulo Ilonga (68), anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwabaka watoto wawili wa familia moja mmoja akiwa na umri wa miaka minane na mwingine miaka tisa, wakiwa watoto wake wa kufikia.
Kamanda Mutafungwa alisema mtuhumiwa huyo aliwabaka watoto hao baada ya kuwatoa ndani walikolala na kuwapeleka nyuma ya nyumba, huku akiwatishia kuwapiga.
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi linamshikilia Jafari Ramadhani (26), mkazi wa Kidudwe Turiani, kwa tuhuma za kumbaka mwanawe wa kumzaa mwenye umri wa miaka sita baada ya kumwita chumbani.
Tukio hilo lilitokea Januari 21, mwaka huu saa nne asubuhi katika kijiji cha Kidudwe Turiani, baada ya mama mzazi wa mtoto huyo kugundua kuwa mtoto wake amebakwa na hivyo kutoa taarifa polisi.
Watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani uchunguzi na taratibu za kisheria utakapokamilika.
Credit: Nipashe
0 comments:
Post a Comment