Wadau wa sekta ya madini nchini wameeleza kusikitishwa na namna ambavyo biashara ya madini inavyoendelea kuendeshwa kimagendo huku wakaguzi wa madini na Jeshi la Polisi wakiwa hawazijui njia hizo.
Wadau wameeleza njia hizo wakati wakizungumza mbele ya Rais Magufuli ambaye ni mgeni rasmi katika mkutano wa kisekta wa Wizara ya Madini katika ukumbi wa mikutano wa JNICC Jijini Dar es salaam.
Mdau wa dhahabu aliyejitambulisha kwa jina la Solomon Mihayo wa mkoani Geita amesema kuwa watu wanasafirisha dhahabu kimagendo mipakani na licha ya ukaguzi unaofanyika lakini hawawezi kujulikana.
"Mhe. Rais kuna watu wanaiibia serikali lakini siwezi kutaja ni watu gani, watu wanachana kabichi na kuweka hadi kilo mbili za dhahabu na wanapita nazo tu mipakani, watu wanatumia tairi za gari wanaweka dhahabu hadi kilo 10 na hawatambuliki, wengine wanapasua matikiti maji haya wanaficha dhahabu na kupita nazo mipakani", amesema Solomon.
"Kuna mazingira mengi ambayo Polisi pekee hawawezi kutambua, tutawalumu bure tuu. Wanafanya kazi kubwa sana polisi lakini hawawezi kupambana nao", ameongeza.
Pia bwana Solomon kwa niaba ya wadau wa dhahabu, ametoa mapendekezo kuwa wajumuishwe katika kamati zinazoundwa na Wizara husika ili waweze kusaidia kuwatambua na kuwakamata wezi hao.
0 comments:
Post a Comment