Siku mbili baada ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kusema Wilaya ya Temeke
inaongoza mkoani Dar es Salaam kwa kuwa na wagonjwa sita wa
kipindupindu, Mkuu wa wilaya hiyo (DC), Sophia Mjema amesema hadi jana
hakukuwa na mgonjwa hata mmoja.
Baada ya DC huyo kukanusha, jana wizara hiyo ilitoa taarifa ikisisitiza kuwa wilaya hiyo inakabiliwa na ugonjwa huo.
Kipindupindu
ni moja ya vigezo vinne vilivyowekwa na Rais John Magufuli kupima
utendaji kazi wa wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri
kabla ya kufanya uteuzi mpya.
Jumatatu iliyopita akiwa Hospitali
ya Taifa Muhimbili, Waziri Ummy alitoa takwimu za ugonjwa huo na
kuitaja Temeke kuwa kinara lakini juzi, Mjema alisema kulikuwa na
wagonjwa ambao hawakuwa wamethibitika kama wanaugua kipindupindu.
Jana,
Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Temeke, Joyce Msumba alisema juzi
kulikuwa na mgonjwa mmoja wa kipindupindu lakini aliruhusiwa baada ya
kupona.
“Kwa hiyo leo (jana) Manispaa ya Temeke haina hata mgonjwa mmoja na kambi ni nyeupe haina mtu,” alisema.
Alisema
manispaa hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kanuni za afya
ili kujikinga na ugonjwa huo baada ya kufanikiwa kuutokomeza.
“Hatutapumzika tutaendelea kuwakumbusha wananchi kutunza mazingira yao kuwa safi kwa sababu kipindupindu ni hatari,” alisema.
Wakati
ofisa hiyo akisema hayo, Waziri Ummy alitoa taarifa akisema Mkoa wa Dar
es Salaam kwa siku 10 zilizopita kuanzia Februari 7 hadi 16 kulikuwa na
wagonjwa 16; Temeke 12 na Ilala wanne.
Alisema wizara yake
ndiyo yenye dhamana ya kusimamia huduma za afya kwa jamii, hivyo
wagonjwa hao walikidhi vigezo vya ainisho sanifu na kupata matibabu
katika kambi ya kipindupindu kwa wagonjwa wa Temeke na Hospitali ya
Amana kwa wagonjwa wa Ilala hivyo kulazimu kutolewa taarifa kwa mujibu
wa mwongozo.
0 comments:
Post a Comment