Jeshi la Polisi limeweka ulinzi katika Bandari ya Dar es Salaam, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga kuwa ilindwe na vyombo vya dola badala ya kampuni binafsi za ulinzi.
Akizungumza kwenye kikao cha kazi kilichowahusisha makamanda wa mikoa na vikosi vya polisi nchini, Mkuu wa jeshi hilo (IGP), Ernest Mangu, alisema tayari wamepeleka askari bandarini ambao wanafanya kazi kwa muda wakishirikiana na walinzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
Mangu alisema askari hao wanakwenda kulinda kwa muda wakitokea Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.
Alisema amewaomba TPA wajenge kituo cha polisi bandarini hapo, ili askari wawepo muda wote.
“Tumetekeleza agizo la waziri, kwa sasa bado tunamalizia logistics fulani ili tuwe pale bandarini permanently (muda wote). Tunahitaji ushirikiano wa watendaji wote ili kuimarisha ulinzi wa mali za wananchi,” alisema Mangu.
Alisema polisi wamejipanga vyema kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kurudisha nidhamu ya utendaji, kupambana na uhalifu, dawa za kulevya, ujangili na ujambazi.
Mkuu huyo wa polisi alisisitiza kwamba, kuanzia Juni Mosi, mwaka huu wataanza utaratibu mpya wa utendaji chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ili kuhakikisha wanashirikiana na wananchi kulinda mali na maisha yao.
“Kaulimbiu yetu ni ‘badilika kifikra, acha kufanya kazi kwa mazoea’. Kaulimbiu hii ni kielelezo cha jinsi tulivyodhamiria kubadilika kiutendaji,” alisema.
Awali, akifungua kikao hicho, Waziri Kitwanga aliwapongeza makamanda hao kuandaa kikao ili kuelekezana nini cha kufanya kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na Taifa.
“Serikali haitafumbia macho askari au ofisa yeyote atakayeomba na kupokea rushwa, kuchelewesha upepelezi, kutowajali wateja, kubambikia wananchi kesi na mambo mengineyo. Tutachukua hatua bila kujali cheo chake,” alisisitiza.
Kitwanga alisema Serikali imejipanga kuboresha maisha ya askari na mazingira yao ya kazi.
Alisema Serikali imeagiza magari na kupanga kujenga nyumba 3,500 kwa ajili ya makazi ya askari.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ineke Bussemaker ambayo pia imedhamini kikao hicho alipendekeza matumizi ya fedha kielektroniki kwa kuwa ndiyo njia salama ya kutumia huduma za kibenki.
0 comments:
Post a Comment