Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), limeagiza kusitishwa kwa ugawaji wa vyeti vya kidato cha sita kwa wanafunzi waliohitimu mwaka 2015, huku vile vilivyokwisha gawanywa kwa watahiniwa hao vikitakiwa kurejeshwa kwenye chombo hicho.
Hali
hiyo imeibua utata mkubwa, huku baadhi ya wadau wakiwamo maofisa elimu,
wakihisi hatua hiyo ya Necta huenda inalenga kuvibadili vyeti hivyo
kutoka kwenye mfumo wa wastani wa alama (GPA), kwenda kwenye ule wa
jumla (division).
Ofisa
Elimu Mkoa wa Dodoma, Juma Kaponda, alipoulizwa kama amepokea agizo
hilo, alithibitisha kuwa shule zote za mkoa huo zenye kidato cha tano na
sita zimepewa taarifa ya kutakiwa kurudisha vyeti hivyo Necta.
Alisema sababu ya kuvirudisha vyeti hivyo anadhani ni kufanya mabadiliko kutoka GPA na kurudi kwenye divisheni.
Ofisa
Elimu Mkoa wa Arusha, Nestory Mloka, alisema amepata barua ya maelekezo
hayo kutoka Necta ikimuelekeza kuwataka maofisa elimu wilaya
wawasiliane na wakuu wa shule za kidato cha tano na sita wasigawe vyeti
vya wanafunzi waliohitimu mwaka 2015.
Mkuu
wa Shule ya Sekondari ya St. Matthew iliyoko Kongowe, Mkuranga mkoani
Pwani, Abraham Shafuri, naye alikiri kuwapo kwa agizo la Necta la
kusimamisha utoaji wa vyeti hivyo kwa wahusika.
Alisema
aliambiwa na maofisa wa Necta kuwa vyeti hivyo vinatakiwa kurejeshwa
kwenye baraza hilo na kwamba sababu zilizotolewa ni kuwa kuna
marekebisho kidogo yanapaswa kufanyika.
“Nilichoambiwa
ni kwamba shule karibu zote za Dar es Salaam zimesharejesha vyeti hivyo
na kwamba kwa sisi wa mkoa wa Pwani, maofisa hao watapita kuvichukua
lakini hatujui ni lini watakuja,” alisema Shafuri.
Hata
hivyo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk, Charles Msonde, alipoulizwa
alikanusha vikali madai hayo, akisema vyeti hivyo havitabadilishwa
kutoka kwenye mfumo wake bali vimesitishwa kugawanywa ili baraza
lijiridhishe na baadhi ya vitu.
“Vyeti
hivi baraza limevigawa hivi karibuni na lilichofanya sasa limezuia
kwanza shule zisigawe mpaka litakapotoa maelekezo mengine, msingi huo wa
kuzuia uko kwenye hoja ya kuhakikisha tu kwamba linajiridhisha kwenye
takwimu zake kama zimekaa sawasawa katika vyeti vilivyokwenda kila
shule.
“Baadhi ya vyeti kwenye mkoa wa Dar es Salaam vipo Necta, lakini kwenye mikoa mingine yote viko shuleni,” alisema Dk Msonde na kuongeza;
“Kama mkuu wa shule alikuwa amegawa vyeti viwili, vitatu kabla
havijarejeshwa baraza ni suala jingine, lakini kiujumla kinachofanywa na
baraza hapa ni kuhakiki cheti hiki, kama vimekaa kama utaratibu wetu
ulivyo.”
Alisema
suala la kubadilisha kutoka kwenye GPA kwenda kwenye divisheni halipo
na kwamba matokeo yaliyotangazwa kwa utaratibu wa GPA vyeti vyake
vitaendelea kuwa katika mfumo wa GPA na matokeo yaliyotangazwa kwenye
utaratibu wa divisheni vyeti vyake vitabaki kuwa kwenye divisheni.
Alisema
kwa wale ambao tayari wako nje ya nchi, hakuna atakayeathirika na kama
baraza likihitaji cheti chake litafanya utaratibu wa kukipata.
0 comments:
Post a Comment