1.Tunapenda
kuuarifu umma kwamba, Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu Tanzania (SJUIT)
Kampasi ya Arusha ni mojawapo ya vyuo vikuu vilivyosajiliwa na Tume ya
Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ambacho kilianza kudahili wanafunzi kwa mara
ya kwanza mwaka wa masomo 2013/2014.
2.Kwa
mujibu wa kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura ya 346 ya
Sheria za Tanzania, Tume ina mamlaka ya kusimamia na kudhibiti ubora na
usimamizi wa uendeshaji wa Vyuo Vikuu hapa nchini.
3.Kwa muda
mrefu na kwa wakati tofauti kumekuwapo na matukio ya migogoro baina ya
uongozi wa Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu Kampasi ya Arusha na wanafunzi.
Kwa
kipindi hiki chote Tume imekuwa ikifuatilia kwa karibu chimbuko la
migogoro hiyo na kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kutoa
maelekezo kwa uongozi wa chuo kurekebisha kasoro zinazosababisha
migogoro chuoni hapo.
Kwa sehemu kubwa migogoro hiyo imekuwa ikitokana
na matatizo ya ubora, uongozi, ukiukwaji wa sheria na taratibu za
uendeshaji wa chuo kikuu kama zilivyobainishwa na Sheria ya Vyuo Vikuu.
Hata hivyo jitihada za Tume ya Vyuo Vikuu kukitaka Chuo Kikuu cha Mt.
Yosefu Tanzania (SJUIT) Kampasi ya Arusha kuhakikisha kuwa elimu
inayotolewa katika Kampasi hii inakidhi viwango vya ubora vilivyowekwa
na Tume hazikupewa uzito stahiki na uongozi wa chuo.
4.Hivi sasa Kampasi ya Arusha ina jumla ya wanafunzi 1557 wanaosoma programu za masomo ya ualimu wa sayansi zifuatazo:
5.Kutokana
na yaliyobainishwa hapo awali, tunapenda kuuarifu umma kwamba, Tume
imejiridhisha kuwa Kampasi ya Arusha ya Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu
Tanzania imepoteza sifa na vigezo vya kuendelea kutoa elimu ya chuo
kikuu.
Kwa kuzingatia ukweli kwamba wanafunzi ndio waathirika wakuu wa
matatizo yaliyopo kwenye Kampasi hii, Tume imeamua kama ifuatavyo:
a)Imefuta
kibali kilichoanzisha Kampasi ya Arusha ya Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu
Tanzania (SJUIT) na kuidhinisha uhamisho wa wanafunzi wote waliokuwa
wanasoma katika Kampasi hiyo ya Arusha kwa gharama za Chuo Kikuu cha
SJUIT. Orodha ya majina yao na vyuo watakavyopangiwa itatangazwa na
kuwekwa katika tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu hivi punde.
b)Imefuta
udahili wa wanafunzi wapya katika programu ya shahada ya miaka mitano
ya ualimu wa sayansi. Na kwamba, wanafunzi wanaoendelea na masomo katika
programu hii watahamishiwa katika Kampasi ya Luguruni, Dar es Salaam,
na watalazimika kwanza kuhitimu katika ngazi ya Stashada (Diploma) kama
ilivyokuwa imeidhinishwa na Tume hapo awali. Utaratibu wa uhamisho wa wanafunzi wa programu hii utatangazwa hivi punde na kuwekwa katika tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu.
c) Imeidhinisha
wanafunzi wa mwaka wa kwanza ambao hawakuweza kupata udahili katika
vyuo vikuu vingine, kutoka katika kundi la wapatao 500 waliofukuzwa
chuoni kutokana na migogoro iliyojitokeza katika Kampasi ya Arusha mwezi
Juni, 2015 kuendelea na masomo katika vyuo watakavyopangiwa baada ya
taratibu za uchambuzi wa taarifa zao kukamilika. Orodha ya majina yao na
vyuo watakavyopangiwa itatangazwa na kuwekwa katika tovuti ya Tume ya
Vyuo Vikuu hivi punde.
6.Kufuatia
uamuzi huu, wanafunzi wote wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu
Kampasi ya Arusha wanaarifiwa kuwa watahamishiwa kwenye vyuo vikuu
vingine vinavyofundisha programu za masomo zinazofanana na masomo
wanayosoma hivi sasa chini ya utaratibu na masharti yafuatayo:
i)Wanafunzi
wote wanapaswa kuondoka chuoni mara moja baada ya kukamilisha taratibu
za kukabidhi mali na vifaa vingine vya chuo kwa mujibu wa taratibu
zilizowekwa.
ii)Wanafunzi
wote wanatakiwa kuripoti kwenye vyuo watakavyopangiwa wakati wa
kufunguliwa kwa muhula (semester) wa pili. Tarehe halisi ya kuanza kwa
muhula wa pili kwa kila chuo watakachopangiwa itatangazwa na kuwekwa
kwenye tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania.
iii)Wanafunzi
wanaosoma shahada ya miaka mitatu ya ualimu wa sayansi katika masomo
yafuatayo watahamishiwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM):
a)Bachelor of Science in Education with Mathematics & Chemistry;
b)Bachelor of Science in Education with Physics & Chemistry, na
c)Bachelor of Science in Education with Physics & Computer Science.
iv)Wanafunzi wanaosoma shahada ya miaka mitatu ya ualimu wa sayansi na Kompyuta (Bachelor of Science in Education with Mathematics & Computer Science) watahamishiwa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha (RUCU):
v)Wanafunzi
wanaosoma shahada ya miaka mitatu ya ualimu wa sayansi katika masomo
yafuatayo watahamishiwa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge
(MWECAU):
a)Bachelor of Science in Education with Physics & Mathematics; na
b)Bachelor of Science in Education with Biology & Chemistry.
vi)Orodha
ya wanafunzi waliohamishwa na majina ya vyuo vikuu walivyohamishiwa
itatangazwa na kuwekwa kwenye tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu hivi punde.
vii)Wanafunzi
wote waliohamishwa ambao hawakukamilisha mitihani yao ya mwisho wa
muhula wa kwanza, au hawakufanya kabisa mitihani hiyo, watatakiwa
kufanya mitihani hiyo katika vyuo vikuu watavyohamishiwa kwa utaratibu
maalum utakaondaliwa na chuo husika.
viii) Kila
mwanafunzi anawajibika kutunza kumbukumbu zake zote muhimu za maendeleo
ya kitaalama kwa ajili ya matumizi ya baadaye, ikiwa ni pamoja na
matokeo ya mitihani aliyokwishafanya.
ix)Wanafunzi
wote ambao ni wanufaika wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu,
mikopo yao itahamishiwa katika vyuo wakapokuwa wamehamishiwa.
7.Kampasi
nyingine za Chuo Kikuu cha SJUIT (Luguruni na Boko – Dar es Salaam; na
Makambako – Njombe) zitaendelea na masomo kama kawaida.
8.Kwa
taarifa hii, vyuo vikuu vyote nchini vinakumbushwa kufuata sheria na
kuzingatia utoaji wa elimu inayokidhi viwango vya ubora vinavyokubalika
kitaifa na kimataifa. Tume haitasita kuchukua hatua stahiki kwa chuo
kikuu chochote kitakachobainika kutoa elimu isiyokidhi viwango vya ubora
kwa kisingizio cha aina yoyote.
PROF. YUNUS D. MGAYA
Katibu Mtendaji
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania
26 Februari 2016
26 Februari 2016
0 comments:
Post a Comment