Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), Profesa Yunus Mgaya.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU),
Profesa Yunus Mgaya, amesema katika ukaguzi wa vyuo vikuu unaoendelea
nchi nzima, wamebaini kasoro mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyuo vyote
kutokuwa na walimu wa kutosha huku vingine vingi vikitumia mitala
isiyoendana na soko la ajira.
Alisema kwa vyuo vingi visivyo vya serikali, kati ya asilimia 60
mpaka 80 ya walimu wake, hawana kiwango cha elimu kinachotakiwa kwa
mwalimu wa chuo kikuu (shahada ya uzamivu).
Ukaguzi wa TCU kwa vyuo vyote nchini, unafuatia Waziri wa Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kuiagiza
taasisi hiyo kufanya ukaguzi kwenye vyuo vikuu vyote na vile
watakavyobaini vimekiuka kanuni za kutoa elimu ya juu, vipewe adhabu
ikiwa ni pamoja na kuvifutia ithibati.
“Ukaguzi umebaini Tanzania kwa ujumla wake kuna upungufu wa walimu
kwenye vyuo vikuu vyote, hakuna kinachojitosheleza kwa walimu, hata Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam na Muhimbili...lakini tulichokiona kweye vyuo
kama cha Dar es Salaam, Muhimbili, St. Augustine na Tumaini, vimekuwa
vinawasomesha walimu wake, vina mradi na bajeti za kusomesha ili wapate
shahada ya tatu ndani na nje ya nchi,” alisema na kuongeza:
“Baadhi ya vyuo vikuu binafsi, wao hawasomeshi, kazi yao ni
kuwavizia wenzao wakisomesha ndipo wawachukue, bahati nzuri hawana fedha
za kuwalipa, maana hawa wakisomeshwa mishahara yao ni mikubwa hawawezi
kuwalipa, wanaishia kuwachukua kwa muda wa ziada,” alisema.
Kuhusu viwango vya elimu vya walimu, Profesa Mgaya alisema: “Ukiona
chuo kina walimu karibu asilimia 60 hadi 80 ni wa shahada ya pili
(shahada ya uzamili) tu, hawana ya tatu (shahada ya uzamivu).
Pia tumebaini vyuo vikuu vinavyofundisha sayansi vina upungufu
kwenye maabara, hakuna vifaa vya kisasa vya kutosha vinavyoendana na
idadi ya wanafunzi. Hii ipo karibu vyuo vikuu vyote binafsi
tulivyovikagua angalau vile vya umma vina mpango wa kutekeleza hilo,”
alisema Profesa Mgaya.
Akielezea kuhusu mitaala alisema baadhi ya vyuo binafsi vimekuwa vikizalisha wahitimu wasioendana na soko.
Alisema wanapobaini upungufu kama huo, hurudi chuoni kuwataka waipitie mitaala yao ili iendane na soko.
Pia alisema changamoto nyingine waliyoibaini ni ufinyu wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa maktaba.
“Lipo tatizo la maktaba siyo kubwa na tatizo la vitabu, mfano UDSM
kinaprogramu ya kuongeza ukubwa wa maktaba yake mara tatu ya iliyopo,
lakini baadhi ya vyuo vikuu binafsi hawana program yoyote,” alisema.
Profesa Mgaya akizungumzia kuhusu ujio wa wanafunzi zaidi ya 100 wa
Chuo Kikuu cha Mt. Joseph Tanzania (SJUIT) kampasi ya Arusha waliokuja
Dar es Salaam ili kueleza changamoto zinazowakabili, alisema bahati
nzuri waliyoyaeleza jopo la wataalam waliotumwa kuchunguza
wameshakabidhi ripoti Jumatatu ya wiki hii.
Alisema wanafunzi hao walibainisha changamoto zao kuwa ni walimu
hawatoshi, wengine hawana viwango, baadhi wakifundisha hawaeleweki kwa
sababu lafudhi zao ni za Kihindi.
Alisema wataalam wa TCU wameshafanya ukaguzi kwenye chuo hicho na
ripoti yake itajadiliwa leo kwenye Kamati ya Ithibati ya Vyuo Vikuu
kisha kutoa mapendekezo ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa.
Alisema uamuzi wa kitakachoafikiwa yatatolewa kwa umma kesho.
Alisema matawi mengine ya chuo hiyo yaliyo Bagamoyo, Luguruni na Boko vya Dar es Salaam, ukaguzi wake umekamilika.
Pia alisema wanafunzi hao wamesema wana tatizo la maabara, maktaba, ada ni kubwa na kuzilalamikia sheria za chuo kuwa ni kali.
Kuhusu ada alisema serikali haijawa na ada elekezi, lakini Aprili 9, mwaka jana walipeleka mapendekezo yao serikalini.
Alisema kutokana na bajeti wakati huo ilikuwa imeshapita, wanatarajia mwaka huu watafanikiwa.
"Changamoto zao serikali tumeshaunda tume ya uchunguzi juzi
Jumatatu jopo lilituletea matokeo, kesho tunaingiza kwenye kamati yetu
ya ithibaki," alisema.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment