Vigogo
watatu wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), akiwemo Mtendaji Mkuu
wa mradi huo, Asteria Mlambo, wamepandishwa kizimbani, kwa tuhuma za
kuisababishia serikali hasara ya Sh milioni 83.5.
Mbali
na Asteria, washitakiwa wengine wanaokabiliwa na mashitaka hayo ya
uhujumu uchumi ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Evodius Katale,
Mwanasheria Mkuu wa mradi huo, Francis Kugesha na Mkurugenzi wa kampuni
ya Yukan, Yuda Mwakatobe.
Walifikishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana na kusomewa
mashitaka matatu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage.
Walisomewa
mashitaka na wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), Jackline Nyantori akisaidiwa na Estazia Wilson na Stellah
Mafuru.
Nyantori
alidai kati ya Septemba Mosi na Oktoba Mosi 2013, Kinondoni Dar es
Salaam, Asteria, Katale na Kugesha wakiwa wafanyakazi wa mradi huo,
walishindwa kutekeleza majukumu yao vizuri na kuisababishia serikali
hasara ya Sh milioni 83.5.
Katika
mashitaka yanayomkabili Mwakatobe, inadaiwa Juni 29, 2005 katika ofisi
za kodi Ilala, Dar es Salaam, alitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa
Mamlaka ya Mapato (TRA), wakati akiwasilisha taarifa ya fedha ya mwaka
2004 na ya 2005 ya kampuni yake ya Yukan Business, jambo lililosababisha
alipe kodi ndogo.
Awali,
Wakili Nyantole alidai kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) amewasilisha
hati ya kuruhusu mahakama hiyo, kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi
hivyo washitakiwa wataruhusiwa kujibu mashitaka yao.
Washitakiwa
walikana mashitaka na upande wa Takukuru ulidai kuwa upelelezi wa kesi
hiyo haujakamilika, pia hawana pingamizi ya dhamana kwa washitakiwa.
Hakimu
Mwijage alisema Asteria, Katale na Kugesha watapata dhamana endapo kila
mmoja atakuwa na mdhamini mmoja anayefanyakazi serikalini au kwenye
taasisi inayofahamika, atakayesaini hati ya Sh milioni 15. Pia kila
mshitakiwa awasilishe Sh milioni 15 au hati isiyohamishika yenye thamani
ya Sh milioni 15.
Kwa
upande wa Mwakatobe, dhamana yake ipo wazi endapo atapata mdhamini
mmoja mwenye barua kutoka taasisi inayofahamika, asaini hati ya Sh
milioni tano.
Wote
waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti. Asteria na Katale
wametakiwa kuwasilisha hati hizo Machi 3 mwaka huu. Kesi itatajwa tena
Machi 9 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment