Monday, 22 February 2016

Bandari wazidi kubanwa

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani ameonya na kuahidi kuwachukulia hatua baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Tanga watakaobainika kuendelea kuhamasisha wananchi waliolipwa fidia kupisha ujenzi wa Bandari ya Mwambani tangu mwaka 2011 wasihame katika eneo hilo.
Ametoa kauli hiyo wakati wa majumuisho ya ziara yake ya siku moja iliyolenga kukagua shughuli za bandari hiyo ambako alitembelea eneo la ujenzi wa bandari mpya ya Mwambani lenye ukubwa wa hekta 174.2 pamoja na mita za kupimia mafuta zilizoko maeneo ya Raskazone na Chumvini.
Naibu Waziri alisema pamoja na serikali kukamilisha malipo ya fidia ya zaidi ya Sh bilioni 2.5 kwa ajili ya TPA kulitwaa eneo hilo kutoka kwa wananchi waliokuwa wakilimiliki awali, amebaini kwamba wapo baadhi ya watumishi wa bandari wanaowashawishi wananchi kutokuondoka katika eneo hilo mpaka sasa ili wadai fidia zaidi.
“Dhamira yetu ya kujenga bandari iko pale pale, ila nasikia uchochezi uko ndani ya wafanyakazi wa hapa bandarini … watu wamelipwa fidia hawajaondoka na wanaowafanya hao wasiondoke wanaowapa matumaini naambiwa ni ninyi wafanyakazi wa bandarini,” alisema Naibu Waziri.
Aliongeza, “Hiyo tabia muiache mara moja ili mtoe fursa kwa serikali pamoja na TPA kutimiza azma yake ya kujenga bandari mpya Mwambani pamoja na reli yake ya kwenda Musoma,” aliongeza Ngonyani.
Alisema serikali itahakikisha ndani ya awamu hii ya tano ya uongozi ujenzi wa Bandari ya Mwambani utatekelezwa na kwamba kazi inayoendelea hivi sasa ni kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Tanga hadi Musoma.
“Kwamba kitakachofuata sasa ni kutafuta fedha za kujenga reli kutoka Mwambani hadi Musoma… tukijenga hiyo reli tutakuwa tumefungua biashara ya Bandari ya Mwambani,” alieleza.
Akizungumzia matumizi ya mita za kupimia mafuta wakati wa ushushaji wa mafuta kupitia Bandari ya Tanga ambayo imefungiwa tangu mwaka 2011 mpaka sasa, alitaka TPA kukamilisha haraka marekebisho katika mita hizo zilizoko eneo la Raskazone ili zitumike katika shehena inayotarajiwa kushushwa mapema mwezi ujao.
“Mimi naamini wanaozuia flow meters kutotumika ni sisi…wanaonufaika na hilo ni wafanyabiashara wa mafuta wanaotumia nguvu zao kupitia sisi humu humu ndani,” alisema Naibu Waziri na kuongeza: “Maamuzi mbalimbali ya kipuuzi yamefanyika kama huo uamuzi wa kuzifungia hizo flow meters zisitumike tangu mwaka 2011. Ni uamuzi wa kipuuzi ukiuchunguza kwa makini utabaini sisi wote tunahusika kwa sababu ulipotolewa mwaka huo mpaka sasa hakuna mtumishi yeyote wa bandari aliyethubutu kuupigia kelele.”
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Tanga, Mussa Mbaruku ameiomba TPA na Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Tanga kushughulikia tatizo la matumizi ya mita za mafuta ili zisaidie kuongeza mapato mkoani humo.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger