TAARIFA KWA UMMA
MGOGORO WA CHUO KIKUU CHA MT. YOSEFU TANZANIA(SJUIT) KAMPASI YA ARUSHA
1.
Tunapenda kuuarifu umma kwamba, Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu
Tanzania (SJUIT) Kampasi ya Arusha ni mojawapo ya vyuo vikuu
vilivyosajiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ambacho kilianza
kudahili wanafunzi kwa mara ya kwanza mwaka wa masomo 2013/2014.
2.
Kwa mujibu wa kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura ya 346 ya
Sheria za Tanzania, Tume ina mamlaka ya kusimamia na kudhibiti ubora na
usimamizi wa uendeshaji wa Vyuo Vikuu hapa nchini.
3.
Tume inatambua kuwa kwa nyakati tofauti kumekuwapo na matukio
ya migogoro baina ya uongozi wa Chuo Arusha na wanafunzi.
Tume
imekuwa ikifuatilia kwa karibu chimbuko la migogoro hiyo na kuchukua
hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kutoa maelekezo kwa uongozi wa chuo
kurekebisha kasoro zinazosababisha migogoro chuoni hapo.
Katika
kutekeleza azma hiyo, hivi karibuni Tume iliunda jopo la wataalam
kufanya ukaguzi wa kina katika Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu Tanzania
Kampasi ya Arusha. Ripoti ya ukaguzi huo iliwasilishwa tarehe
22/02/2016.
4.
Kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa kisheria, ripoti hii inatakiwa
kuwasilishwa na kujadiliwa na Kamati ya Ithibati ya Tume ya Vyuo Vikuu,
ambayo itatoa mapendekezo kwa Tume kuhusu hatua stahiki za maamuzi.
Kamati hii itakutana katika kikao cha dharura tarehe 25/02/2016 saa 3:00
asubuhi, na taarifa ya Kamati hiyo itawasilishwa kwenye Mkutano
wa dharura wa Tume tarehe hiyohiyo saa 9:00 alasiri.
5.
Kwa mantiki hiyo, taarifa rasmi kuhusu maamuzi yaliyofikiwa juu ya
hatma ya Kampasi hiyo ya Arusha ya Chuo cha Mt. Yosefu itatolewa siku ya
Ijumaa tarehe 26/02/2016.
6.
Kwa taarifa hii, Tume inawaomba wanafunzi wote wa Chuo cha Mt. Yosefu
Kampasi ya Arusha kuwa watulivu wakati huu ambapo suala lao
linashughulikiwa.
7.
Tume inapenda kutumia fursa hii pia kuwaarifu wanafunzi wote wa
vilivyokuwa Vyuo Vikuu Vishiriki vya Sayansi za Kilimo na Teknolojia
(SJUCAST) na Teknolojia ya Habari (SJUCIT), kuwa orodha ya majina yao na
vyuo walivyopangiwa inapatikana katika tovuti ya Tume ya Vyuo
Vikuu. Hivyo wanashauriwa kuondoka Chuoni mara moja na kujiandaa kwa
ajili ya kuripoti katika vyuo walivyopangiwa katika muhula wa pili.
Imetolewa na
PROF.
YUNUS
D. MGAYA
Katibu
Mtendaji
Tume
ya Vyuo Vikuu Tanzania
24 Februari 2016
0 comments:
Post a Comment