Waziri zamani, Joseph Mungai amerejesha sehemu ya ardhi ya Hospitali ya
Wilaya ya Mufindi, aliyodaiwa kuihodhi kinyume cha sheria.
Baada
ya hatua hiyo ya Mungai ambaye aliwahi pia kuwa Mbunge wa Mufindi,
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Dk Hamisi Kigwangalla ametoa siku saba
kwa uongozi wa hospitali hiyo kujenga uzio ili kulinda mipaka yake.
Pia,
ameutaka kupeleka ofisini kwake, ramani ya eneo lote la hospitali hiyo
na taarifa itakayobainisha kumalizika kwa mgogoro huo.
“Haya ni
mambo ya kisheria, isije ikawa leo mnasema mgogoro umekwisha halafu
kesho tukasikia mzee Mungai kaenda mahakamani,” alisema Dk Kigwangalla.
Alizitaka
halmashauri zote nchini kulinda maeneo yake kwa kuhakikisha
yamesajiliwa na yana hati ili inapokuja mipango ya kuboresha au kutanua
matumizi kusiwapo na changamoto.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya
Mufindi, Jowika Kasunga alitoa taarifa ya kurejeshwa kwa eneo hilo na
kusema lipo nyuma ya hospitali hiyo, mjini Mafinga.
Akizungumzia
mipaka ya kiwanja cha hospitali hiyo baada ya waziri huyo kutaka kujua
kama haijakumbwa na uvamizi kutoka kwa wananchi, Kasunga alisema eneo
hilo lilikuwa na mgogoro wa muda mrefu baada ya Mungai kudai analimiliki
kihalali.
Hata hivyo, alisema mgogoro huo umemalizika baada ya Mungai kuamua kulirejesha hospitalini.
Mbunge wa Mafinga Majini, Cosato Chumi alisema eneo hilo lilitengwa kwa ajili majengo ya uzazi.
“Nashukuru mzee wetu ameamua kulirejesha eneo hilo na sasa lipo mikononi mwa Serikali,” alisema Chumi.
Katika
hatua nyingine, Dk Kigwangalla alitoa miezi mitatu kwa Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Shaibu Nnunduma kukamilisha ukarabati wa
vyumba vya upasuaji ambavyo hali yake ni mbaya vinginevyo, atatumbuliwa
jipu.
Alisema kama angetembelea hospitali hiyo akiwa mkaguzi, angelazimika kufunga vyumba hivyo kutokana na hali yake kutoridhisha.
“Nimekagua
na kujionea hospitali hii, kuna maeneo ya changamoto ikiwamo vyumba
vyake vya upasuaji, nyie mnaona kama mnavyo lakini kiukweli ni kama
hamna kwani vilivyopo vinafanana na stoo, siyo kipimo chake,” alisema Dk
Kigwangalla.
0 comments:
Post a Comment