Monday 1 February 2016

True Memories Of My life – 46

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Wiki iliyopita niliishia nilipokuwa nasema kuwa bunduki sizilaumu kwa uhalifu unaoendelea nchini, maana hazina uwezo wa kujifyatua, bali nalaumu mikono ya vijana wetu inayozigusa bunduki hizo na kufyatua! ninachoiomba serikali ya awamu ya tano ni kufanya kile kila kinachowezekana kutengeneza mazingira ya vijana kufanikiwa, tuendelee kubana matumizi, ufisadi lakini pia tutengeneze njia za kuleta mzunguko wa fedha. SASA ENDELEA…
Watu wa Ruangwa, jimboni kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wapo katika hali mbaya, mvua kubwa imenyesha na mafuriko yametokea, pamoja na nyumba nyingi kubomolewa na nyingine kuezuliwa mapaa! Ni tukio baya ambalo limewafanya watu zaidi ya 500 kukosa makazi. Tukio hili lilitokea takribani wiki mbili zilizopita.
Januari 28, 2016, nipo ofisini kwangu nikimsubiri Mzee Hanga, ambaye ni mmoja wa wanakamati iliyoundwa kwa ajili ya kukusanya fedha ambazo zitawasaidia watu wa Ruangwa kwenye tatizo lililokuwa limewakuta, mimi pia ni mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambayo pia yumo Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mama Mtima.
Pamoja na kazi nyingi ofisini kwangu, siku hizi ni lazima nitenge muda kwa ajili ya kuzunguka kwenye ofisi mbalimbali jijini Dar es Salaam kuomba msaada, juzi tu nilikuwa Ofisi za Kampuni ya Bia na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, kote huko kutafuta misaada kwa ajili ya wananchi wa Ruangwa ambao hivi sasa wanateseka.
Namsubiri Mzee Hanga kwa sababu tuna ahadi ya kwenda pamoja ofisi za MMI Steel, watengenezaji wa mabati, misumari, vinywaji vya Sayona, maji ya kunywa na pia wanamiliki Hoteli za Sea Cliff, White Sands na majengo mengi jijini Dar es Salaam.
Tuna ahadi ya kuonana na mmiliki wa kampuni hiyo, Bw. Subash Patel, ambaye kwa miaka mingi nimesikia juu ya utajiri wake lakini hata siku moja sikuwahi kukutana naye ana kwa ana! Ambacho nafahamu kutoka kwa watu wengine kuhusu mtu huyu ni mpole, mkarimu, mwenye kujishusha ambaye hafanani kabisa kama ukikutana naye barabarani na utajiri alionao, nina hamu kubwa ya kukutana na mtu huyo, ahadi yetu ni kukutana naye saa kumi kamili ofisini kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam, mita kama mia mbili hivi kutoka ofisini kwangu.
Saa tisa na nusu napigiwa simu na sekretari wangu ambaye ananitaarifu kuwa Mzee Hanga amekwishafika, nilichokifanya ni kumuomba amlete ofisini kwangu! Mzee huyu ni mcheshi na anapenda utani, alipoingia ofisini kwangu akiwa ameongozana na Subira ambaye ni sekretari wangu, alifanya matani mawili matatu na binti huyo kabla hajaketi na kuanza kuongea.
“Swahiba, nashukuru sana bwana dua zako zimesaidia ule mfupa ulionikwama umeondoka!” ndiyo maneno aliyoanza nayo baada ya kusalimiana.
Mzee Hanga alipatwa na tatizo la kukwamwa na mfupa wa samaki kooni, tatizo ambalo lilimsumbua kwa muda katika hospitali kadhaa, aliponieleza mimi niliongea kwa kujiamini kwamba “Mfupa huo kwa jina la Yesu kesho hautakuwepo!” Ingawa kesho yake ulikuwa bado upo kooni, siku iliyofuata ambayo ndiyo alikuwa ameketi mbele yangu mfupa ulitoka wenyewe.
Tuliongea mengi kuhusu kazi tuliyokuwa tukiifanya ya kukusanya misaada ya kuwasaidia watu wa Ruangwa, saa tisa na dakika arobaini na tano ndipo tuliondoka ofisini kwangu moja kwa moja hadi MMI Steel, ambako tulikaribishwa ofisini kwa Bw. Subash ambaye hakika alitupokea kwa furaha kubwa tofauti kabisa na matajiri wengi niliowahi kukutana nao.
Mambo yote yaliyokuwa yakiongewa kuhusu Subash yalikuwa ni kweli, alikuwa mpole, mcheshi, asiye hata na chembe ya dharau pamoja na utajiri wote aliokuwa nao! Moyoni mwangu nikajisemea “Laiti matajiri wote wangekuwa hivi…” Tuliongea naye juu ya lengo la kumuona, akatuhakikishia kwamba angewasaidia watu wa Ruangwa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh. milioni hamsini! Moyoni nikamshukuru Mungu, nilijua angetusaidia lakini sikuwa nimewaza kwamba Mungu angemuongoza atusaidie kiasi kikubwa namna hiyo.
Tulimshukuru kwa moyo wake wa kuwa tayari kutumia utajiri wake na watu ambao hawajabarikiwa kama yeye, kama ilivyo kawaida yangu, kila ninapokutana na tajiri huwa ni lazima nimuulize jinsi ya kuwa kama yeye, siwezi kuondoka bila kujifunza kitu kwa sababu mimi sikukaa sana darasani kujifunza kama ilivyo kwa wasomi wengi.
“Naomba nikuulize swali Subash, unawezaje kuzisimamia mali zote ulizonazo na bado ukaendesha maisha ya furaha?”
“Siku zote namuweka Mungu mbele, yeye ndiye kila kitu katika maisha yangu, naswali asubuhi na jioni nikimuomba anisaidie katika kazi zangu, lakini pia nafanya kazi na watu waaminifu na wenye akili huku nikiwalipa vizuri na kuwafuatilia!”
“Kama ungekuwa unaanzisha kiwanda leo, ungeanza na kutengeneza bidhaa gani?”
“Nitaangalia mahitaji yaliyopo, kisha nitaanza kidogo na baadaye kuendelea kukua, start small, think big and grow rich!” alisema Bw. Subash kwa sauti ya unyenyekevu.
Baada ya hapo tuliongea mambo mengi kuhusu biashara na nchi yetu kwa jumla, nikagundua nilikuwa naongea na Mtanzania anayeipenda nchi yake pamoja na kuwa ana asili ya India, nilishangaa aliponiambia yeye ni mzaliwa wa Chalinze, Kijiji cha Lugoba ambako alisoma mpaka darasa la nne na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete.
Tuliondoka ofisini kwa Subash tukiwa na furaha mno kwamba matatizo ya watu wa Ruangwa hatimaye yalikuwa yanakwenda kutatuliwa kwa misaada tuliyokuwa tukiikusanya, wakati naingia ofisini kwangu kutoka ofisini kwa Subash ilikuwa tayari saa kumi na mbili kasoro, sikuwa tena na nguvu za kufanya kazi, nilishachoka tayari na mambo ambayo nilishayafanya siku nzima.
Hata hivyo, sikuondoka ofisini, nilibaki nikisoma baruapepe na kujibu barua za mashabiki wangu mpaka saa mbili za usiku nilipoondoka kwenda nyumbani kwa mama yangu kabla sijaelekea nyumbani kwangu Kijitonyama, mke wangu alinipokea vizuri nikamweleza habari za siku nzima, alishangaa ukarimu wa Subash Patel, mtazamo wake kuhusu Waasia ukabadilika.
Kwa sababu ya kuchoka sana siku hiyo niliingia kitandani mapema, kabla sijasinzia, majira ya saa nne hivi usiku, simu yangu iliita, nikanyanyuka na kwenda kuiangalia, kwenye kioo nilisoma maandishi “Mrisho” hili ni jina la Meneja Mkuu wa kampuni yetu, moyo ukashtuka sana kwa sababu mimi na Mrisho huwa hatuna tabia ya kupigiana simu na kuelezana mambo ya kipuuzi, ni kazi tu!
“Mungu wangu, sijui kuna nini!” nilisema mke wangu akisikia.
“Nini?”
“Mrisho!” nikajibu, kumbukumbu zikanijia kichwani kwamba Mrisho aliondoka ofisini mapema sana siku hiyo akinitaarifu kuwa kaka yake, Dawood Mrisho alikuwa mgonjwa na alipelekwa Hospitali ya Tumaini kwa matibabu.
“Pokea tu!”
“Lazima kuna tatizo, kaka yake alikuwa mgonjwa, isije kuwa kimetokea kitu kibaya!” nilisema na kuipokea simu hiyo.
Alichonielezea Mrisho kwenye simu ni kwamba hali ya kaka yake ilikuwa imebadilika na kuwa mbaya, hivyo alikuwa akiniulizia kama nilimfahamu daktari yeyote Hospitali ya Muhimbili ili wamhamishe Hospitali ya Tumaini ambako huduma zilikuwa mbaya.
“Nakuja kaka, tukutane Muhimbili Idara ya Wagonjwa wa Dharura!” nilisema.
Nilichokifanya ni kuvaa haraka na kumuaga mke wangu ambaye alitaka kuongozana na mimi lakini nilimkatalia kwa sababu bado alikuwa akiumwa kichwa na pia siku iliyofuata alikuwa na kazi nyingi sana za kufanya ofisini kwake, alichokifanya ni kunisindikiza hadi mlangoni, akanipiga busu la shavuni, nami nikafanya hivyo tukaagana.
Nikaingia kwenye gari na kuwasha, walinzi wakafungua lango na nikatoka kwa kasi na kuendesha hadi Muhimbili ambako nilimkuta Mrisho na kaka yake, Dawood wakiendelea kufanyiwa vipimo, alikuwa kwenye mashine ya oksijeni ambayo alidai ilikuwa haisaidii chochote katika kuhema, pumzi ilikuwa haitoshi!
Daktari aliyekuwa akimtibu alikuwa kijana mdogo, ambaye alikiri kwamba wakati akisoma shule ya msingi alikuwa msomaji sana wa maandishi yangu na alifurahi mno kuniona siku hiyo. Tukampeleka mgonjwa kufanya kipimo cha X-Ray ya kifua na kumrejesha tena wodini, mpaka kila kitu kinakamilika na kupewa dawa kisha kupelekwa Wodi ya Mwaisela kulazwa, ilikuwa ni saa kumi za usiku!
Ndipo nikarejea nyumbani kupumzika, saa kumi na mbili nilikuwa macho tayari kwa kuwapeleka watoto wangu shule, nilitamani kuendelea kulala lakini haikuwezekana, haraka nikakimbia bafuni nikajimwagia maji ili kuondoa usingizi! Saa moja na nusu nilishawafikisha watoto shule na kuelekea ofisini ambako niliendelea na kazi mpaka saa tatu na nusu, Mrisho aliponipigia simu akinitaarifu kuwa, kaka yake Dawood hatimaye alikuwa amefariki dunia.
“Nakuja kaka!” ndiyo maneno pekee niliyosema na kukata simu.
Nikaondoka ofisini na Mhariri Mtendaji, Richard Manyota, Mhariri wa Gazeti la Championi Ijumaa, John Joseph, Mhariri wa Gazeti la Risasi Jumamosi, Erick Evarist na Mhariri wa Gazeti la Uwazi, Elvan Stambuli hadi chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Muhimbili ambako nilimkuta Mrisho, tukakumbatiana na wote tukalia kwa uchungu, kifo cha Dawood kilikuwa kimemuumiza kila mmoja wetu kwa namna yake.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger