Monday 22 February 2016

Vita ya ubunge yahamia kortini

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

MASHAURI 13 ya uchaguzi wa wabunge yanatarajiwa kuanza kunguruma leo katika kanda mbalimbali za Mahakama Kuu ya Tanzania nchini.
Miongoni mwa mashauri yatakayonguruma ni yale yaliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila, aliyekuwa mgombea ubunge Iringa Mjini Fredrick Mwakalebela, aliyekuwa Mbunge wa Kahama James Lembeli, aliyekuwa Mbunge wa Nyamagana Ezekiel Wenje na aliyekuwa Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Msajili wa Mahakama Kuu, Ilvin Mugetta wiki iliyopita, mashauri hayo yataanza kusikilizwa kwa njia ya vikao vya Mahakama Kuu katika vituo mbalimbali vya Mahakama hiyo nchini.
Mugetta alizitaja kesi zitakazoanza kusikilizwa kuwa ni kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa Longido yaliyompa ushindi Onesmo ole Nangole (Chadema) iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Stephen Kiruswa.
Itasikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha. Aidha, alisema kesi nyingine ni ile ya kupinga matokeo ya uchaguzi iliyofunguliwa na Benedicto Mutungirehi (Chadema) dhidi ya mshindi wa ubunge katika Jimbo la Kyerwa, Innocent Bitakwate (CCM). Kesi hiyo itasikilizwa Bukoba.
Mkoani Iringa, pia kutakuwa na kesi iliyofunguliwa na Mwakalebela ya kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompatia ushindi wa ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).
Alitaja kesi nyingine kuwa ni ya kupinga matokeo ya ubunge inayomkabili Mbunge wa Njombe, Edward Mwalongo (CCM) iliyofunguliwa na Emmanuel Godfrey (Chadema).
Kesi nyingine ni ile ya kupinga matokeo ya ubunge katika Jimbo la Mafinga, iliyofunguliwa na William Mungai (Chadema) dhidi ya mbunge wa jimbo hilo, Cosato Chumi wa CCM.
Pia kesi iliyofunguliwa na Zella Abraham ya kupinga matokeo ya ubunge Mbeya Vijijini dhidi ya Oran Njeza nayo itasikilizwa na kesi nyingine ni iliyofunguliwa na Fanuel Mkisi dhidi ya ushindi wa ubunge katika Jimbo la Vwawa wa Japhet Hasunga. Kesi hizi zitasikilizwa Mbeya.
Aidha, kesi nyingine zitakazoanza kusikilizwa siku hiyo ni pamoja na kesi dhidi ya Mbunge wa Newala, George Mkuchika iliyofunguliwa na Juma Manguya anayepinga ushindi wa mbunge huyo na kesi iliyofunguliwa na Mangungu dhidi ya ushindi wa matokeo ya ubunge Kilwa yaliyompatia ushindi Vedastor Ngombale wa CUF.
Pia Msajili huyo alisema kesi nyingine ni ile iliyofunguliwa na Wenje ya kupinga matokeo yaliyompatia ushindi Stanslaus Mabula (CCM) itakayosikilizwa Mwanza wakati kesi iliyofunguliwa na Lembeli ya kupinga matokeo ya ubunge Kahama yaliyompatia ushindi Jumanne Kishimba itasikilizwa Shinyanga.
Kesi nyingine zilizopangwa kusikilizwa ni iliyofunguliwa na Kafulila kupinga matokeo ya ubunge Kigoma Kusini yaliyompatia ushindi Husna Mwilima wa CCM na kesi yao itasikilizwa Tabora wakati kesi iliyofunguliwa na Amina Mwidau kupinga matokeo ya ubunge Pangani yaliyompatia ushindi Jumaa Aweso wa CCM itasikilizwa Tanga.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo mbali na washindi wa ubunge ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo husika.
Hivi karibuni, Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman alisema tayari Mahakama hiyo imejipanga kumaliza kesi zote za uchaguzi hadi Juni mwaka huu, na imejipanga kusikiliza kesi 20 za wabunge.
Tangu uchaguzi huo umalizike Oktoba mwaka jana, jumla ya kesi 221 zilifunguliwa kati ya hizo 53 ni za ubunge na 173 madiwani na jumla ya Sh bilioni tatu zinahitajika kukamilisha usikilizaji wake.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger