Thursday 25 February 2016

Chanzo cha Mgomo Chuo Kikuu St. Joseph Hiki Hapa

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY


Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya

WANAFUNZI 1,548 wa Chuo Kikuu cha St. Joseph tawi la Arusha, wamegoma kuingia darasani kwa siku tatu na kukodi mabasi matatu kwenda Dar es Salaam kumwona Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.

Lengo la safari yao hiyo ya Dar ni kujua hatma yao, baada ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), kufungia chuo hicho tawi la Songea.

Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya, alibainisha kuwa hatma ya chuo hicho, itatolewa rasmi kesho baada ya tume hiyo kupitia mapendekezo ya tume ya wataalamu iliyoundwa mapema kwa ajili ya ukaguzi wa chuo hicho, tawi la Arusha.

Kulikuwa na vurugu miongoni mwa wanafunzi juzi jioni, hali iliyofanya uongozi kufikia uamuzi wa kufunga chuo hicho kwa muda usiojulikana. Wakizungumza jana kabla ya kuanza safari kwenda Dar es Salaam kumwona Waziri Ndalichako, wanafunzi hao walisema mmiliki wa St. Joseph ni mmoja, hivyo kama tawi la Songea lina shida ni wazi matawi yote nchini yana shida.

Waliomba serikali kutoa ufafanuzi, kabla ya kuendelea kupoteza fedha za umma walizopatiwa kama mikopo.

“Pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu kutoa waraka kwenye mtandao kuwa kufungwa kwa chuo cha Songea, hakuhusiani na matawi ya chuo hicho, lakini sisi hatuna hakika tunataka watu hakikishie kama tupo salama,” alisema mwanafunzi Joel Lameck.

Aliendelea kusema, “na tukimaliza masomo yetu, je, tutapata ajira serikalini, yasije yakatukuta ya Chuo cha St. John cha Dodoma ambao hawakupata ajira kwa sababu elimu waliyopata haikuwa na viwango.”

Wanafunzi hao ambao wengi wao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini, walisema wamekuwa wakilalamika mara kwa mara kuwa chuo hicho kina upungufu mwingi, ikiwemo uhaba wa vifaa vya kufundishia.

Pia wanafunzi hao walihoji sababu za serikali, kutowaleta wanafunzi wa tawi la Songea iwapo tawi lao la Arusha lipo salama, badala yake wamepelekwa vyuo vingine, nje ya St Joseph.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Siles Balasingh, aliomba serikali kutoa majibu haraka kwa wanafunzi hao wanaosomea ualimu wa masomo ya Sayansi, waendelee na masomo yao, kwani wamepata wasiwasi baada ya kufungwa tawi la Songea, japo hawana shida na chuo.

Alisema wao kama chuo, wamejitahidi kubandika chuoni hapo tangazo la TCU kwamba tawi hilo halihusiki na matawi mengine, lakini wanafunzi hawaelewi, wamegoma kuingia darasani, pia wameharibu mali za chuo.

“Hawa wanafunzi leo siku tatu hawataki kuingia darasani na wamekodi mabasi matatu wanaelekea Dar es Salaam kumwona waziri, lakini wamewapiga baadhi ya wanafunzi wenzao kwa kuwakataza kufanya mitihani mpaka wapate uhakika wa masomo tunayowapatia kama tumekidhi vigezo vya mitaala ya elimu,” alisema.

Alisema walimu wanasikitika kuona vurugu zinatokea kwa sababu hiyo, hivyo ikiwezekana wanamwomba waziri wa elimu afike chuoni hapo, kutoa ufafanuzi ili wanafunzi wao hao wapatao 1,518 waendelee na masomo yao.

Hatma ya chuo kujulikana Ijumaa

Akihojiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dar es Salaam jana, Profesa Mgaya alisema mgogoro wa chuo hicho, ulianza muda mrefu tangu mwaka 2014, hali iliyosababisha tume hiyo kufanya ukaguzi chuoni hapo.

“Tume iliunda timu ya wakaguzi iliyoongozwa na maprofesa wa taaluma mbalimbali, waliokagua mfumo wa ufundishaji, mazingira ya ufundishaji na kuhoji wanafunzi chuoni hapo. Tayari timu hii imewasilisha ripoti yake kwa TCU,” alisisitiza.

Alisema leo tume hiyo inatarajia kukutana na timu hiyo na Kamati ya Ithibati majira ya saa 3 asubuhi, kuijadili ripoti ya ukaguzi wa chuo hicho na saa 9 mchana itaitisha mkutano wa dharura kujadili mapendekezo ya taarifa hiyo na kutoa maamuzi dhidi ya chuo hicho.

“Tutautangazia umma Ijumaa (kesho) majira ya saa nne asubuhi kuhusu hatma ya chuo hiki cha St Joseph tawi la Arusha.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger