Thursday 25 February 2016

Wadaiwa 16 Waliotorosha Makontena Bandarini Kuanza Kufilisiwa Leo

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Wadaiwa 16 waliokwepa kulipa kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), baada ya kutorosha kontena za mizigo yao kwenye Bandari Kavu (ICD) ya Azam mwishoni mwa mwaka jana, mali zao zinaanza kukamatwa leo na kufilisiwa.

Mkurugenzi wa Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono, iliyopewa kazi ya kufuatilia wadaiwa hao wakiwemo baadhi ambao wamekamilisha malipo, Yono Kevella alisema hayo Dar es Salaam jana.

Kevela alisema kuanzia leo wanakaa na vyombo vya dola, kuanza utaratibu wa kukamata na kufilisi mali za wahusika na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Kevela alisema hadi sasa hakuna zuio lililotolewa, linazowazuia kutekeleza wajibu wao katika kukusanya madeni hayo. Hata hivyo alisema, wengi wa wadaiwa baada ya kutolewa kwa muda huo wa siku 14, wameonesha moyo wa kulipa.

Wadaiwa 16 hawajamaliza madeni
Alitaja wadaiwa 16 ambao hawajalipa madeni yao wala kupunguza, ambao watafilisiwa wasipojitokeza kufanya malipo ni Said Ahmed Said Sh 28,249,352.50, Strauss International (45,393,769.95), Farid Abdallah Salum (52,185, 614.97).

Wengine ni Nasir Saleh Mazrui (60,105,873.77), Simbo Yona Kimaro (64,221,009.10), Ally Masoud Dama (102,586,719.22) na Juma Kassem Abdul (130,182,395.12), Salum Link Tyres (233,447,913.31) na Tybat Trading Co.Ltd (448,690,271.90).

Pia wamo IPS Roofing Co.Ltd (966,723,692.10), Tuff Tyres General Co Ltd, (7,435,254,537.03), Swalehe Mohamed Swalehe (34,687,165.00), Rushwheel Tyre General Co Ltd, (1,802,988,679.20), Said Ahmad Hamdan (68,362,558.31), Ahmed Saleh Tawred ( 59,237,578.40) na Farida Abdullah Salem Sh 75,334,871. 85.

Akizungumzia wadaiwa waliolipa ndani ya siku 14 walizopewa na zikaisha juzi, alisema wanane kati ya 24, ndiyo walijitokeza kulipa madeni baada ya kampuni yake kuwafuatilia.

Kevela alisema hadi jana zaidi ya Sh milioni 200 zimelipwa na wadaiwa hao.

Wadaiwa hao 24 walishindwa kulipa kodi kwa wakati kama walivyotakiwa kufanya, ndipo TRA ilimpa dalali huyo kazi ya kuwafilisi. Kampuni hiyo ya udalali ilitoa siku 14, kuanzia Februari 10, mwaka huu wawe wamekamilisha; muda ambao umeisha juzi.

Kevela alisema katika siku hizo 14, kati waliojitokeza kulipa,wanne kati yao wamemaliza madeni na wengine wanne wamepunguza madeni na kuahidi kumalizia kiasi kilichobaki.

Waliomaliza madeni yao
Wadaiwa waliolipa madeni yao yote ni Issa Ali Salim aliyekuwa akidaiwa Sh 94,543,161.96, Libas Fashion (26,593,245.78), Omary Hussein Badawy (21,346,615.40) na Zulea Abas Ali (16,760577.24).

Waliopunguza madeni yao
Waliopunguza madeni yao ni Zuleha Abbas Alli aliyelipa Sh milioni 47 na kubakiwa na deni la Sh 28,508,551, awali alikuwa akidaiwa Sh 75,508,551.88, mwingine ni Ally Awes Hamdani aliyelipa Sh milioni 17.26 awali alikuwa akidaiwa Sh 55,485,904.07).

Wengine waliopunguza kidogo ni Tifo Global Trading Co Ltd waliolipa Sh milioni mbili ilhali deni lao ni Sh 1,573,300,644.58, Lotai Steel Tanzania Ltd, waliolipa Sh milioni mbili ilhali deni lao ni Sh 5,476,475,738.19.

“Tulikabidhiwa wadaiwa 24 na TRA, waliokwepa kodi kwa kutorosha kontena katika bandari kavu ya Azam mwishoni mwa mwaka jana, sasa walipewa muda wa kulipa ila walikaidi, tukakabidhiwa tuwafilisi mali zao zote ili kulipia madeni na wamejitokeza hao na kuanza kulipa wengine wamemaliza”, alisema Kevela.

Awali wadaiwa 24, walikwepa kodi ya Sh bilioni 18.95 kwa kutorosha makontena 329 ya bidhaa zao kutoka Kampuni ya SSB ambayo ndiyo mmiliki wa bandari kavu ya (Azam ICD) na kampuni ya Regional Cargo Services.

Mapema Desemba mwaka jana aliyekuwa Kaimu Kamishna wa TRA, Dk Philip Mpango alizungumza na waandishi wa habari na kusema kampuni 15 kati ya 43, zilizokwepa kodi baada ya kutorosha kontena 329 katika ICD ya Azam, wamelipa.

Dk Mpango alisema Desemba 12, mwaka jana ndiyo ilikuwa siku ya mwisho aliyotoa Rais John Magufuli ya siku saba kwa wakwepa kodi hao 43, kulipa wenyewe kwa hiari, vinginevyo sheria zitachukua mkondo wake. Kufuatia kauli hiyo ya Rais Magufuli, wadaiwa 15 walijitokeza na kulipa na waliobaki hawakujitokeza kulipa.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger