Monday 29 February 2016

Halmashauri Ya Jiji la Tanga Hatarini Kufutwa

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Wakati sakata la kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam likiendelea kupamba moto baada ya mchakato huo kuwekewa zuio la mahakama juzi, serikali imetishia kuivunja Halmashauri ya Jiji la Tanga iwapo haitamaliza mgogoro wake wa kisiasa.

Akizungumza na viongozi serikali na kisiasa jijini Tanga jana, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema serikali italazimika kuivunja halmashauri hiyo endapo mgogoro huo hautamalizwa haraka, kutokana na ukweli kwamba tangu kuanza kwa uongozi wa awamu ya tano baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana imeshindwa kufanya vikao vyake halali kwa mujibu wa katiba kutokana na mgogoro wa kisisa bina ya Chama Chama cha Mapinduzi (CCM) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa, huku wananchi wakishindwa kutatuliwa kero zao kwa wakati hivyo kuzorotesha maendeleo yao.

“Mpaka sasa jiji la Tanga hakuna uongozi uliosimama, sasa hatuwezi kwenda kwa mwendo huu, wananchi wanahitaji maendeleo na kurudia uchaguzi hatuwezi ni gharama kubwa, kilichobaki ni kuivunja halmashauri mpaka hapo muda wa kufanya uchaguzi kwa mujibu wa katiba ya nchi utakapotimia, hivyo kwa maana nyingine kama itavunjwa serikali kuu ndiyo itasimamia shughuli za jiji hili,” alisema Suluhu.

Alisema mkoa huo una mipango mbalimbali ya maendeleo lakini haiwezi kutekelezeka kutokana na mgogoro uliopo na kuwataka viongozi wa mkoa kwa kushirikiana na wazee kukaa chini kutafuta namna ya kuumaliza haraka.

“Jiji ni kioo cha mkoa mzima, sasa kama wazee hawatakaa kitako na viongozi kutafuta suluhu, basi hii mipango yenu yote ya kufufua viwanda itakuwa ni ndoto tu kwa sababu hapa mjini hakupo shwari na tunalitambua hilo,” alisema.

Mgogoro wa umeya Tanga umeibuka baada ya CCM yenye madiwani wachache kushinda nafasi hiyo dhidi ya Ukawa yenye madiwani wengi jambo ambalo linapingwa na umoja huo unaondwa na vyama vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD.

Hatua kama hiyo ya kuvunja halmashauri si mara ya kwanza kutokea nchini, kwani mwaka 1996, Halmashauri ya Jiji la Dar  es Salaam ilivunjwa na serikali na badala yake ikaundwa Tume ya Jiji iliyokuwa chini ya Charles Keenja.

Makamu wa Rais pia alisema mkoa wa Tanga unakabiliwa na changamoto kubwa ya biashara ya magendo, hali ambayo inarudisha nyuma mkoa huo kiuchumi na kimaendeleo.

Kufuatia hatua hiyo aliiagiza kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo kutumia kila mbinu kuzuia biashara hiyo ili mkoa uweze kuimarika kiuchumi na kimapato.

Kuhusiana na suala la chakula, Makamu wa Rais alisema serikali ya awamu ya tano haitamvumilia mkuu wa mmoa yeyote wala wilaya ambaye atatoa malalamiko ya kukosekana kwa chakula kwenye eneo lake na badala yake atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe.

Alisema kukosekana kwa chakula wakati viongozi wa eneo husika wana uwezo wa kujenga malambo ili kukinga maji ya mvua kipindi cha masika na kuwaelekeza wananchi kulima mazao yanayostahimili ukame, itakuwa ni kipimo chao cha uongozi na wale ambao watashindwa kupata madawati kwa ajili ya shule kwenye maeneo yao.

Awali akisoma taarifa ya mkoa wa Tanga kwa Makamu wa Rais, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza, alisema hali ya chakula mkoani humo hadi kufikia mwezi huu si ya kuridhisha kutokana na kuchelewa kunyesha kwa mvua msimu wa mwaka 2014/2015 na hata ziliponyesha hazikuwa na mtawanyiko mzuri.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger