Tuesday 23 February 2016

Magufuli Atinga GHAFLA Kivukoni

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY



Rais John Magufuli ameendelea kufanya ziara za kushtukiza, baada ya kutembelea ofisi za Kivukoni Dar es Salaam kimyakimya juzi jioni kuangalia mwenendo wa utoaji huduma za vivuko.

Mashuhuda waliokuwepo eneo hilo Jumapili jioni wakati Rais anafanya ziara hiyo, walieleza mtindo alioingia nao Dk Magufuli ulikuwa ni wa kawaida na vigumu kwa mwananchi wa kawaida kung’amu uwapo wa Rais.

Mfanyabiashara wa eneo hilo, Sharif Mkamba alisema Rais Magufuli aliingia saa 11 jioni akiwa na msafara wa magari matatu ya kawaida yaliyokuwa na namba za kiraia.

“Hakukuwa na king’ora chochote kama tulivyozoea bali ulikuwa ni msafara wa kimya kimya. Aliingia moja kwa moja kwenye zile ofisi na alitumia kati ya dakika 10 hadi 15 kabla ya kutoka,” alisema Mkamba.

Said Likoko alisema kuwa baada ya kugundua kati ya magari matatu alikuwepo Rais, walisogea kufuatilia kwa kina kwa kuwa haijazoeleka na walitegemea huenda baadhi ya watumishi wangewajibishwa.

“Aliteremka na kumuuliza aliyemkusudia na taarifa tulizozipata jana zinadai hakumkuta huyo bosi, sijui ni meneja au ofisa sisi hatujui,” alisema Likoko ambaye hujishughulisha pia na biashara ndogondogo eneo la kivukoni.

Likoko alisema pamoja na kwamba aliingia kimya kimya, Rais Magufuli hakusita kuwasalimia wasafiri waliokuwa wakisubiri kivuko wakati alipofanya ziara hiyo.

Alieleza kuwa kama wananchi walifurahishwa na hatua hiyo ya Rais, kwa kuwa watendaji wengi hawafanyi kazi siku za wikiendi licha ya huduma zake kufanyika siku zote.

Tangu jana asubuhi kumekuwa na video inayosambaa ikimuonyesha Rais Magufuli akiwa Kivukoni akitembea kwa miguu ndani ya eneo hilo huku akishangiliwa na wasafiri waliokuwa wakingoja kivuko.

Hata hivyo, jitihada za kutafuta mamlaka husika kueleza kwa undani malengo ya ziara hiyo ziligonga mwamba baada ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue kutopokea simu.

Ofisa habari wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) Theresia Mwami, alitaka utafutwe uongozi wa juu kueleza yaliyojiri kwenye ziara hiyo kwa kuwa yeye yupo likizo.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger