Majibizano kati ya Tundu Lissu na Spika Job Ndugai yamezidi kukua baada ya mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema), kuhoji maswali lukuki kuhusu taarifa za matatizo yake akijibu hoja kwamba hana kibali cha kuwa nje ya nchi.
Juzi, Lissu alitoa waraka alioupa jina la “Baada ya Risasi Kushindwa, Sasa Wanataka Kunivua Ubunge”, ukieleza tuhuma zake dhidi ya Serikali kuwa kuna mpango wa kumvua uwakilishi wake wa Singida Mashariki.
Lakini Spika Ndugai aliiambia Mwananchi juzi madai hayo ya Lissu ni “uzushi”, akieleza kuwa Lissu anapaswa kutambua “hana ruhusa ya Spika ya kuwa huko anakozurura”.
“Yeye ametoka kuugua aache uzushi, arudi nyumbani. Tunamsubiri nyumbani,” alisema Spika Ndugai juzi.
“Kitu muhimu ni kwamba ajue hana ruhusa ya Spika ya kuwa huko anakozurura. Sasa achunge kidogo, maana Spika ana nguvu zake, asimpe sababu.”
Ndugai alisema hawezi kumpangia Lissu mambo ya kusema ila ofisi yake haina taarifa.
Hata hivyo, Lissu, ambaye ni mnadhimu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, alikuwa na maswali mengi wakati alipozungumza na Mwananchi jana kuhusu majibu hayo ya Ndugai.
“Spika anajuaje kwamba nimepona? Anajua masharti niliyopewa na daktari ni yapi? Anajua nimetokaje hospitalini?” alihoji Lissu, ambaye alipelekwa Ubelgiji kumalizia matibabu ya majeraha aliyopata mwaka juzi baada ya kushambuliwa kwa risasi takriban 30 na watu wasiojulikana akiwa nje ya makazi yake, Area D mjini Dodoma.
“Spika hajui. Hajui kwa sababu yeye, tume ya utumishi wa Bunge au maofisa wa Bunge hawajaja kuniona tangu Septemba 7 mwaka juzi niliposhambuliwa.
“Spika Ndugai hajui chochote, hajui nimepona au sijapona. Hajui kwa sababu hajataka kujua, hajataka kunipigia simu kuniuliza kama ambavyo wengine wananipigia simu. Hajataka kuwasiliana na familia yangu, hajui kwa sababu ametaka kubaki asiyejua,” alisema Lissu.
Lissu, mmoja wa watu walioibukia kuwa wakosoaji wakubwa wa Serikali, alisema Spika amesikia tu kuwa yuko Uingereza lakini hajui yuko wapi.
“Ukimuuliza leo Lissu yupo wapi sidhani kama atakuwa na jibu. Hawezi kuwa na jibu kwa sababu yeye na watu wake hawataki kumjulia hali Lissu,” alisema.
Mwanasheria huyo alisema Spika aliwahi kusema kuwa angemtembelea wakati akiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya au sehemu yoyote ile, lakini mpaka jana hakuwa ametimiza ahadi hiyo.
Lissu pia alizungumzia hoja ya Ndugai kuwa hana kibali cha ofisi ya Spika.
“Hicho kibali kinatolewa katika mazingira gani? Nilishambuliwa mchana kabisa Dodoma na kusafirishwa nikiwa sijitambui. Sasa ni muda gani nilipaswa kuomba kibali?” alihoji.
Alisema suala hilo la kusafirishwa kwenda Nairobi kwa matibabu liliamuliwa katika kikao kilichofanyika Dodoma kilichomuhusisha Ndugai, Dk Tulia Ackson (Naibu Spika), Dk Thomas Kashililah (katibu wa Bunge wa wakati huo, Freeman Mbowe (Mwenyekiti Chadema), Ummy Mwalimu (Waziri wa Afya) na Dk Mwigulu Nchemba (aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani).
“Mimi nikiwa sijitambui, napigania roho yangu,” alisema Lissu ambaye alisema taarifa za kikao hicho alipewa baadaye.
“Katika kikao kile iliamuliwa mimi nipelekwe Hospitali ya Nairobi na nikasindikizwa na daktari wa Dodoma na ndege ikaruhusiwa kuruka saa 6:00 usiku. Sasa hicho kibali ninachoambiwa na Spika Ndugai ni kipi?
“Yeye alikuwepo, aliniona, hicho kibali anachokisema ni kipi? Mtu aliyejeruhiwa vile anaweza kuomba kibali? Au kuniona Uingereza ndio nimepona?”
“Hawajaja kuniona ndio maana wanasema nimepona. Wangekuja kuniona wangejua hicho wanachokisema kina ukweli kiasi gani. Wangejua nimepona au bado, sasa wanabaki kusema nimepona bila kuja kuniona?”
Via Mwananchi
0 comments:
Post a Comment