Monday, 21 January 2019

CAG Kikaangoni Leo....Atua Dodoma Tayari Kwa Kuhojiwa na Kamati ya Bunge

...
LEO  macho na masikio ya Watanzania yatakuwa Jijini Dodoma ili kujua nini kitajiri katika mahojiano ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad  na Kamati ya Maadili ya Bunge.
 
Assad anafika mbele ya Kamati hiyo ya Bunge kutokana na wito uliotolewa na Spika wa Bunge Job Ndugai  January 7, mwaka huu kumtaka afike mwenyewe leo January 21 la sivyo Bunge linaweza kumfikisha mbele ya Kamati hiyo kwa pingu kuonesha kuwa wao sio dhaifu kama inavyodaiwa.
 
Aidha, mbali na CAG lakini pia Mbunge wa Kawe Halima Mdee (CHADEMA) naye ametakiwa kufika mbele ya Kamati hiyo kesho ili kuhojiwa pia kutokana na kile kilichodaiwa kuwa alinukuu maneno ya CAG. 

Chimbuko la sakata hilo ni mahojiano ya hivi karibuni wakati mkaguzi huo wa Hesabu za Serikali, alipokuwa akihojiwa na Mwandishi wa habari wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa na Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa (UN), Arnold Kayanda.
 
Kayanda alimuuliza CAG kuwa Ofisi yake imekuwa ikijitahidi kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonyesha kuna ubadhirifu lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea.
 
CAG alijibu:”Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.


“Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafi kiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.”
 
“Sitaki kuwa labda nasema hili kwa sababu linahusisha watu fulani, lakini ninachotaka kusema ni kuwa Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata huu udhaifu unaoonekana utapungua.”alisema
 
Kauli hiyo ndiyo iliyomuibua Spika Ndugai na kumtaka CAG Assad kufika mbele ya Kamati ya Maadili ya Bunge ili ahojiwe kuhusu kauli hiyo ambapo Spika alidai imelidhalilisha Bunge lake.
 
Hatua ya Bunge kumwita Profesa Assad kumhoji, iliibua mjadala mkubwa kwa madai kuwa Spika hana mamlaka ya kumwita CAG na kutaka ahojiwe. 

Mvutano huo ndio uliomfanya Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) aandike barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) Ma-CAG na Maspika wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), akiwataka waingilie kati sakata la Spika Ndugai na CAG Assad.
 
Zitto pia aliamua kufungua kesi mahakamani akishirikiana na wabunge wenzake wanne, wakiomba tafsiri ya Mahakama juu ya mamlaka ya Spika kwa CAG.
 
Hata hivyo, mwishoni mwa wiki iliyopita CAG Prof Assad alivunja ukimya kwa kusema kwamba yuko tayari kwenda kuhojiwa na Kamati ya Bunge kuitikia wito wa Spika.
 
Profesa Assad pia alisema neno ‘Udhaifu’ alililolitumia kulieleza Bunge, ni lugha ya kawaida sana katika taaluma yao ya ukaguzi.

“Ni wazi kuwa watu wengine wanaweza kuchukua tafsiri tofauti ya maneno kama haya. Yametokea malumbano makali na marefu katika nyanja zote za mawasiliano kuhusu rai, nafasi na maamuzi mbalimbali yaliyochukuliwa na viongozi.
 
“Januari 15, nilipokea wito wa kisheria ulionitaka kutokea mbele ya kamati ya Bunge tarehe 21 Januari mwaka huu, kwa mantiki ya kudumisha mahusiano mazuri kati ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali na Bunge, ninayo
nia ya kuitikia wito huo hapo tarehe 21” alisema.
 
Pia wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) walikaa kwenye Kamati ya Wabunge wa CCM(Caucus) kulijadili jambo hilo na kwa umoja wao walimpongeza Spika Ndugai kwa uamuzi huo huku wakidai kwamba Zitto anataka kuigawa nchi.


from MPEKUZI http://bit.ly/2CybhRn
via Malunde
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger