Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Aliyekuwa Mbunge wa Tarime Mjini na Mtia Nia wa nafasi hiyo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2025 Michael Kembaki, ameonyesha ukomavu wa kisiasa na uzalendo kwa chama chake kwa kukubali maamuzi ya vikao vya CCM vilivyopitisha jina la Ester Matiko kuwa mgombea wa jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Kembaki ambaye aliibuka mshindi wa kwanza kwenye kura za maoni kwa kupata kura 1,572, amethibitisha kuwa si kila ushindi unaolengwa ni wa sanduku la kura, bali kuna ushindi mkubwa wa kusimamia misingi ya chama na kuvunja makundi kwa ajili ya mshikamano.
Mbunge huyo wa Tarime anayemaliza muda wake ameeleza hayo leo Agosti 25,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo ameeleza, “Nawashukuru sana wananchi wa Tarime kwa kuniamini na kunipa kura zenu,lakini kama mnavyojua, utaratibu wa chama chetu hauishii kwenye kura za maoni pekee bali Mgombea hupatikana kupitia mchakato wa kina wa vikao halali vya chama,” amesema
Kembaki pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa imani na nafasi aliyopewa kulitumikia Taifa kama Mbunge kwa miaka mitano na kueleza kuwa ametambua kuwa uongozi si kiti cha kudumu, bali ni fursa ya kupokezana kwa wakati sahihi.
“Mwaka 2020 nilikuwa wa pili kwenye kura za maoni lakini nikaaminiwa kupeperusha bendera ya chama,leo, pamoja na kuongoza kura za maoni, sikuteuliwa lakini nimepokea maamuzi ya chama kwa mikono miwili,” amesema kwa utulivu.
Kembaki ametumia nafasi hiyo kuwatoa hofu wafuasi wake akisisitiza kuwa CCM haina upendeleo kama inavyoaminika na baadhi ya watu, bali ina utaratibu wake madhubuti wa kufanya maamuzi kwa kuzingatia vigezo vyenye mashiko.
“Mwaka 2020 nilipata kura 64 tu, mpinzani wangu alipata zaidi ya 200 – lakini chama kilinichagua. Leo nimeongoza kura, lakini chama kimempitisha mwingine hii ni ishara kuwa CCM haijengwi kwa hisia, bali kwa vigezo na utaratibu,” ameeleza.
Katika ujumbe wake kwa wanachama na mashabiki, Kembaki amesisitiza kwamba huu si wakati wa lawama wala migawanyiko badala yake, amewataka kuvunja makundi yote, kusimama pamoja na kuhakikisha ushindi wa chama kwa kuhamasisha wananchi kumchagua mgombea aliyeteuliwa.
“Sitabomoa nyumba niliyoijenga. Nitaendelea kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo. Huu si wakati wa hisia binafsi – huu ni wakati wa CCM. Mgombea tayari amepatikana; sasa kazi yetu ni moja tu – kumnadi na kuhakikisha chama kinashinda kwa kishindo,” alisema kwa msisitizo.
Akiangazia hali ya maendeleo wilayani Tarime, Kembaki amesema kuwa ahadi nyingi zilizotolewa na serikali ya awamu ya sita tayari zimetekelezwa kwa kiwango cha asilimia 85, huku akibainisha kuwa fedha nyingi zimepelekwa mkoani humo kwa ridhaa ya Rais Samia.
“Hii ni sababu ya msingi ya kuhakikisha serikali inaendelea kuaminiwa. Wanachama na wananchi wa Tarime tuendelee kuiunga mkono serikali na chama – kwa sababu miradi tuliyoahidi tumetekeleza, na mengine bado yanaendelea,” alisema.
Kembaki ametuma ujumbe mzito kwa wale wote wanaohisi kuumizwa na mchakato wa ndani ya chama.
Ametoa mfano wake kama ushahidi kuwa demokrasia ndani ya CCM ipo, na kwamba nafasi ya uongozi ni fursa ya muda, si haki ya kudumu.
“Uhai wa CCM ndio unaosababisha watu kulalamika lakini hiyo ndiyo dalili kuwa chama hiki kipo hai na kinafuata taratibu zake,Mimi nitaendelea kuwa mwanachama mtiifu na mwenye kuisapoti CCM kwa moyo wote,” amesema Kembaki.

0 comments:
Post a Comment