Friday, 29 August 2025

NABII RABIEL KUFANYA MAOMBI YA TAIFA

...

 


Nabii Rabiel Akyoo wa Kanisa la Ukombozi akiongea na waandishi wa habari 


Na Woinde Shizza Arusha Arusha

Nabii Rabiel Akyoo wa Kanisa la Ukombozi anatarajiwa kuongoza maombi ya kitaifa kesho jijini Arusha kwa lengo la kuliombea taifa kudumisha amani na mshikamano wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.


Akizungumza na waandishi wa habari Nabii Akyoo alisema maombi hayo yatakusanya waumini kutoka maeneo mbalimbali nchini na yatakuwa na ajenda kuu ya kuombea utulivu na mshikikano wa taifa.


“Ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda amani Ikitoweka, hakuna kazi, hakuna kipato, na maisha yatakuwa magumu kwa kila mmoja wetu,” alisema.


Sambamba na maombi hayo, kutafanyika harambee ya kuchangia kituo kipya cha habari cha kanisa hicho, kitakachojumuisha televisheni na redio, huku sera yake ikizinduliwa rasmi.


Katika siku hiyo pia kutakuwa na burudani ya nyimbo za injili kutoka kwa waimbaji mbalimbali maarufu akiwemo Upendo Nkone, anayetarajiwa kupamba maombi kwa nyimbo zake za kumsifu Mungu.


Waumini na wananchi wataungana kushiriki ibada ya Meza ya Bwana, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mshikamano wa kiroho na taifa kwa ujumla.


Nabii Akyoo aliwaasa Watanzania kujitokeza siku ya kupiga kura kwa amani na utulivu, akisisitiza kuwa kura ni sauti ya kila raia, lakini amani ya taifa ni urithi wa kudumu.


“Kura yako ni sauti yako, lakini zaidi ya yote, amani ya taifa letu ndiyo urithi mkubwa tunaopaswa kuudumisha,” alisema Nabii huyo.


Maombi hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na waumini wa madhehebu mbalimbali, viongozi wa dini na wananchi kutoka mikoa tofauti, huku Arusha ikitarajiwa kuwa kitovu cha ibada kubwa ya taifa

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger