Saturday, 30 August 2025

CHUO KIKUU HURIA NA JESHI LA POLISI RUVUMA WATOA MSAADA KITUO CHA WATOTO YATIMA CHIPOLE

...


Na Regina Ndumbaro, Songea – Ruvuma

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma kimetoa msaada kwa Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Chipole kilichopo Kata ya Magagura, Halmashauri ya Songea Vijijini. Msaada huo ulihusisha fedha taslimu shilingi milioni moja na laki mbili (1,200,000) pamoja na mahitaji muhimu kama vyakula, nguo na bidhaa nyingine za matumizi ya kila siku.

Akizungumza wakati wa makabidhiano, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu Huria, Vincent Mpepo, alisema kuwa waliguswa na hali ya watoto hao baada ya kuona picha na video zilizosambazwa na Inspekta Dominic Msangi, Polisi Kata wa Magagura, ambazo zilionesha mazingira ya kituo hicho na kuhamasisha wadau kujitokeza kusaidia.

Mpepo ameeleza kuwa msaada huo ni mwanzo wa safari ya ushirikiano kati ya chuo hicho na kituo hicho, na kuahidi kuwa wataendelea kujitokeza kadri watakavyoweza ili kusaidia watoto hao kupata maisha bora.

 Pia amesema wana mpango wa kufadhili bima za afya kwa watoto 50, jambo litakalosaidia sana katika kukabiliana na changamoto za matibabu.

Kwa upande wake, Inspekta Msangi alieleza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa mkakati wa Kamishna wa Polisi Jamii wa kushirikiana na wadau kusaidia jamii, hasa makundi maalum kama watoto yatima, kwa lengo la kuimarisha mshikamano na huruma miongoni mwa Watanzania.

Akizungumza kwa niaba ya kituo, Mtawa Maria Akwinata kutoka Shirika la Watawa wa Chipole alishukuru kwa msaada huo na kueleza kuwa kituo hicho kinalea watoto wa rika mbalimbali kuanzia wanaozaliwa hadi kufikia elimu ya sekondari, hivyo mahitaji yao ni makubwa na yanahitaji msaada wa mara kwa mara kutoka kwa jamii.

Mmoja wa watoto wa kituo hicho, Richard Haule, ameeleza kufarijika kwao kwa kutembelewa na kusaidiwa, akisema kuwa msaada huo umeonyesha kuwa bado wanakumbukwa na jamii.

 Ametoa wito kwa taasisi na watu binafsi kuendelea kujitokeza kusaidia ili kuwajengea watoto hao matumaini na mustakabali mzuri wa maisha.





Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger