Wednesday, 27 August 2025

DKT. SAMIA AREJESHA FOMU YA URAIS INEC

...


Na Dotto Kwilasa,Dodoma

MGOMBEA wa urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Agosti 27, 2027, amerejesha rasmi fomu ya kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), zilizopo Njedengwa, jijini Dodoma.

Dkt. Samia, ambaye pia ni Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliwasili katika ofisi hizo saa 1:50 asubuhi akiwa ameongozana na mgombea mwenza wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi, pamoja na viongozi waandamizi wa CCM wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Alhaj Adamu Kimbisa.

Mara baada ya kuwasili, msafara wa Dkt. Samia ulipokelewa rasmi na Mkurugenzi wa INEC, Kailima Ramadhan, kabla ya kuelekea ofisini kwa ajili ya zoezi la urejeshaji wa fomu – hatua muhimu inayowezesha kuendelea kwake katika mchakato wa kugombea nafasi ya juu kabisa ya uongozi wa taifa.

Dkt. Samia alichukua fomu ya kugombea Urais mapema Agosti 9, 2027, na leo amerejesha rasmi ikiwa ni ishara ya kuhitimisha hatua muhimu katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Mbali na CCM, vyama vingine 17 vimeshachukua fomu za kuwania nafasi hiyo ya juu serikalini. Miongoni mwa vyama hivyo ni pamoja na ACT-Wazalendo, CUF, NCCR-Mageuzi, UDP, ADC, TLP, na vyama vingine kama NRA, UMD, CHAUUMA, AAFP, Chama Makini, NLD, UPDP, ADA-TADEA, CCK, DP na SAU.

Urejeshaji huu wa fomu unafungua ukurasa mpya kuelekea kuanza kwa kampeni rasmi, huku Watanzania wakisubiri kwa hamu kuona namna wagombea watawasilisha hoja na dira zao za kuiongoza Tanzania katika kipindi kijacho.



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger