Na Dosca Kusenha, Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amelielekeza Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) kuongeza nguvu ya utoaji elimu na kusogeza huduma karibu zaidi kwa watumiaji ili kuboresha uelewa wa haki na wajibu wao kuhusu huduma za mafuta, gesi, umeme na maji.
Akizungumza leo Agosti 5, 2025 baada ya kutembelea banda la EWURA CCC katika Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Senyamule amesema wananchi wengi wa pembezoni hukosa taarifa muhimu za namna ya kushughulikia changamoto na malalamiko kuhusu huduma za nishati na maji, jambo linalozuia maendeleo yao ya kiuchumi.
"Ili kuongeza uelewa wa haki na wajibu wao katika matumizi ya huduma za mafuta, gesi, umeme na maji, ni lazima wananchi wapate elimu endelevu itakayowawezesha kufahamu taratibu za kudai huduma bora, " amesema
Licha ya hayo Senyamule ameipongeza EWURA CCC kwa hatua yake ya kutumia maonesho ya Nanenane kutoa elimu ya moja kwa moja kwa wananchi na kueleza kuwa ni njia bora ya kuwajengea uwezo wa kutambua haki na wajibu wao.
Amesisitiza kuwa elimu hiyo itasaidia wakulima kupunguza gharama za uzalishaji kupitia matumizi sahihi na endelevu ya nishati na maji.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma amesisitiza umuhimu wa EWURA CCC kuongeza kasi ya kutoa elimu kuhusu utaratibu sahihi wa kushughulikia na kuwasilisha malalamiko, ili watumiaji wawe na uelewa mpana na waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kilimo na biashara kwa tija na ufanisi zaidi.
Aidha Senyamule ameshauri EWURA CCC kuendelea kutumia majukwaa ya maonesho kama Nanenane sio tu kwa kutoa elimu, bali pia kukusanya maoni na changamoto za wananchi ili kusaidia Serikali kuboresha sera na mikakati ya kudhibiti huduma hizo.
Amesema ;“Tukiwaelimisha wananchi namna bora ya kutumia huduma za nishati na maji, tutakuwa tunawawezesha kuongeza tija katika kilimo na uzalishaji, "ameeleza
Kwa upande wake Afisa Uelimishaji na Uhamasishaji wa EWURA CCC, Lugiko L. Lugiko, ameeleza kuwa ushiriki wa Baraza hilo katika maonesho ya mwaka huu ni sehemu ya mkakati wa kusogeza huduma kwa wananchi na kuwaelimisha kuhusu haki zao na taratibu sahihi za kushughulikia changamoto wanazokutana nazo.
Lugiko amesema kupitia maonesho hayo, EWURA CCC inatoa mafunzo ya moja kwa moja kwa wakulima na wananchi kwa ujumla kuhusu namna ya kutambua bei halali za mafuta, kushughulikia bili zisizoeleweka na kushirikiana na watoa huduma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Aidha, Lugiko amebainisha kuwa banda la EWURA CCC limekuwa likitoa elimu kwa vikundi vya wanawake, vijana na wakulima wadogo,kuhusu namna huduma bora za nishati na maji zinavyoweza kuongeza thamani ya mazao .
Kutokana na hayo baadhi ya Wananchi waliotembelea banda hilo wamepongeza jitihada hizo, akiwemo Lucy Joseph mkulima kutoka Singida ambaye amesema: “Kupitia EWURA CCC tunajua sasa njia sahihi ya kushughulikia changamoto za maji na umeme ,mwanzoni hatukijua namna ya kutatua kero zetu.”
EWURA CCC imeahidi kuendeleza ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuhakikisha elimu na ushawishi wa watumiaji wa huduma za nishati na maji unawafikia Watanzania wote, hatua inayotarajiwa kuchochea uwajibikaji na uboreshaji wa huduma kwa manufaa ya taifa.






0 comments:
Post a Comment