Na Barnabas Kisengi, Dodoma
Shangwe, nderemo na vifijo vilitawala leo katika ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kilimani Jijini Dodoma baada ya Mgombea wa nafasi ya Udiwani kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Mussa Mkunda, kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Wanachama wa CCM, wananchi pamoja na viongozi wa chama walijitokeza kwa wingi kumsindikiza Mhe. Mkunda katika hatua hiyo muhimu ya kisiasa. Tukio hilo limeonyesha mshikamano mkubwa wa wana CCM wa kata hiyo, ishara ya umoja kuelekea ushindi wa chama hicho katika uchaguzi ujao.
Akizungumza katika ofisi ya Mtendaji wa Kata mara baada ya Mgombea kuchukua fomu, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kilimani, Comrade Nathan Chibeye, alisema kuwa chama hicho kina utaratibu wa kidemokrasia wa kupitia mchakato wa ndani na kuteua mgombea mmoja wa nafasi ya Udiwani, ambaye sasa ni Mhe. Mussa Mkunda.
“Sisi kama chama, tukimaliza uchaguzi wa ndani, tunavunja makundi yote yaliyokuwepo na sasa tunakuwa kitu kimoja – chama kimoja na kundi moja la wana CCM – kwa lengo la kuhakikisha wagombea wetu walioteuliwa wanashinda kwa kishindo kwenye uchaguzi mkuu,” alieleza Chibeye.

Akikabidhi fomu za kugombea kwa Mhe. Mkunda, Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata ya Kilimani, Bi. Neema Simanjilo, alimwelekeza kuzisoma kwa umakini na kuzijaza kikamilifu kama inavyoelekezwa kabla ya kuzirejesha kwa wakati.
Baada ya kupokea fomu, Mhe. Mussa Mkunda alitoa shukrani kwa chama chake kwa imani waliyoionyesha kwake, pamoja na Tume Huru ya Uchaguzi kwa kurahisisha mchakato wa kuchukua fomu hiyo.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu, chama changu, pamoja na wana Kilimani wote kwa kuniunga mkono. Nashukuru tume kwa ufanisi wa mchakato huu – hakuna changamoto yoyote nimekutana nayo,” alisema Mkunda.
Akiwahutubia wananchi na wanachama waliomsindikiza, Mkunda aliwaahidi kuendeleza miradi yote iliyoanzishwa na aliyekuwa Diwani mstaafu na kuhakikisha inakamilika kwa wakati. Alitaja mfano wa shule yenye vyumba vinne vya madarasa ambavyo bado havijakamilika – akiahidi kuvimalizia na kuongeza miundombinu mingine ya elimu.
Mkunda alitaja vipaumbele vyake ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara, hasa katika Mtaa wa Chinyoyo,kujenga kituo cha afya, shule ya sekondari, kituo cha polisi, na ofisi za viongozi wa serikali za mitaa yote minne.
Vipaumbele vingine ni kuanzisha soko la kisasa la kata ya Kilimani,kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kusimamia na kuhamasisha shughuli za maendeleo kwa ushirikiano na wananchi wote wa kata hiyo.
Amehitimisha kwa kuahidi kuwa uongozi wake utakuwa wa ushirikiano, uwazi na kushirikisha wananchi wote bila ubaguzi, ili kwa pamoja kuijenga Kilimani mpya yenye maendeleo endelevu.



0 comments:
Post a Comment