Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Martin Griffiths amelikaribisha pendekezo la waasi wa Houthi la kusitisha mashambulizi yote dhidi ya Saudi Arabia akisema hatua hiyo inaweza kumaliza miaka kadhaa ya umwagaji damu nchini Yemen.
Griffiths amesema utekelezaji wa pendekezo hilo la waasi wa Houthi litatuma ujumbe wa wazi wa nia ya kukomesha vita na kusifu matamanio ya kutumia njia za kisiasa kumaliza mzozo huo hatari.
Mnamo Ijumaa iliyopita, waasi wa Houthi walitoa pendekezo hilo kama sehemu ya juhudi za kusaka amani, lakini Saudi Arabia imesema itasubiri kuona iwapo waasi hao watatekeleza kwa vitendo kile walichosema.
Pendekezo la waasi wa Houthi linafuatia mfululizo wa mashambulizi ya kutumia ndege zisizo na rubani katika miundombinu ya mafuta ya Saudi Arabia ambayo yalivuruga karibu nusu ya uzalishaji wa nishati hiyo muhimu na kutikisa soko la mafuta duniani.
0 comments:
Post a Comment