Sunday, 22 September 2019

Iran yataka vikosi vya kigeni viondoke Ghuba ya Uajemi

...
Rais wa Iran amesema siku ya Jumapili kuwa nchi yake ndiyo inastahili kuongoza usalama wa kikanda katika Ghuba ya Uajemi na kuonya kuhusu kuwepo kwa majeshi ya kigeni katika eneo hilo.

Haya yanakuja wakati ambapo mkataba wa nyuklia wa nchi hiyo na nchi zenye nguvu duniani unasambaratika na Marekani imetuma vikosi zaidi kwa ajili ya kuongeza usalama kwa washirika wake wa Kiarabu.

Akizungumza wakati wa gwaride la kijeshi, Rais Hassan Rouhani amesema kwamba uwepo wa majeshi ya kigeni katika Ghuba huenda ukasababisha matatizo kwa usalama wa nishati duniani.

Amesema Iran inaunyoosha "mkono wa urafiki na udugu" kwa mataifa mengine ya kanda hiyo kwa kusimamia usalama katika Ghuba ya Uajemi na njia ya bahari ya Hormuz ambapo asilimia ishirini ya mafuta yanayouzwa nchi za nje yanapitia.
 
Pamoja na kuongeza idadi ya wanajeshi na vifaa vya kijeshi kwa Saudi Arabia na nchi za Umoja wa Kiarabu, Marekani inaongoza muungano wa kijeshi wa majini ambao unaojumuisha nchi za Umoja wa Kiarabu, Saudi Arabia, Bahrain, Uingereza na Australia ili kuimarisha usalama wa njia za majini za eneo hilo na njia zengine muhimu za biashara ya mafuta.
 
Kwa muda mrefu Iran imetaka kuondolewa kwa vikosi vya majeshi ya nchi za Magharibi na Marekani kutoka nchi za Kiarabu zilizo katika eneo la Ghuba kwa kuwa inaona hatua hiyo kama kitisho kinachoikodolea macho nchi hiyo.

Rais Hassan Rouhani anatarajiwa kusafiri kuelekea mjini New York hapo Jumatatu, siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Rouhani amesema kuwa atatoa mpango wa amani wa kanda hiyo katika Baraza hilo la Umoja wa Mataifa wakati ambapo wasiwasi unaongezeka kati ya Iran na Marekani kufuatia kusambaratika kwa mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Javad Zarif ambaye amewekewa vikwazo na Marekani, tayari amewasili New York kuelekea mkusanyiko huo wa viongozi wa dunia unaofanyika kila mwaka.


Share:

Related Posts:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © 2025 MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger