Wednesday 29 May 2019

Waziri Ummy Aipa Kipaumbele Hedhi Salama

...
 Na.WAMJW-Dodoma
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameahidi kuweka masuala ya hedhi salama kwenye Sera mpya ya Afya ambayo iko mbioni kukamilika ili kuona kama hedhi salama imewekwa kama kipaumbele.

Ameyasema hayo jana jijini Dodoma wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Hedhi Salama Duniani ambayo kitaifa yamefanyika jijini hapa.

Waziri Ummy amesema masuala ya hedhi salama katika jamii hususan watoto wasichana na wanawake ni muhimu katika kuweka hali ya usafi wa mazingira rafiki ambapo katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania inakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama, vyoo bora hasa mashuleni na sehemu za kazi vyenye chumba cha kubadilishia wakati wa hedhi.

“Katika ripoti za UNICEF na WHO ya mwaka 2013 zinasema kuwa katika kila msichana mmoja kati ya kumi kusini mwa jangwa la sahara anakosa kwenda shule kwa siku tatu hadi tano kwa sababu ya kuwa kwenye siku za hedhi”,Alisema Waziri Ummy.

Hata hivyo alisema asilimia 52 ya vyoo vya wasichana mashuleni havina milango na ni asilimia 1 tu ya shule zimetenga chumba maalum kwa ajili ya wasichana kujisitiri wakiwa kwenye hedhi kikiwa na maji na vifaa vya hedhi.

Aidha, aliwataka wadau kuweka mkazo kwenye kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara kuzingatia upunguzaji wa bei kwani taulo za hedhi si bidhaa ya anasa ila ni bidhaa muhimu kwa mstakabali wa afya na maendeleo ya wanawake na wasichana nchini.

Waziri Ummy ametoa rai kwa wadau wote wa hedhi salama kutenga fedha kwa ajili ya kujenga walau choo kimoja cha mfano katika halmashauri kwani jamii ipo tayari kuchangia maendeleo. Aidha, amekusudia kila taulo za kike zikatazoingizwa au kuzalishwa Tanzania ziwe na idadi maalumu za katika kila paketi angalau taulo kumi.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger