Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Group, Mohammed Kiluwa akitiliana saini na Rais wa kampuni ya Kiisu Minyuan International Trading Ltd, Yu Liang kuhusu mkataba wa makubaliano ya uwekezaji wa kujenga kiwanda cha sukari na kilimo. Makubaliano hayo yamefanyika leo katika ofisi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Group, Mohammed Kiluwa akipeana mkono mara baada ya kutiliana saini na Rais wa kampuni ya Kiisu Minyuan International Trading Ltd, Yu Liang kuhusu mkataba wa makubaliano ya uwekezaji wa kujenga kiwanda cha sukari na kilimo. Makubaliano hayo yaliyoshuhudiwa na Mkurugenzi Idara ya Uhamasishaji TIC John Mathew kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Geoffrey Mwambe, yamefanyika leo katika ofisi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya mashahidi Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Group Naima Kiluwa na Mwakilishi wa kampuni ya Kiisu Minyuan International Trading Ltd, wakitia saini makubaliano kama sehemu ya Mashahidi wa tukio hilo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Group, Mohammed Kiluwa akizungumza jambo mbele ya Wageni waalikwa mbalimbali wakiwemo wawekezaji kutoka nchini China,mara baada ya kutiliana saini kuhusu mkataba wa makubaliano ya uwekezaji wa kujenga kiwanda cha sukari na kilimo.
Mkurugenzi Idara ya Uhamasishaji TIC John Mathew kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Geoffrey Mwambe, (wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Wawekezaji wa nchini Tanzania na China mara baada ya kumaliza kusaini makubaliano yao,leo katika ofisi hizo jijini Dar
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Group, Mohammed Kiluwa akipeana mikono na Wabia wake mara baada ya kusaini makubaliano yao leo jijini Dar
***
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimewakaribisha Watanzania wazalendo kutembelea katika ofisi za kituo hicho kwa lengo la kujua taarifa mbalimbali na fursa za uwekezaji zilizopo kwenye maeneo tofauti.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Idara ya Uhamasishaji TIC John Mathew kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Geoffrey Mwambe katika hafla ya kutia saini mikataba ya makubaliano ya uwekezaji kati ya kampuni za Tanzania na China ambapo amesema huu ndio wakati wa vijana kuwa karibu na kituo hicho ili kupata taarifa za kila siku juu ya uwezekaji.
Amefafanua kuwa Kampuni ya Kiluwa Group inafanya kazi kubwa ya kuzungumza na wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali hasa China ambapo leo wanashuhudia utiwaji saini mkataba wa mwakubaliano ili kuanzisha kiwanda cha sukari nchini.
"Wachina hawa baada ya kuvutiwa na mikataba hii watavutia wawekezaji wengine ndani na nje ya nchi, Kampuni ya Kiisu Minyuan International Trading Ltd inataka kuwekeza katika kiwanda cha kutengeneza sukari, hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya uzalishaji wa bidhaa hii muhimu kwa maendeleo ya nchi,,"amesema Mathew.
Ameongeza wadau wengine wajitokeze ili wasaidiwe namna bora ya kuunganisha kampuni kutoka nje na kampuni za ndani ili kuhakikisha kunapatikana urahisi katika baadhi ya masuala.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kiluwa Group, Mohammed Kiluwa amesema mara nyingi anapokuwa katika mikutano ya kimataifa inayohusu uwekezaji amekuwa akijitahidi kuhakikisha anavuta wawekezaji wakubwa kuja kuwekeza nyumbani Tanzania.
"Hivi karibuni nilikuwa katika mkutano wa One Belt One Road, nikauza fursa za uwekezaji, wengi walipenda na baadhi yao ni hawa tuliotiliana nao saini. Sisi ndio wajenga nchi na hasa katika kipindi hiki ambapo Rais Dk. John Magufuli ameamua kwa dhati kuifanya nchi kuwa na uchumi wa kati kwa kutegemea viwanda.
"Hivyo, viwanda vingi iwezekanavyo vinahitajika. Kwa mfano kwa uwekezaji huu sisi tutahitaji eneo lenye ukubwa wa hekta 30,000 na hili si eneo moja bali tutaweza kuwa na uwekezaji katika mikoa mbalimbali.
"Kama mnavyofahamu kiwanda cha sukari uzalishaji wake una mambo mengi, muwa unapoingizwa kiwandani unakuwa na vitu vingi hivyo tutakuwa na Industrial Park za kutosha,"amesema Kiluwa.
Pia amewataka Watanzania kushirikiana katika kutangaza fursa zilizokuwepo nchini kwenye uwekezaji, anadai anajiona yuko peke yake wengi hawachangamkia nafasi za kutangaza maeneo ya nchi kwenye uanzishwaji viwanda kwa faida ya taifa.
Wakati huo huo Rais wa kampuni ya Kiisu Minyuan International Trading Ltd, Yu Liang amesema amevutiwa na namna Tanzania inavyothamini wageni hasa wawekezaji. Anaamini watakuwa na muda mzuri wakiwa nchini kwenye shughuli za kukuza uchumi wa Afrika na China.
"Undugu kati ya China na Tanzania ni wa kupigiwa mfano, tumezunguka maeneo mengi ambayo bwana Kiluwa alitueleza tukiwa China na sasa tumeamini hakika Tanzania inayo nafasi kubwa ya kukua katika sekta ya viwanda,,"amesema Liang.
0 comments:
Post a Comment