Friday, 31 May 2019

NAMNA WAKULIMA WANAVYOPOTEZA FURSA KWA KUTOKUCHANGAMKIA FURSA

...

Kaimu Mkurugenzi Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele, Dk Fortunatus Kapinga akionyesha maziwa yanayotegenezwa kwa kutumia korosho.
Kaimu Mkurugenzi Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele, Dk Fortunatus Kapinga akionyesha maziwa yanayotegenezwa kwa kutumia korosho.
Mtafiti kutoka kituo cha utafiti wa kilimo Tari- Naliendele, Regina Msoka akinyesha bidhaa zinazotengenezwa kwa kutumia mabibo ya korosho, juisi kusho na kulia ni mvinyo.
Mtafiti kutoka kituo cha utafiti wa kilimo Tari- Naliendele, Regina Msoka akinyesha bidhaa zinazotengenezwa kwa kutumia mabibo ya korosho, juisi kusho na kulia ni mvinyo.
Chupa zenye mvinyo ulio tayari kwa ajili ya kwenda sokoni.

Chupa zenye maziwa yanayotengenezwa kwa kutumia korosho.
****
Mara nyingi wakulima wa korosho hulima zao hilo kwa lengo la kuuza korosho ghafi ambazo kwa kiasi kikubwa husafirishwa kwenda nje nchi na baadhi yao wachache huzibangua ili kuziongezea thamani.
Lakini bado wamekuwa wakipoteza mapato kwa kiasi kikubwa kutokana na kutotumia vyema fursa inayopatikana kwenye korosho.
Kutokana na utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele katika zao hilo mkulima anaweza kuzalisha bidhaa nyingine kwa mbali na ile korosho anayoiuza ikiwa ghafi.
Katika zao hilo kuna tunda la bibo ambalo wakati wa mavuno mkulima hulazimika kutenganisha bibo na korosho ndipo apeleke korosho ghalani. Wakulima wengi huyateketeza kwa moto licha ya kuwa yanafaa kuzalisha bidhaa kama mvinyo, jam na juise’
Mtaalamu kutoka kituo cha utafiti wa kilimo Tari- Naliendele, Regina Msoka anasema mkulima anapopata kilo moja ya korosho ghafi shambani anaacha mabibo kilo tisa huku akiambulia kati ya Sh 2,400 hadi 4,000 kulingana na bei ya mnada.
“Mkulima akipata kilo moja ya korosho  ghafi maana yake ameacha kilo tisa za mabibo shambani unaweza kuona ni jinsi gani anaacha bidhaa ambayo ni muhimu shambani,”anasema Msoka
Anabainisha katika katika kilo tisa ya mabibo yakisindikwa na kutengenezea mvinyo na kuuthaminisha ana uwezo wa kupata Sh 100,000 huku kilo moja pekee ya korosho hazidi Sh 4,000.
“Ukipiga hesabu za haraka katika kilo kumi za korosho ana mabibo kilo 90 maana yake ana Sh 40,000 ya korosho na ambaye anatumia mabibo kutengeneza mvinyo ana Sh 1milioni kwa hiyo hapo unaona ni faida gani iliyopo kwenye mabibo,”anasema Msoka na kuongeza;
“Tumefanya utafiti teknolojia zipo tuna uwezo wa kutengeneza juisi ya mabibo ambayo haina ukakasi, ambapo katika mabibo kilo moja unapata nusu lita ya juisi,wengi wanakimbia bibo sababu ya ule ukakasi wake,sisi tumefanikiwa kuutoa na pia tunapata juisi nzuri, tunapata jam na pia mashine zinapatikana Sido na tunaendelea kutoa mafunzo kwa badhi ya wakulima,”anasema
Kutokana na bibo kutohifadhika kirahisi anasema baadhi ya wakulima huyakausha na kutenegenezea pombe za kienyeji maarufu kama ulaka ambazo hazijathibitishwa kwani kiutaalamu.Anasema kitaalamu yanapaswa kutunzwa sehemu yenye ubaridi (cold room).
Muda wa kupata mvinyo, jam na juisi
Ili kupata mvinyo uliokamilika inahitajika miezi mitatu ili kuyasindika mabibo ili ukomae ambapo kilo moja ya mabibo una uwezo wa kuzalisha lita moja ya mvinyo.
Ili kupata juisi zinahitajika siku mbili ambapo mtengenezaji anahitaji mabibo kilo moja ili kupata nusu lita ya juisi na kwa jam ni siku moja.
Utengenezaji  siagi ya korosho na maziwa
Mtafiti Msoka anasema kwa kutumia  kilo moja ya daraja la mwisho ambalo ni vipande vidogo vya korosho (small pieces WW450) baada ya kubanguliwa na kupangwa katika madaraja unaweza kutengeneza siagi kilo moja ambayo huuzwa Sh 20,000 na korosho hizo thamani yake ni Sh 10,000 kwa kilo.
 “Badala ya kuuza korosho Sh 10,000 natengeneza siagi kilo moja na kuuza Sh 20,000,nikitoa gharama za uzalishaji bado nitakuwa na faida, na nikitumia kilo moja hiyo hiyo ya korosho nina uwezo wa kupata maziwa takribani lita tatu ambazo nitaziuza Sh 25,000,”anasema
Kuhusu madaraja ya korosho,Kaimu Mkurugenzi Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele, Dk Fortunatus Kapinga anasema kwenye saizi ya mbegu kiutafiti wamefanikiwa kuwa na mbegu ambazo zina ukubwa unaostahili  kwenye soko kwa maana zinazokidhi daraja kubwa na kuvutia wanunuzi kutoka nje.
Anafafanua daraja la mbegu 500 nchini hazipo na badala yake zipo zinazokidhi daraja kubwa la mbegu 180 huku zile za daraja la 450 zikiwa ni chache sana na ndizo hutengenezea maziwa na siag.
“Korosho za Tanzania zina ubora wa kimataifa unaokubalika kwa sababu tuna mbegu ambazo tumezizalisha na tumezigundua zina sifa za soko la kimataifa na ndio maana tunahimiza wakulima wetu wapande mbegu bora kutoka Naliendele il tunapoenda kwenye ushindani soko lolote la kimataifa hakuna anayetushinda,”anasisitiza Dk Kapinga
Anafafanua kutokana na baadhi ya watu kama watoto kushindwa kutafuna korosho au kuwa na mzio (allergy) ya maziwa ya ng’ombe ndio sababu za wao kuwa na utafit wa maziwa ya korosho.
Upatikanaji wa malighafi
Msoka anasema malighafi wanazotumia kutengeneza mvinyo,jam na juisi hupatkana katika mashamba yao ya utafiti huku korosho zinazotengenea ,maziwa na pinetbutter hutokana na korosho zinazobanguliwa katika kiwanda kilichopo kwenye taasisi hiyo kwa ajili ya utafiti.
Mwakilishi wa mkurugenzi mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) Dk Bakari Msangi anasema kwa kuwa Taasisi ya Utafiti wa kilimo Naliendele imeshafanya utafiti na kuthibitisha teknolojia inayoweza kutumika watu wachangamkie fursa.
Anasema wafanyabiashara wakubwa wanatakiwa kuona fursa na kuweka viwanda katika mikoa inayozalisha korosho kwa kuanzisha viwanda vitakavyozalisha bidhaa zitakazotokana na mabibo.
“Wanachotakiwa ni kuona tayari katika level ya research tumeprove teknolojia kwamba inaweza na tumeshatoa product zinazoingia sokoni, kwa hiyo tunawavutia wawekezaji wa ndani na nje waone umuhimu wa kuweka viwanda,”anasema Dk Msangi
Hata hivyo, anasema kwa kuwa sasa ni uchumi wa viwanda hawawalengi tu wajasiriamali wadogo, bali wafanyabiashara wakubwa na watunga sera wote.
“Watu wote wanaoongelea sera za nchi wajitahidi kuitangaza teknolojia hii ambayo imeshahakikiwa na Naliendele kuhamasisha watu kuwekeza katika maeneo yanayozalisha korosho ili kutumia hii product (bidhaa) ambayo inapotea,ni potential area,”amesema Dk Msangi
Wakulima
Mkulima Elisha Millanzi anasema katika msimu mmoja ana uwezo wa kupata korosho tani mbili hadi tatu na mabibo yatokanayo na korosho hizo hutengeneza juisi ya kunywa wawapo shmbani na yanayosalia ambayo ni mengi huyateketeza kwa moto pindi yanapokauka.
Pia, anasema wapo baadhi ya watu huyatumia kutengenezea pombe maarufu kama ulaka pindi yanapokuwa mabichi na hutumika katika familia na hutumika kama burudani ya familia na wengine huyakaush na kutengenezea pombe ya gongo ambayo hairuhusiwi.
“Unapokula bibo linakuwa na asili ya sukari, mara nyingi tunakamua na kuchuja na kunywa bila hata kuweka sukari wala kuongeza maji, hata kama uko shambani umekosa maji ya kunywa unayakamua na kunywa,”anasema Millanzi
“Kama serikali ikituletea viwanda vya kutengeneza bidhaa nyingine itakuwa imetusaidia kwa sababu tunatupa rasilimali nyingi, mtu akivuna tani kumi ina maana kila korosho moja ilikuwa na bibo lake moja hapo mabibo na yenyewe ni tani kumi au zaidi,”
Mikakati iliyopo
Mbunge wa Tandahimba, Katani Katani anasema baadhi ya wakulima hutengeneza pombe asili ya gongo ambayo haina viango na hairuhisiwi nchini na hivyo kupelekea mabibo mengi kuteketezwa.
Anasema utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa kilimo Naliendele unahitaji mashine zitakazotakiwa kufanya uzalishaji.

“Bahati nzuri waziri wa kilimo tulifika naye Naliendele anajua mabibo yanaweza kutengeneza mvinyo, kwa hiyo tunajaribu kuangalia namna iliyo sahihi tuweke kwenye sera ya kuona hilo jambo linaweza kuwanufaisha wakulima kwa namna nyingine,”anasema Katani

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger