Mkazi wa Kata ya Buhalahala mjini Geita, Magreth Digugulo, anadaiwa kumchoma moto na kisha kumkatakata na wembe mjukuu wake kwenye mkono wa kulia kwa madai ya kukomba mboga.
Mtoto huyo (jina linahifadhiwa) alizungumza na Nipashe jana nyumbani kwao alitaja sababu za kufanyiwa kitendo hicho kuwa ni kujipakulia mboga aina ya kisamvu.
Alisema siku ya tukio, hakuwa amekwenda shuleni ila hakuwapo nyumbani na baada ya kurudi alipakua mboga kidogo akala na baada ya bibi yake kurudi, alimwita na kumkaripia ndipo akamchoma moto na kumkatakata vidole na wembe.
"Sikuwa nimeenda shuleni siku hiyo. Baada ya kutoka kucheza nilikuja nyumbani kula, sikumkuta bibi hivyo nikajipakulia mboga kidogo nikala. Bibi aliporudi akasema nimekomba mboga ndiyo akanifanyia hiki kitendo," alisema.
Baadhi ya majirani ambao walishuhudia tukio hilo, akiwamo Ayoub Bwanamadi, ambaye ni Mratibu wa Mtandao wa Marafiki wa Elimu, alisema walipata taarifa za tukio hilo na baada ya kusogea eneo la tukio, walitafuta namna yakumsaidia mtoto huyo.
Kwanza, alisema walitaka kujua nini chanzo cha tatizo na walimuuliza bibi yake akawajibu mtoto amekomba mboga ndiyo maana amemchoma moto.
Alisema tabia hiyo inaonekana imezoeleka kwa bibi huyo kutokana na mtoto kuonekana na majeraha mengine makubwa kwenye mwili wake ambayo yamekwisha pona.
"Hali ilivyo kwa huyu mtoto ni kama matukio haya ni ya kujirudia. Ukitazama kwenye kiganja cha mkono wake kuna kovu moja na mtoto anavyodai bibi alishawahi kumchoma kwenye majivu kabla ya tukio hili," alisema Bwanamadi.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Kata hiyo, Neema Emmanuel, alisema alipokea taarifa ya tukio hilo na kumpeleka mtuhumiwa polisi kisha kumpeleka mtoto hosptalini kwa ajili ya matibabu.
"Mwezi huu wa tano (Mei) matukio kama haya yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara. Hili ni tukio la nne kutokea kwenye kata yangu, mengine tumeshayafikisha kwenye ngazi husika. Hata hivyo tunawashukuru wananchi wamekuwa wakitoa taarifa za matukio haya," alisema.
Babu mzazi wa mtoto huyo, Stephano Matata, alisema tukio hilo limemsikitisha kutokana na mtoto huyo kutokuwa na msaada wowote wa malezi ya wazazi wake kwa kuwa anaishi na bibi yake kwa sababu mama yake mzazi ameshatokomea kwenye machimbo huku baba akiwa hajulikani ni nani.
"Mimi huwa sikai hapa nyumbani, lakini nilivyopata taarifa hizi zilinisikitisha kwani huyu mtoto ni kama hana wazazi. Mimi nitamchukua nikae naye kwa sababu hana msaada mwingine," alisema Matata.
Kutokana na kitendo hicho, bibi huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili kuhojiwa kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria.
0 comments:
Post a Comment