Bunge la
bajeti linaanza kesho huku Serikali ikiwa imetoa mwelekeo wa bajeti ya
mwaka wa fedha wa 2014/15 kuwa ni Sh19.6 trilioni, ikilinganishwa na
Sh18.2 za Bajeti iliyopita.
Vipaumbele
vya bajeti hiyo ni kuendeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
ulioanza mwaka 2011 na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambao
unajumuisha maeneo sita ya kitaifa ya kilimo, elimu, maji, utafutaji wa
rasilimali fedha, nishati, uchukuzi na uboreshaji wa mazingira ya
kufanyia biashara.
Kwa
mujibu wa Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, matumizi ya kawaida kwa mwaka
ujao wa fedha yanalenga kufanikisha mambo 20 muhimu, yakiwamo Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa mwaka 2014, Uchaguzi Mkuu 2015, kukamilisha
mchakato wa Katiba na nyongeza ya mishahara na kulipa kwa wakati.
Waziri
huyo alisema makadirio ya matumizi ya maendeleo ni Sh7.7 trilioni sawa
na asilimia 39 ya matumizi yote ya Serikali na kati ya fedha hizo miradi
ya maendeleo imetengewa Sh5.4 trilioni sawa na asilimia 27 na matumizi
mengine ya maendeleo ni Sh2.2 trilioni.
Pia
alisema katika mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali imekusudia kukopa
Sh4.2 trilioni kutoka vyanzo vya mapato vya ndani na nje ili kuziba
pengo la mapato.
Serikali
imetenga Sh5.4 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo na imeonyesha
vipaumbele vyake vikuu katika miradi hiyo ya maendeleo ni kilimo, elimu,
maji, utafutaji wa rasilimali fedha, nishati, uchukuzi na uboreshaji wa
mazingira ya kufanyia biashara huku michezo ikikosekana katika
vipaumbele hivyo.
Sisi
tunaamini sekta ya michezo ilistahili kuingizwa katika vipaumbele vya
Serikali katika bajeti yake ya 2014/15 kwani sekta hii ikitengewa fedha
nyingi na kuwekewa misingi imara ni chanzo kikubwa cha mapato.
Tumeshuhudia
katika nchi mbalimbali duniani ambazo Serikali zao zinaithamini sekta
ya michezo kwa kuitengea bajeti kubwa ya miradi ya maendeleo,
wanamichezo wa nchi hizo wamekuwa wakinufaika na kupata mapato makubwa
na hivyo kulipa kodi kubwa ambazo zimekuwa ni chanzo kikubwa cha mapato.
Ni wazi
ukiangalia kwa undani nchi zote zilizoendelea katika michezo utaona kwa
nanma moja au nyingine kuna nguvu nyingi za Serikali za nchi hizo hasa
utagundua Serikali za nchi zao hutoa fedha na kuboresha miundombinu ya
michezo ili kuweza kuwa na programu nzuri za kuendeleza michezo na
husaidia timu zao za taifa.
Tunaamini
kwamba hata kama mapato ya nchi ni madogo, Serikali ikiwa na dhamira ya
dhati ya kupenda michezo na kuipa kipaumbele, haitashindwa kupata
vyanzo mbalimbali vya mapato kwa ajili ya kuhakikisha sekta ya michezo
inakuwa katika vipaumbele vya bajeti na kutengewa fedha za kutosha kwa
ajili ya miradi ya maendeleo.
Inaeleweka
kuwa Tanzania tuna bahati ya pekee duniani kwani tuna utajiri mkubwa wa
rasilimali ambazo kama kama zitatumika ipasavyo zitanufaisha sana taifa
letu na wanamichezo wetu watapata vifaa vya michezo kwa bei nafuu,
viwanja vya michezo na walimu bora wa michezo.
Hata
hivyo katika hali ya kushangaza utajiri huo wa rasilimali umekuwa
ukionekana kunufaisha wachache huku hali hiyo ikionekana kama ni jambo
la kawaida. Tunatarajia wabunge watatuunga mkono na kuisimamia Serikali
ipasavyo katika kuhakikisha kuanzia Bunge hili la bajeti sekta ya
michezo inatambuliwa na kutengewa fedha nyingi katika miradi ya
maendeleo.(CHANZO: MWANANCHI) (FS)
0 comments:
Post a Comment