Thursday 29 May 2014

KUDAI TANGANYIKA KULIANZIA BUNGENI 1993 - 5

...
Tulieleza jinsi wabunge 55 walivyotaka kuirudisha Serikali ya Tanganyika na jinsi baadhi yao ‘walivyonyamazishwa’ kwa kupewa uwaziri na Mwalimu Julius Nyerere alivyozima hoja.

Tuliona pia maoni ya Nyerere kwamba lengo lake lilikuwa ni kuwa na serikali moja Tanzania. Wazanzibari wako wazi hata leo, wanapinga muundo wa muungano wa serikali moja na badala yake wanataka ule wa serikali tatu na wengine mbili.
Sababu kubwa inayowafanya Wazanzibari wakatae muundo huo wa serikali moja ni kwamba wanadai Zanzibar ilikuwa na serikali yake kamili wakati muungano ulipofanyika Aprili 26, 1964.
Nikweli kabisa, tangu Januari hadi Aprili 1964 Zanzibar ilikuwa nchi huru (Sovereign State) ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Mnamo Aprili 6, 1964 Zanzibar ilikuwa imefungua balozi tatu; London, Uingereza alikuwepo Othman Shariff; Cairo, Misri alikuwepo Dk. Salim Ahmed Salim (pichani) na New York, Marekani alikuwepo Hasnu Makame.
Waziri wa Mambo ya Nje alikuwa Profesa Abdulrahman Mohammed Babu.
Pia nchi 17 zilikwishaitambua Zanzibar kama nchi huru hadi kufikia Aprili 26, 1964. Nchi hizo na tarehe za kutambuliwa katika mabano ni Ghana (28/1/1964), Cameroon (30/1/1964), German Democratic Republic (GDR) (30/1/1964), Poland (30/1/1964) na Israel (1/2/1964).
Zingine ni Misri (4/2/1964), Urusi (4/2/1964), China (6/2/1964), Czechoslovakia (18/2/1964), Algeria (18/2/1964), India (22/2/1964), Uingereza (24/2/1964), Marekani (24/2/1964), Mali (26/2/1964), Congo-Brazzaville (26/2/1964), Ceylon (26/2/1964) na Liberia (29/2/1964).
Nchi tisa zilikwishafungua balozi zao Zanzibar kabla ya muungano. Nchi hizo ni Ghana, GDR, Israel, Urusi, China, Uingereza, Vietnam, Marekani na Ufaransa.
Zanzibar pia tayari ilikuwa mjumbe katika Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Jumuiya ya Madola na Umoja wa Mataifa (UN), mnamo Aprili 6,1964, na ilikuwa inashirikishwa Unesco, ADB na mashirika mengine ya kimataifa.
Jambo la kujiuliza ni kuwa kama hoja ya msingi kwao ya kukataa serikali moja ni kwa vile wakati huo ilikuwa na serikali yake, mbona Tanganyika nayo ilikuwa na serikali yake kamili kabla ya muungano?
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger